Akiba fedha za kigeni inavyopaa katikati ya uhaba Dola

“Upatikanaji wa Dola ni mtihani mkubwa, hivi sasa nikitaka kuagiza mzigo nje najipa kwanza miezi kama miwili hivi ili kukusanya Dola 30,000 ninazozihitaji, nakusanya kila siku kidogokidogo kwa njia tofauti,” anasema Fadhili Joseph, muuzaji wa vipuri vya magari.

Kilio cha upatikanaji wa Dola kiko kila mahali katika mataifa mengi ambayo yanategemea sarafu hiyo ya Marekani katika kufanya manunuzi ya bidhaa zao muhimu. Inatajwa kuwa Dola inatumika katika asilimia 86 ya miamala yote duniani.

Hapa nchini tayari vilio vimesikika kutoka kwa wauzaji wa bidhaa zitokazo nje ya nchi kama mafuta na nyinginezo, lakini pia wauzaji ambao bidhaa zao huuzwa kwa dola, mfano tumbaku. Hali ya upatikanaji wa Dola kwa ujumla ni mbaya.

Hata hivyo, katikati ya changamoto ya uhaba wa Dola unaoendelea kutikisha kwa takribani miaka miwili, ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwenendo wa uchumi wa kila mwezi (MER) inaonyesha ukuaji wa akiba ya fedha za kigeni uliotajwa kufikia Sh13.84 trilioni katika mwaka ulioishia Desemba, 2023 ikilinganishwa na Sh12.95 trilioni katika mwaka ulioishia Desemba 2022.

Agosti 2023, Mkurugenzi wa masoko ya fedha wa BoT, Alexander Nwinamila aliliambia gazeti hili kuwa katika fedha za kigeni zilizokuwa zimehifadhiwa na BoT, asilimia 77 zilikuwa ni Dola za Kimarekani, asilimia 16 Yuani ya China, asilimia 4.78 Pauni ya Uingereza na Asilimia 1.72 Dola ya Australia.

Ongezeko la uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na kupungua kwa uingizaji wa bidhaa kutoka nje kulikoshusha nakisi katika urari wa biashara pia inaweza kuwa chanzo cha ongezeko la akiba ya fedha za kigeni.

Kiwango cha akiba ya fedha za kigeni kilichopo kinatajwa kuwa kina uwezo wa kuhudumia manunuzi ya bidhaa za nje kwa kipindi cha miezi minne na nusu, ambayo ni juu ya kiwango kilichowekwa cha miezi minne.

Akizungumzia ufanisi huo, Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba anasema miongoni mwa mambo yaliyoongeza akiba hiyo ni mikopo ya nje na uamuzi wa Serikali kununua dhahabu kisha kuzitunza kama sehemu ya akiba ya fedha za kigeni.

“Tulinunua dhahabu kwa Shilingi kisha tukazitunza kama fedha za kigeni, lakini pia katika kipindi husika (mwaka 2023) tulipata mikopo kutoka Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF),” anasema Tutuba, akieleza siri ya kukua kwa hifadhi ya fedha za kigeni.

Kuhusu kupungua kwa thamani ya bidhaa zinazonunuliwa na nchi kutoka nje ya nchi, Tutuba anasema hayo ni matokeo ya kuadimika kwa Dola, mikakati iliyoanzishwa na Serikali ya kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

“Kutokana na upatikanaji wa Dola kuwa mgumu, baadhi ya bidhaa zinazoweza kuzalishwa hapa nchini uzalishaji wake uliongezeka, mfano mafuta ya kupikia utegemezi wake ulipungua kutokana na mikakati ya kuongeza uzalishaji wa ndani. Vifaa tiba kama glovu, dripu na baadhi ya dawa sasa vinazalishwa hapa nchini,” anasema Tutuba.

Vilevile anasema kuna bidhaa zilipanda bei zaidi mwaka 2022, baada ya kuanza kwa vita vya Russia na Ukraine, lakini mwaka 2023 bei yake ilipungua, huku kiwango kinachoingizwa kikiwa kilekile, hali iliyosababisha kupungua kwa thamani ya kuagiza bidhaa nje ya nchi.

Kadhalika anasema pamoja na bidhaa kupungua bei, pia sehemu kubwa ya thamani ya bidhaa zilizoagizwa mwaka 2022 ilitokana na mitambo ya utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na vitu hivyo havikuagizwa kwa wingi mwaka 2023.

Aidha, Tutuba anasema matumaini yaliyopo ni kuendelea kupungua kwa utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kutuna kwa mfuko wa akiba ya fedha za kigeni, akisema kuna upanuzi na ujenzi wa viwanda vya mbolea unafanyika, lakini pia matumizi ya gesi iliyokandamizwa, jambo ambalo litapunguza thamani ya fedha zinazotumika kuagiza mbolea na mafuta kwa ajili ya magari.

“Kwa kawaida urari wa biashara hubadilika badilika, lakini tuna imani nakisi yetu kati ya kuuza na kununua nje ya nchi itaendelea kupungua. Uzalishaji wa mbolea unaenda kuongezeka, lakini sasa hata daladala na bajaji zinafunga mifumo ya gesi, jambo ambalo linapunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi,” anasema Tutuba.

Kuhusu kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi kupungua kwa utegemezi wa bidhaa kutoka nje, ripoti ya MER inaonyesha nakisi iliyopo katika urari wa biashara kati ya Tanzania na mataifa ya nje umepungua kutoka Sh13.6 trilioni hadi Sh7.23 trilioni.

Katika mwaka husika Tanzania iliuza nje ya nchi bidhaa zenye thamani ya Sh35.48 trilioni, huku ikinunua bidhaa na huduma zenye thamani ya Sh40.76 trilioni.

Kupungua kwa nakisi hii katika urari wa biashara kumechangiwa na kuongezeka kwa mauzo ya nje katika bidhaa mbalimbali kwa asilimia 16.6, huku uingizaji wa bidhaa kutoka nje ukishuka kwa asilimia 3.6.

Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya uchumi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Desemba 2023, mauzo ya bidhaa na huduma nje yaliongezeka hadi kufikia thamani ya Sh35.48 trilioni, huku mauzo ya dhahabu, bidhaa za asili na huduma vikiongoza.


Sekta zilizofanya vizuri

Uuzaji wa bidhaa zisizokuwa za asili ulikuwa kwa asilimia 4.3 hadi kufikia Sh16 trilioni ambayo ilichochewa zaidi na kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu nje ya nchi ikifuatiwa na mauzo ya bidhaa za viwandani.

Mauzo ya dhahabu yalikua hadi kufikia Sh7.77 trilioni ikilinganishwa na Sh7.186 trilioni zilizokuwapo mwaka ulioishia Desemba 2022 huku kiwango cha dhahabu kilichouzwa na gharama yake vikitajwa kuwa sababu ya ongezeko hilo.

Sekta ya huduma nayo ilifanya vizuri hadi kufikia thamani ya Sh15.919 trilioni kutoka Sh12.071 trilioni katika mwaka ulioishia Desemba 2022 huku ikichochewa zaidi na utalii na usafirishaji huku sekta ya utalii ikichangia kiasi kikubwa kwa Sh8.53trilioni.

Aidha wakati nuru iking’aa katika mauzo ya nje, kama nchi pia ilipunguza thamani ya bidhaa ilizoziagiza kutoka nje ya nchi kwa kipindi husika kutoka Sh42.34 trilioni hadi Sh40.7 trilioni Desemba mwaka jana.
Uagizaji wa mafuta kama ulivyotajwa na Gavana ulipungua kutoka Sh8.4trioni kwa mwaka ulioishia Desemba 2022 hadi Sh6.9 trilioni Desemba 23.


Wasemavyo wachumi

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora anasema kuongezeka kwa mauzo ya nje ni ishara ya kukua kwa uchumi kwa sababu kama nchi inahitaji sana kuuza nje kuliko kununua, jambo litakaloongeza fedha za kigeni zinazohitajika.

“Hata katika utalii watu wanapokuja na kutumia huduma zetu, wakaleta fedha za kigeni nayo ni kuuza bidhaa nje ya nchi, huku nako tumefanya vizuri zaidi, hii ni namna ambayo uchumi unapaswa kuendeshwa kwa kuangalia namna ambavyo vitu vyetu vinapata masoko nje,” alisema Profesa Kamuzora.

Katika hilo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti na Sera (REPOA), Dk Donald Mmari anasema kadiri nchi itakavyokuwa na uwezo wa kuzalisha na kuuza nje ndivyo itakavyokuwa inakuza uchumi wake.

“Kadiri unavyoweza kuzalisha na kuuza nje, uchumi wako unaanza kukua kwa kasi, hasa unapouza zaidi ya unavyonunua, hii ni dalili za maendeleo katika nchi,” anasema Dk Mmari.

Hata hivyo, anasema kuna hatari ikiwa nchi itaendelea kutegemea dhahabu kama bidhaa kuu inayoleta fedha nyingi za kigeni kila wakati, huku akiweka angalizo kuwa inaweza kuwa na athari ikiwa mabadiliko yatatokea katika masoko yanayouza bidhaa hiyo. “Ni vyema kuongeza wigo wa bidhaa zinazouzwa nje, kuangalia mazao mengine yanayoweza kuleta fedha za kigeni, kuongeza thamani katika mazao kwa kuacha kuuza bidhaa ghafi, kuzalisha zaidi bidhaa ambazo zina soko nje,” anasema Dk Mmari.


Nini kifanyike

Profesa Kamuzora anasema ni vyema kuangalia namna ya kuongeza nguvu katika uzalishaji bidhaa, huku akiitaka Serikali kuangalia namna inavyoweza kutoa ruzuku katika viwanda vinavyodorora.

Anasema kuna viwanda vilivyoathiriwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona (Uviko-19) hadi sasa havijarudi katika uzalishaji wake, huku njia ya ruzuku pekee akiitaja kuwa ndiyo inayoweza kuvihuisha.

“Tuanze kuwekeza kwenye kukopesha wazalishaji, watu wa kilimo wanaotengeneza mashine za kubangua kahawa, korosho hii inaweza kututoa,” alisema Profesa Kamuzora.

Dk Mmari anasema ili kuendelea kupunguza nakisi katika biashara, ni vyema kushughulikia changamoto za kisera na miundombinu, ikiwemo nishati kwa kuimarisha upatikanaji wake.

“Ukiimarisha upatikanaji wa nishati unaweza kuongeza uzalishaji na kushusha gharama za uzalishaji, kuchochea uzalishaji wa bidhaa ili tuweze kuingia katika masoko ya ushindani. Pia kuendelea kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa za ndani ili tusitegemee kuagiza nje, bidhaa kama sukari tuna wazalishaji wetu, tuna mashamba makubwa, tuna maeneo ambayo yanaweza kutumika katika uzalishaji,” anasema Dk Mmari.

Hilo linaungwa mkono na Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi ambaye anasema ni vyema kuweka mazingira yanayovutia wawekezaji na kupunguza vikwazo kwao.

“Hilo lifanyike kwa kuweka miundombinu mizuri inayohitajika, kama katika nishati tungeweza kutumia gesi yetu ili itumike katika mitambo na magari yetu, pia kitu kama chuma tunaagiza sana kutoka nje wakati tunayo nchini tungewekeza huko kwa sababu kuna miradi mingi tunayofanya inayohitaji malighafi hiyo,” anasema.