Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Abiria wa Precision Air walalamikia kukwama Kia kwa zaidi ya saa 24

Muktasari:

  • Mpaka sasa abiria hao zaidi ya 20 wamekwama katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) tangu Juni 8, huku baadhi yao ambao walikuwa wanakwenda kwa matibabu, usaili na wengine kwenye shughuli za kichungaji wakishindwa kuendelea na safari zao.

Moshi. Baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri na ndege ya Kampuni ya Precision Air kutoka Mwanza kwenda Nairobi, Kenya, wameshindwa kuendelea na safari zao kwa zaidi ya saa 24 kutokana na madai kwamba ndege waliyotarajia kusafiria imepata hitilafu ya kiufundi.

Abiria hao zaidi ya 20 wamekwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) tangu Juni 8, 2026. Baadhi yao walikuwa wakielekea nchini Kenya kwa matibabu, usaili wa kazi na shughuli za kichungaji.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Meneja wa Masoko na Mawasiliano wa Precision Air, Hilary Mremi, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema jitihada zinaendelea kuhakikisha abiria wote wanafika walikokusudia.

“Ni kweli tumepata changamoto ndogo ya kiufundi, lakini tangu jana tumekuwa tukitafuta njia mbadala kwa abiria wetu. Hivi sasa tunaendelea na jitihada za kuwawezesha waliobaki kuendelea na safari zao. Wapo ambao tayari wamepangiwa ndege nyingine, na tunaendelea kushughulikia changamoto hii ili kuhakikisha abiria wote wanafanikisha safari zao kama walivyopanga,” amesema Mremi.

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa abiria hao, Shedracky Kilimba, amesema tangu walipotua KIA jana bado hawajafanikiwa kuendelea na safari, huku maelezo wanayopewa na wahusika yakishindwa kuwapa ufafanuzi wa kuridhisha.

“Tangu jana tulikaa muda mrefu katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Tulitarajia kuondoka saa 7 mchana lakini tuliondoka karibu saa 1 kasorobo usiku. Tulipofika KIA tukaambiwa ndege ya kwenda Nairobi ilikuwa tayari imeondoka, hivyo tukapelekwa hotelini. Leo asubuhi tuliambiwa tuwahi kwa safari ya saa 12, lakini baadaye tukaelezwa kuwa ndege imejaa. Tulipohoji tukaambiwa tusubiri hadi jioni. Wakati huo huo, tumekuwa tukiwapigia simu wahusika bila mafanikio kwani hawapokei kabisa,” amesema Kilimba.

Naye, Farid Habibu, aliyekuwa akisafiri kwenda nchini Kenya kwa ajili ya usaili wa kazi, amesema changamoto hiyo imemkwamisha kutimiza lengo lake.

“Nilipaswa kusafiri leo saa 12 asubuhi, lakini nilipofika hapa nikaambiwa hakuna nafasi ya kusafiri. Wale wa jana bado hawajaondoka na tuko pamoja nao hapa. Hali hii inatuathiri kwa sababu kila mmoja ana mipango yake. Mimi nilikuwa na usaili wa saa tano asubuhi leo, lakini nimeshindwa kufika. Pia kuna baadhi ya wenzetu waliokuwa na miadi ya matibabu na tayari muda wao umepita,” amesema Habibu.

Abiria mwingine, Agundason Dominic, amesema ucheleweshaji huo umesababisha washindwe kushiriki mafunzo muhimu yaliyowapeleka Kenya.

“Jana tulitarajia kuondoka Mwanza saa 9 alasiri, lakini ndege ilifika karibu saa 2 kasorobo usiku. Tulipofika KIA hatukupata safari ya kuendelea. Mafunzo tuliyopaswa kushiriki yalianza jana na leo pia tutashindwa kuhudhuria, jambo ambalo linaweza kuonekana kana kwamba tumefanya makusudi. Hata leo tunaambiwa tutalala tena hapa bila uhakika wa kuondoka,” amesema Dominic.

Kwa upande wake, Hilary Mshana, ambaye alikuwa akisafiri kwenda Nairobi kwa ajili ya kumuona daktari wake, amesema amesikitishwa na usumbufu huo.

“Nilikuwa na miadi ya kumuona daktari wangu, lakini nimeshindwa kusafiri. Tangu jana kulikuwa na ucheleweshaji wa safari kutoka Mwanza hadi KIA, ambapo muda wa kuondoka ulisogezwa mbele mara kadhaa. Inaonekana kulikuwa na changamoto kubwa. Kutokana na kushindwa kufika kwa wakati kwenye miadi yangu ya hospitali, nimeathirika kisaikolojia na kujisikia vibaya sana,” amesema.