Wafungwa, wakimbizi wanaweza kunufaika na fursa za kidijitali

Caroline Erikyasiima (kulia) akifafanua jambo kwa Mhariri wa Habari za Uchumi na Biashara wa Mwananchi, Julius Mnganga baada ya kufanya mahojiano kwenye ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL). Picha na Loveness Bernard

Machi 14 ilikuwa siku muhimu kwa Tanzania, hasa kwa Caroline Erikyasiima, mhandisi wa kompyuta, baada ya kushinda tuzo ya dunia ya ubunifu katika kutoa ajira za kidijitali.

Furaha ya Caroline, mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali la Apps and Girls, ilitokana na mafanikio makubwa aliyoyapata kwa kunyakua tuzo hiyo, kwani alishawahi kujaribu mara kadhaa bila mafanikio.

Kutokana na mradi wake wa Jovia unaotekelezwa na Apps and Girls kwa ufadhili wa kampuni ya Tigo kuwawezesha wasichana kunufaika na fursa za ujasiriamali zilizomo kwenye majukwaa ya kidijitali, Tanzania ilishinda tuzo ya ajira za kidijitali (e-employment) iliyotolewa na Mkutano wa Dunia wa Jamii ya Teknolojia (WSIS) jijini Geneva, Uholanzi.

“Hizi ni tuzo kubwa duniani. Tumeliheshimisha Taifa na kujitambulisha mbele ya jamii kwa namna ya pekee. Kila mmoja sasa ataona na kutambua kwamba tunachokifanya ni cha maana. Tunawashukuru sana Tigo kwa kutuwezesha kuwainua wasichana nchini,” anasema Caroline, akiizungumzia tuzo hiyo iliyoandaliwa kwa WSIS kushirikiana na Shirikisho la Mawasiliano Duniani (ITU) pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya Unesco, UNDP na UNCTAD kuhamasisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kufanikisha maendeleo endelevu ya dunia (SDG).

Ingawa Apps and Girls imekuwapo nchini tangu mwaka 2014, programu ya Jovia ilianzishwa mwaka 2018, ikiwafundisha wasichana wenye umri kati ya miaka 17 mpaka 24 walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ujuzi wa kutengeneza tovuti, uundaji wa programu za kwenye simu (mobile apps), uuzaji wa bidhaa au huduma mtandaoni, ujasiriamali, upigaji picha na kusanifu habari (graphics designing).

Kozi hizo zinazofundishwa kwa kati ya mwezi mmoja mpaka miezi sita, zinalenga kuwawezesha wahitimu kujiajiri kutokana na maarifa waliyoyapata na Caroline anajivunia kuona amelifanya hilo kwa kuwawezesha zaidi ya wasichana 270 mpaka sasa.

Caroline, aliyekuwa mhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) kabla hajaamua kujiondoa huko ili ajiajiri, anasema kwa muda wote aliofundisha, ilikuwa akiingia darasani anaona kuna wanaume wengi kuliko wanawake, hivyo akapata hamasa ya kuwawezesha wasichana nao kusoma masomo hayo ya sayansi.

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia yaliyopo duniani kwa sasa, anasema hakuna namna mtu anaweza kujitenga na uchumi wa kidijiti, hivyo huwa anaumia kuona wasichana wanayakimbia masomo ya sayansi kutokana na sababu zisizo na ukweli wala uhalisia.

“Hapa Apps and Girls tunawafundisha watu waliofeli au kuacha shule kutokana na kupata ujauzito au kukosa ada au sababu nyingine yoyote. Jamii inayaogopa masomo ya sayansi na wasichana wanaambiwa hawayawezi, lakini wakija hapa wanafaulu vizuri tu na kwenda kuyatumia maarifa hayo mtaani,” anasema Caroline.

Kwa siku zijazo, anasema watu wenye ujuzi wa kuzitumia fursa za kidijitali watahitajika zaidi, hivyo ni muhimu kwa Serikali kushirikiana na sekta binafsi kuweka mazingira ya kuwaandaa vijana bila kubagua jinsi kwa kuwapa maarifa hayo.

Katika kuhakikisha wasichana wanayaelewa na kutoyaogopa masomo hayo tangu wakiwa wadogo, Caroline alianzisha klabu za kusimba (coding clubs) ambazo kwa sasa zipo 73 katika shule za sekondari kwenye mikoa 15 ya Dar es Salaam, Morogoro, Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Dodoma, Iringa, Tabora, Shinyanga, Unguja na Mbeya.

Iwapo wasichana watapewa fursa na kuhamasishwa kusoma masomo ya sayansi, Caroline anasema jamii itanufaika zaidi, kwani uwezo wao ni mkubwa.

“Mwaka 2020 tulishiriki kwa mara ya kwanza tuzo za WSIS tukaishia tano bora na mwaka uliofuata hatukufika popote, ila mwaka huu tumebeba tuzo hii kubwa baada ya dunia kuona tunachokifanya kwa wasichana. Kati ya vigezo muhimu vilivyotubeba ni kuwawezesha vijana kuchangamkia fursa za kidijitali. Huu ndio uelekeo wa dunia, ITU inazo programu kadhaa zinazojielekeza huko,” anasema Caroline.


Fursa kwa vijana wote

Ingawa Apps and Girls imewalenga zaidi wasichana, Caroline anasema vijana wote wanayo nafasi ya kujifunza na kujiajiri kidijitali, hivyo wanaangalia namna ya kuwafikia wengi zaidi.

Kwa kuwa ofisi yake haiwezi kuwafikia Watanzania kote nchini, anasema wanatamani kushirikiana na Serikali ili kozi wanazozitoa ziwe zinafundishwa kwenye vyuo vya Veta.

“Sio tu tukishirikiana nao vijana wengi watapata maarifa haya, bali wahitimu tunaowatoa vyeti vyao vitatambulika na kukubalika kwa waajiri popote watakapoomba kazi,” anasema Caroline.

Vilevile, anasema kozi wanazozifundisha zinaweza kuwafaa wakimbizi waliopo kwenye makambi mkoani Kigoma pamoja na wafungwa wanaotumikia adhabu zao kwenye magereza yaliyoenea kote nchini.

“Wakimbizi na wafungwa ni makundi yanayoweza kunufaika na ujuzi wa kidijitali. Iwapo wafungwa watatengenezewa mazingira ya kuelimishwa, watakuwa na cha kufanya wakimaliza vifungo vyao hivyo kuwa watu wema watakaporudi mtaani. Tukiruhusiwa, tutafurahi kuwafundisha,” anasema Caroline.

Iwapo vijana kutoka makundi yote watajengewa uwezo kwa kupata maarifa haya, Caroline anasema itakuwa rahisi kwa Tanzania kushindana kimataifa kwa kutoa wataalamu wa Tehama wanaoweza kuzalisha programu zenye viwango vinavyokubalika.

“India inatoa wataalamu wengi wa Tehama kwa sababu vijana wao wanao ujuzi unaohitajika. Ukitaka wakutengenezee programu ya kwenye simu kwa mfano, watahitaji siku chache tu kukukabidhi unachokihitaji. Tunaweza kufika huko iwapo wadau muhimu watashirikishwa,” anasisitiza.


Tigo kuwezesha zaidi

Ofisa Mkuu wa Udhibiti wa Tigo, Sylvia Balwire anasema ufadhili waliotoa kwa Apps and Girls ni sehemu ya mpango wao wa uwajibikaji kwa jamii uliowalenga wasichana na vijana.

Anasema siku zote, Tigo imekuwa ikilenga kumwezesha mtoto wa kike kwa kumpa fursa ya kujumuishwa kidijitali nchini na ushindi huo unadhihirisha dhamira ya dhati waliyonayo kuwawezesha Watanzania katika nyanja tofauti za kiuchumi na kijamii.

“Tumejitolea kuwa kampuni ya kwanza ya kidijitali na tuzo hii ya kimataifa ni kielelezo cha mafanikio tuliyoyapata Tanzania nzima katika kuwawezesha wasichana na wanawake vijana wasiojiweza. Mwaka huu tunaadhimisha miaka mitatu ya kuunga mkono kifedha na kiufundi mradi wa Jovia unaowawezesha wasichana. Kwa tuzo hii tuna msukumo wa kuendelea kuwakuza wasichana zaidi katika anga ya kidijitali,” amesema Sylvia.

Mpango wa Jovia, anasema ulitambuliwa mwaka 2019 ili kushughulikia mgawanyiko wa kijinsia katika sekta ya kidijiti kwa kutoa mafunzo ya Tehama na ujasiriamali ili kuwalea wasichana na wanawake vijana chipukizi wasiojiweza nchini.

Kupitia programu ya Jovia, Sylvia anasema Tigo imewafikia na kuwawezesha wasichana na wanawake 14,965 kwa kuwapa ujuzi na kuendeleza teknolojia ya habari na ujasiriamali ili kuunda miradi inayoendeshwa na teknolojia, kuanzisha miradi yao ya teknolojia na kupata ajira rasmi katika sekta ya Tehama.