Dola yazidi kuwaliza wafanyabiashara

Muktasari:

 Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania kimesema ili kuficha wanachokifanya benki za kibiashara, hurekodi miamala hiyo kwa kiwango cha kubadilishia fedha kilichotangazwa na BoT pekee

Dar es Salaam. Tofauti ya bei ya kununua Dola ya Marekani inayotajwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) dhidi ya hali ya soko, imeleta kilio kwa wafanyabiashara wengi wanaofanya manunuzi nje ya nchi wakidai inaathiri bei na kuongeza mzigo wa uendeshaji katika biashara zao.

Akizungumza leo Februari 15 2024, mfanyabiashara wa nguo na viatu kutoka China, Ali Salehe, amesema, “viwango vya kubadilishia fedha hivi sasa wanasema ni Sh2,535 lakini nakwambia kwa bei hiyo huwezi kupata dola hata Sh2,550 haupati, ukienda benki hazipo ukikuta mtu anazo atakuuzia kwa Sh2,700 kwenda juu.”

Salehe amesema upatikanaji wa dola kwa njia halali (benki na maduka ya kubadilishia fedha) ni mgumu, hivyo wafanyabiashara wengi wanalazimika kununua kupitia masoko bubu (Black market), jambo linaloongeza bei ya sarafu hiyo.

Wakati Selehe akisema hayo, barua inayosambaa mtandaoni ya Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac) kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati nayo imebeba kilio hichohicho ikielezea tofauti ya viwango vya kubadilishia fedha inavyowaumiza katika uendeshaji.

“Katika tangazo la bei mpya ya mafuta kwa Februari, kiwango cha kubadilishia dola kilichotumika cha Sh2,574 ni kidogo ikilinganishwa na uhalisia wa soko, kwa jumla kuna uhaba wa dola katika masoko rasmi,” imeeleza sehemu ya barua hiyo ya Taomac.

Barua hiyo inaeleza hata pale wauzaji wa mafuta wanapofanikiwa kupata dola kutoka benki za biashara hawauziwi kwa kiwango cha kubadilishia kinachotangazwa na BoT, kwani hununua sarafu hiyo kwa faida ya muuzaji ya hadi Sh200.

Taomac walimweleza katibu mkuu kuwa ili kuficha wanachokifanya benki za kibiashara, hurekodi miamala hiyo kwa kiwango cha kubadilishia fedha kilichotangazwa na BoT pekee, huku faida yao ikifichwa na wakati mwingine kulipwa katika akaunti tofauti.

“Hali hii imesababisha wauzaji wa mafuta kununua dola katika masoko yasiyo rasmi kwa gharama ya hadi Sh2,800 na wanachama wamejitahidi kutafuta sarafu hiyo kwa nguvu zote, ili kuhakikisha hakuna upungufu wa mafuta,” inaeleza barua hiyo.

Wauzaji wamemweleza katibu mkuu kuwa kama si juhudi za wanachama wao, nchi ingeshakosa mafuta na wananchi kupata tabu na kusisitiza ukubwa wa changamoto hiyo kwa kusema: “Ewura (Mamlaka ya Nishati na Maji) haitambui masoko yasiyo rasmi, ndiyo maana ilikokotoa bei ya mafuta kwa kutumia Dola milioni 30 zilizopita kwenye masoko rasmi badala ya Dola milioni 250 ambazo ndiyo thamani nzima ya mahitaji ya soko."

Walipotafutwa Wizara ya Nishati kujua wanafanya nini kunusuru hali inayoelezwa na wauzaji wa mafuta baada ya barua hiyo iliyosambaa mtandaoni, Katibu Mkuu wake Felchesmi Mramba amesema wanaendelea kulifanyia kazi.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema viwango vya kubadilishia fedha vinavyotangazwa na taasisi hiyo ni kwa ajili ya soko la jumla (yaani BoT kwenda kwa benki za kibiashara).

“Sisi hatutangazi bei ya soko la rejareja, soko hilo linaendeshwa na mfumo wa soko huria ndiyo maana mwananchi wa kawaida hawezi kuja kwetu kununua dola,” amesema Tutuba.

Amesema kinachotokea ni kuwa bei ya jumla inasaidia kutoa mwelekeo wa mwenendo wa soko ndiyo maana hata unakuta tofauti ya viwango vyao na kwenye benki za biashara ni ndogo.

Tutuba amesema wakati mwingine kwa waagizaji wa bidhaa za nje ya nchi kinachoongeza gharama ya kupata dola ni kwa kuwa wanazikopa kutoka kwa taasisi za kifedha, hivyo kiwango wanachopewa kinakuwa kimebeba riba na maoteo ya viwango vya kubadilisha fedha kwa muda atakaorejesha.

“Yaani anaagiza mzigo kwa mkopo (letter of credit) anakopa leo, lakini anapewa maoteo ya viwango vya kubadilishia vya wakati wa marejesho (Forward rate) vyote hivyo vinafanya gharama zake za kufanya manunuzi kuwa kubwa,” amesema Tutuba.

Hata hivyo, amesema hali ya upatikanaji wa dola inazidi kuimarika tofauti na siku zilizopita, kwani mapato ya fedha za kigeni zitokanazo na shughuli za utalii yameongezeka kwa zaidi ya Dola bilioni tatu na baadhi ya bidhaa kama mbolea na mafuta ya kupikia utegemezi wake kutoka nje unapunguzwa.