Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bandari Dar yapaa Afrika Mashariki

Muktasari:

  • Kupaa huko ni matokeo ya maboresho ya miundombinu na uendeshaji wa shughuli za bandari nchini.

Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam, imepanda nafasi 105 kwa ufanisi wa huduma zake, ikizipiku bandari kadhaa katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwemo ya Mombasa nchini Kenya.

Hiyo ni kwa mujibu wa Ripoti ya Ufanisi wa Bandari Duniani ya mwaka 2025, iliyotolewa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Taasisi ya S&P Global Market Intelligence.

Hatua hiyo, imetajwa ni matokeo ya maboresho ya miundombinu na uendeshaji wa shughuli za bandari nchini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Bandari ya Dar es Salaam imepanda kutoka nafasi ya 360 mwaka 2024 hadi nafasi ya 255 mwaka 2025 duniani.

Miongoni mwa vigezo vilivyotumika kupima ufanisi huo, ripoti hiyo inaeleza ni muda wa kuhudumia meli, kasi ya upakuaji na upakiaji mizigo na matumizi bora ya miundombinu ya bandari (CPPI).

“Bandari ya Dar es Salaam imekuwa bandari iliyofanya vizuri zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Wakati Bandari ya Dar es Salaam ikipanda kwa kasi, Bandari ya Mombasa nchini Kenya imeshuka kutoka nafasi ya 375 mwaka 2024 hadi 396 mwaka 2025. Hilo linaonyesha mabadiliko ya ushindani katika sekta ya bandari ndani ya ukanda huo.

Akizungumzia matokeo hayo leo, Juni 22, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amesema hayo yametokana na uwekezaji uliofanywa katika kuboresha miundombinu ya bandari.

Miongoni mwa uwekezaji huo, amesema ni ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kuhudumia mizigo na mageuzi ya kiutendaji yaliyolenga kuongeza ufanisi wa huduma.

“Kama tulivyoona, takwimu zilizotolewa zinaonyesha kuwa ufanisi wa bandari umeongezeka kwa takribani asilimia 98 kutokana na kupungua kwa muda wa kuhudumia meli,” amesema Mbossa.

Amesema maboresho hayo yameongeza uwezo wa bandari kuhudumia meli na mizigo kwa haraka zaidi, hatua inayoiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa lango kuu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Hata hivyo, amesema TPA inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na ongezeko la mizigo kwa kupanua miundombinu katika bandari mbalimbali nchini.

“Licha ya mafanikio haya, tunaendelea kuwekeza katika upanuzi wa miundombinu ili kuhakikisha bandari zetu zinaendana na ongezeko la mahitaji ya usafirishaji na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania na nchi jirani zinazotumia huduma zetu,” amesema.