Dola ilivyotikisa shughuli nyingi za kiuchumi nchini

Dar es Salaam. Siku chache zimebakia kabla ya kufunga kalenda ya mwaka 2023 unaoacha kumbukumbu ya maumivu makali katika mfumo wa maisha ya watanzania kupitia ongezeko la thamani ya Dola ya Marekani dhidi ya Shilingi katika shughuli za kiuchumi pamoja na kupanda marudufu bei ya mafuta katika soko la Dunia.

Mwezi Januari thamani ya dola ilikuwa Sh2,310 lakini hadi tunafunga mwaka huu, thamani ya dola imekuwa ikinunuliwa katika makadirio ya Sh2,520, sawa na ongezeko la Sh200 juu ya thamani ya Januari huku Benki ya Tanzania(BOT) ikikiri ukata wa sarafu hiyo iliyokuwa imeadimika kimataifa kutokana na sera za Marekani.

Kwa hivyo ulikuwa ni mwaka wa vikao vya majadiliano ya mara kadhaa kati ya wafanyabiashara, Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (Taomac) na BOT iliyobeba dhamana ya kunusuru changamoto hiyo kwa mbinu kadhaa ikiwamo akiba ya dhahabu, utafutaji wa mikopo na kufanya biashara ya kuuza dola.

Mbinu nyingine za BOT ilikuwa ni kuweka dhamana katika bidhaa zinazouzwa nje, utoaji wa leseni za maduka ya kubadilishia fedha, hamasa ya mauzo ya bidhaa nje na matumizi ya shilingi ya Tanzania katika miamala yote badala ya dola na utoaji wa taarifa za masoko yasyokuwa rasmi ya dola.

Wachumi wanasema ongezeko lolote la kiwango cha kubadilishia fedha za kigeni huongeza mzigo wa malipo kwa wafanyabiashara, uagizaji wa malighafi za uendeshaji wa viwanda, migoni na miradi ya uwekezaji nje ya nchi na hata malipo ya Serikali. Hii ni kwa sababu kiwango kikubwa cha shilingi kilitajika ili kufidia kiwango kile kile cha dola.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania(JWT), Hamis Livembe anasema maelfu ya wafanyabiashara waliathirika mitaji yao kutokana na athari za mafuta na dola.

“Kuna baadhi ya wafanyabiashara walijikuta wakishindwa kuagiza mizigo au kuagiza kidogo baada ya uhaba wa dola kwa sababu kama ulikuwa unahitaji dola 300,000 badala yake unapata dola 260,000 , hii iliathiri mtaji kwa kiwango kikubwa sana,”anasema Livembe akifafanua:

Livembe anasema wafanyabiashara wa mafuta pia waliathiriwa na mitaji kupitia uhaba wa Dola. “Dola iliadimika kwneye maduka maalumu kwa thamani ya Sh2,400 lakini ikasambaa mtaani kwa magendo kwa thamani ya Sh2,700 kwa hiyo Serikali haitambui ukokotoaji wa dola za mtaani hivyo inasababisha hasara kwenye mauzo.”

Miezi mitatu iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Makampuni ya Uuzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya aliliambia gazeti hili kampuni zilifikia mahitaji ya jumla ya dola hizo(wastani wa Sh1.9 trilioni) kwa ajili ya kufuta malipo ya bidhaa za petroli zilizoingizwa nchini kati ya Machi na Julai mwaka huu.

Hatua hiyo ilihitajika kupunguza athari kwani waagizaji hao wanasema uagizaji wa petroli na dizeli ulipungua kwa asilimia 24.2 kati ya Januari na Agosti mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. Aidha, uagizaji wa bidhaa hiyo ulipungua hadi tani milioni 1.43, chini sana ikilinganishwa na tani milioni 1.89.

Mchumi mwandamizi , Profesa Jehovaness Aikaeli kutoka Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) anasema njia pekee ya kumaliza changamoto hizo ni kuongeza kiwango cha uzalishaji wa bidhaa zinazoagizwa nje.

“Kwanza tuongeze uzalishaji wa bidhaa zote tunazolazimika kuagiza kwa dola nje, pili tuongeze mauzo ya bidhaa zetu nje ili kuongeza ukwasi wa dola, kwa hiyo tutazame sera zetu upande wa uzalishaji na sera zetu kwenye uwezeshaji wa mauzo ya nje, ”anasema Profesa Aikael.

Uchambuzi wa gazeti hili ulibaini nyongeza ya Sh1.83trilioni juu ya deni halisi la Taifa la Sh42.67 trilioni hadi Juni mwaka huu kupitia ongezeko la thamani ya dola dhidi ya shilingi huku kampuni za madini pia zikiathirika katika gharama za uendeshaji na uzalishaji.

“Katika shughuli za uzalishaji na uendeshaji wa migodi yote hutegemea uagizaji wa bidhaa kutoka nje. Mfano, vifaa mbalimbali, spea, mitambo, kemikali za kusafishia madini ambayo yanahiyajika kila siku,” anasema Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini na Nishati Tanzania (TCME), Benjamini Mchwampaka akifafanua:

“Kwa hiyo uhaba wa dola uliathiri sana kwenye uagizaji wa baadhi ya mahitaji hayo, nashauri Serikali iwe na utaratibu wa kutoa kipaumbele cha mahitaji ya dola kwa sekta zenye mahitaji makubwa ya dola.”

Mbali na athari za dola, mwanzoni mwa mwaka huu kulikuwa na uhaba wa kemikali aina ya cyanide inayotumika kuchenjulia madini katika migodi mikubwa na ya kati hatua iliyochagiza anguko la uzalishaji kwa kipindi cha miezi mitatu kwa madai ya athari zilizotokana na vita vya Ukraine.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, mahitaji ya kemikali hiyo migodini ni wastani wa tani 500 hadi 700 kwa mwezi lakini mahitaji yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 hatua iliyoshawishi matumizi mbadala ya kemikali hatarishi ya Zebaki iliyopigwa marufuku.
Maumivu mapya

Tayari viashiria vinaonyesha kuendelea kwa maumivu hayo mwakani baada ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kutangaza ongezeko la Sh100 nauli za daladala na mabasi ya mikoani kwa wastani wa Sh10,000 bila kujali maumivu ya ongezeko la Sh455 katika lita ya Petroli kati ya Januari hadi Novemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Latra, nauli hizo zimepanda baada ya kupanda bei za mafuta pekee, gharama za uwekezaji na uendeshaji, gharama za matengenezo ya gari, kubadilisha matairi, bima, kodi ya mapato, tozo za Halmashauri, ada na tozo za Latra, uchakavu, ukaguzi wa magari, mishahara ya madereva na makondakta.

Hata hivyo nauli hiyo inaongezeka wakati hali ya vipato vya wananchi ikiwa bado haijabadilika kwa ujumla wake. Maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanaojihusisha na vibarua vya viwandani, machinga, mama lishe, kazi za ndani katika makazi na usafi wa maofisi ni miongoni mwa waathirika wa nauli hizo kutokana na vipato vyao.

“Naishi Kinyerezi, natuamia Sh30,000 mwezi na chakula Sh30,000 kwa mwezi, ongezeko la nauli litafanya nitumie Sh36,000 kwa mwezi wakati mshahara wangu ni Sh120,000 kwa mwezi tangu mwaka 2018 haujabadilika,” anasema Hassan Juma, mfanyakazi wa kampuni ya usafi jijini Dar es Salaam.
 

Sakata la bandari

Uchambuzi wa gazeti hili umebaini sakata la mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari(IGA) ni miongoni mwa matukio yaliyotikisa mwaka 2023.

Mkataba huo ulitikisa mfululizo wa miezi minne ndani na nje ya mahakama na bunge kabla ya kufungwa mjadala Oktoba DP World ilipokabidhiwa bandari.
Baadhi ya hoja zilizoibua hofu ni pamoja na dalili za bandari kuuzwa, uhalali na kesi za DP World, ukomo wa mkataba, umilikishaji wa bandari zote nchini na ulinzi wa ajira za wazawa.

Hata hivyo, hoja hizo zilijibiwa na watalaamu kabla ya kuhamia majukwaa ya kisiasa.

“Taifa linapoingia kwenye mijadala ya namna hii, nashauri tujitahidi kuchuja hoja za msingi, sakata hilo lilikuwa ni kipimo cha gharama za uhuru tulionao,”anasema James Mwamaja. mkazi wa Mikocheni, Jijijini Dar es Salaam.

Hatimaye Oktoba 22, mwaka huu, Serikali ikasaini mikataba mitatu na kampuni ya DP World; Mikataba iliyosainiwa ni Mkataba wa Nchi Mwenyeji (HGA), Mkataba wa Upangishaji Ardhi (LA) na Mkataba wa Uendeshaji wa Bandari (CA) huku mageuzi ya kiuchumi yakiwekwa wazi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa alisema kuna mkataba wa ukodishaji na uendeshaji wa gati 4 – 7, na uendeshaji wa pamoja wa gati 0 – 3 kati ya TPA na DP World kwa shughuli za kibiashara na za kiserikali.

Mapato yanayokusanywa na TRA katika bandari hiyo yataongezeka kutoka Sh7.8 trilioni kwa mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh26 trilioni ifikapo mwaka 2032 na kwamba mkataba una ukomo wa miaka 30 na utendaji wa DP World utakuwa ukipimwa kila baada ya miaka mitano.

“Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)atakusanya mapato kutokana na idadi ya meli zilizohudumiwa, kwa hiyo tukiongeza ufanisi, badala ya kuhudumia meli 90, tukahudumia meli 130 maana yake TRA atakusanya kodi katika meli 130 badala ya meli 90 ndani ya mwezi mmoja,” anasema Mbossa.