Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bandari kavu, kusubiri mchongo chanzo cha foleni Dar

Muktasari:

  • Madereva wa malori wanasema uhaba wa maegesho, ucheleweshaji wa huduma za kupakia na kushusha mizigo, pamoja na kusubiri ‘michongo’ kwa muda mrefu, hulazimisha magari kuegeshwa barabarani na kuchangia msongamano katika maeneo ya bandari kavu.



Dar es Salaam. Kuongezeka kwa idadi ya bandari kavu jijini hapa kunatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia msongamano wa malori na foleni za magari katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Mbali na uwepo wa bandari kavu nyingi, kutokuwepo kwa utaratibu maalumu wa utoaji wa mizigo, madereva kuegesha malori karibu na maeneo ya bandari hizo wakisubiri kupata mizigo ya kusafirisha “mchongo”, idadi ndogo ya mashine za kupakia na kushusha mizigo pamoja na uwepo wa gereji bubu kando ya barabara, ni baadhi ya sababu zinazochangia hali hiyo.

Wamiliki wa bandari kavu nchini wanasema ongezeko kubwa la mizigo inayopitia Bandari ya Dar es Salaam limezidi uwezo wa miundombinu iliyopo, jambo linalochochea msongamano wa malori na foleni zinazolalamikiwa na wananchi.

Kwa mwezi mmoja pekee, makontena 110,000 huingia nchini na ili yahudumiwe, ni lazima yatoke bandarini kwenda katika bandari kavu.

Kwa mujibu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Wilaya ya Temeke ina bandari kavu 74, sawa na asilimia 64.3 ya zote zilizopo jijini Dar es Salaam. Kigamboni ina bandari kavu 13 (asilimia 11.3), Ilala 22 (asilimia 19.1), Kinondoni nne (asilimia 3.5) na Ubungo mbili (asilimia 1.7).

Kisheria, Sheria ya Bandari Kavu ya mwaka 2018 inamtaka mwekezaji kupata vibali kutoka mamlaka za mipango miji, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (Tarura) au Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), pamoja na kufanya tathmini za athari za mazingira.

Tangu kuanzishwa kwa bandari kavu mwaka 2007, kiwango cha mizigo kinachohudumiwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam kimekua kikiongezeka kutoka tani milioni tisa hadi kufikia tani milioni 37 kwa mwaka, mizigo ambayo inahudumia kupitia bandari kavu.

Ukuaji huo umechangiwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa bandarini pamoja na maboresho yaliyoruhusu meli kubwa zaidi kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam.

Wadau wa sekta ya usafirishaji wanaeleza kuwa pamoja na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kupunguza foleni, usimamizi madhubuti wa maeneo ya bandari kavu na maegesho ya malori, unaweza kusaidia kupunguza changamoto hiyo.

Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, imeweka mkakati wa kuondoa msongamano wa malori jijini Dar es Salaam kwa kuanza kusafirisha mizigo kwa njia ya reli kwenda Bandari Kavu ya Kwala.

Mpango huu wa kimkakati unalenga kuondoa zaidi ya asilimia 90 ya malori na kuleta unafuu kwa wakazi na watumiaji wengine wa barabara.

Aidha, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kwa upande wake naye anatafuta suluhisho endelevu la tatizo hilo kwa kuanzisha shindano la ubunifu la “Foleni Challenge”, lililolenga kukusanya mawazo kutoka kwa vijana na wadau mbalimbali kuhusu namna bora ya kuzipunguza jijini Dar es Salaam.


Kwa nini malori yanajaa

Katika baadhi ya maeneo yenye shughuli za usafirishaji wa mizigo imebainika kuwa madereva wengi hulazimika kusubiri mizigo kwa muda mrefu huku wakiegesha magari yao pembezoni mwa barabara kutokana na uhaba wa maeneo maalumu ya maegesho.

Dereva aliyekutwa nje ya Chuo cha Uhasibu (TIA) wilani Temeke, Yesse Mapendano amesema baadhi ya magari hukaa kwa siku kadhaa yakisubiri kupata mizigo na mengine yakifanyiwa huduma ndogo za kiufundi katika maeneo hayo hayo.

"Ili upate mzigo wakati mwingine unalazimika kubaki karibu na eneo la upakiaji, magari mengi yanakuwa yameegeshwa hapa yakisubiri mchongo wa mzigo, ndiyo maana unaona yamejaa barabarani," amesema Mapendano.

Amesema pamoja na umuhimu wa kusubiri mizigo karibu na wateja, hali hiyo imekuwa ikisababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara kutokana na nafasi kubwa inayochukuliwa na malori hayo.

Kwa mujibu wa dereva huyo, baadhi ya magari hufanyiwa matengenezo kandokando ya barabara badala ya kupelekwa gereji kutokana na mazingira ya kazi na uhitaji wa karibu na maeneo ya kupakia mizigo.

"Hii siyo sehemu sahihi ya kufanya ‘service’, lakini wakati mwingine dereva analazimika kufanya hivyo kwa sababu anasubiri mzigo na hataki kuwa mbali na eneo la kazi," amesema.

Mbali na usumbufu wa matumizi ya barabara, madereva hao wameeleza kuwepo kwa hatari ya moto kutokana na magari mengi kuegeshwa karibu karibu.

Amesema iwapo moto utatokea kwenye gari mojawapo, unaweza kuenea kwa haraka na kuathiri magari mengine yaliyopo jirani.

"Kuna maeneo tumeshuhudia gari moja likiungua na kusababisha magari mengine kushika moto kwa sababu yalikuwa yameegeshwa karibu sana na hasara yake huwa kubwa," amesema.

Aidha, Mapendano amesema msongamano huo unaweza kuathiri upatikanaji wa huduma za dharura kama vile magari ya zimamoto na ya wagonjwa pindi ajali au moto vinapotokea.

"Hata kama moto unatokea, wakati mwingine njia zinakuwa zimezibwa na magari mengi kiasi kwamba huduma za uokoaji zinachelewa kufika," amesema.

Dereva mwingine katika bandari kavu ya Mbagala Zakhem, Abdalla Mlolo amesema miundombinu iliyopo katika bandari hiyo imejikita zaidi katika kuhudumia makontena lakini maegesho ya malori yamepewa kipaumbele kidogo.

"Wamejenga sehemu za kuhifadhi makontena, lakini hawakuweka miundombinu ya kutosha kwa ajili ya maegesho ya magari, endapo lori linapata hitilafu au dereva analazimika kusubiri zamu yake, hakuna eneo la kutosha la kuegesha," alisema.

Kwa mujibu wa dereva huyo, idadi ya malori yanayofika katika bandari hiyo ni kubwa kuliko uwezo wa miundombinu iliyopo, hali inayosababisha magari mengi kuegeshwa pembezoni mwa barabara kusubiri huduma.

"Unaweza kukuta mbele yako kuna malori zaidi ya 20 yakisubiri kuingia, wakati mwingine unalala kwenye lori kwa siku moja au mbili ukisubiri zamu yako ifike na lango moja kutumika kupitisha magari mengi," alisema.

Mbali na usumbufu huo, amesema maegesho ya kandokando ya barabara yanawaweka katika hatari ya kugongwa na magari mengine yanayopita au kuharibiwa mali zao na watu wasiojulikana.

Changamoto nyingine iliyotajwa ni ucheleweshaji wa huduma za kupakia na kushusha makontena kutokana na idadi ndogo ya mashine zinazotumika.

"Ukiingia leo si lazima upate huduma siku hiyo hiyo, wakati mwingine unaweza kusubiri siku moja au mbili kutegemea na foleni iliyopo na upatikanaji wa mashine za kuhudumia makontena," amesema Mlolo.

Madereva hao wamezitaka mamlaka husika pamoja na uongozi wa bandari kavu kuboresha miundombinu ya maegesho na kuongeza uwezo wa kuhudumia magari ili kupunguza msongamano unaoendelea kujitokeza.

Walisema hatua hiyo itasaidia kuongeza usalama, kupunguza muda wa kusubiri huduma na kuboresha ufanisi wa shughuli za usafirishaji wa mizigo kupitia bandari kavu hiyo.

"Hili ni jambo la muhimu kwa sababu sisi ndiyo tunasafirisha mizigo tukipata maeneo salama ya kusubiri na huduma kwa wakati, tutafanya kazi kwa ufanisi zaidi," amesema.


Wananchi walia

Mkazi wa Sandali Temeke, Malume Msigani amesema magari hayo makubwa baadhi kuingia hadi katika miji ya watu, yameweka ugumu kupatikana kwa huduma za dharula pale itakapotokea.

“Mtu akiugua ni ngumu kumfikisha hospitalini kwa hali hii, kuna wakati hata pikipiki haiwezi kupita, inabidi mumbebe mgonjwa mgongoni. Karne hii ni ya kushindwa kumfikisha mgonjwa hospitalini kwa dharula kweli,” amehoji.

Maneno yake yaliungwa mkono na Mashaka Mashaka akisema ni vyema Serikali ikaweka utaratibu wa uwashawishi wawekezaji kununua nyumba zilizo karibu na bandari kavu, ili kuepusha kelele na mivutano.

“Hawa hela wanayo, kama vipi watununue tu sisi tuwaachie hapa wafanye kazi kwa uhuru na sisi tuwe na amani, hali hii ipo siku watu watapigana hapa kwa sababu baadhi ya madereva wakisimamisha magari yao huondoka, ikitokea dharula hadi apigiwe simu aje si leo,” amesema Mashaka.


Itaendelea kesho……