Bashe awaka wanasiasa wanaohujumu zao la pamba

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
Muktasari:
- Aweka bayana sababu zinazochangia zao la pamba kushindwa kuwa na tija ya kutosha katika uzalishaji na soko.
Dodoma. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amewakosoa baadhi ya wanasiasa na viongozi ambao kwa maelezo yake, wamegeuza kilimo cha pamba kuwa nyenzo ya kisiasa badala ya kusaidia kukiinua kwa maslahi ya wakulima na uchumi wa Taifa.
Akijibu hoja za wabunge wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Waziri Hussein Bashe amesema haitakuwa rahisi kupata tija katika kilimo cha pamba endapo viongozi kutoka kanda ya pamba hawatakubali kubadilika na kuzingatia misingi ya kisayansi katika uzalishaji wa zao hilo.
Amesema kuwa moja ya changamoto kuu katika uzalishaji wa pamba ni kukataa misingi ya kisayansi, ambapo licha ya kuelekezwa kuwa wakulima wasichanganye mazao mengine katika mashamba ya pamba, bado wengi wanaendelea kufanya hivyo, jambo linalopunguza tija na ubora wa zao hilo.
“Tunaambiwa tusichanganye mazao kwenye mashamba ya pamba. Wote tunakubaliana kwenye vikao, hasa kule Usukumani. Lakini, tukifika hadharani, tunasema ‘Shamba ni lake, mwache achanganye pamba na mahindi.’ Hivi kwa mtazamo huo, tija inatoka wapi?” amehoji Waziri Bashe.
Ameeleza kuwa hali hiyo inaathiri moja kwa moja uzalishaji, na kwamba hoja kuu si bei ya pamba pekee, bali ni namna ya kuzalisha kwa tija.
“Kama tutakubali kuondoa siasa katika kilimo cha pamba na tukazingatia sayansi ya uzalishaji, basi zao hili linaweza kuleta mafanikio makubwa kama ilivyo kwa tumbaku.
“Kama Waziri wa Kilimo, madaraka yangu yanaisha baada ya kuapishwa mwingine. Wakati sisi bei yetu ni Sh1,150 kwa kilo, bei ya pamba katika nchi za Zambia ni Sh800, Malawi Sh864, Msumbiji Sh918 na Zimbabwe Sh800,” amesema.
Bashe amesema hao wote hawapati ruzuku yoyote kutoka Serikali zao, lakini hakusikiki kelele kwa sababu wanazalisha kwa tija, kwa ekari moja wanapata zaidi ya kilo 1,500 hadi 2,000.
Amesema wataalamu na wanasayansi wanasema kila ekari moja ipandwe miche ya pamba 44,000 hadi 50,000, lakini viongozi na wanasiasa wakienda katika mikutano ya hadhara wanawaambia wakulima wachanganye na mazao mengine.
“Walahi nitawaweka ndani watu. Nataka niwe mkweli kwenye hili. Brazil, mkulima mmoja kwenye hekta moja anapata kilo 6,500. Mwaka jana tulipeleka BBT, tulipeleka matrekta, tumewalimia kwa Sh35,000 kwa ekari, tumewapelekea mbegu na dawa,” amesema.
Bashe amesema wapo watu sasa wako mahakamani kwa makosa ya kukamua mafuta ya mbegu za pamba walizopelekewa kwa ajili ya kupanda.
“Ukimkamata, unapigiwa simu na kila mtu unayemjua. Lazima tubadilike kama tunataka kubadilika, watu wa pamba,” amesema.
Amesema mwaka 2018/19 uzalishaji wa pamba ulikuwa ni tani 340,000, lakini tija hiyo ilifia ndani ya ukumbi wa Bunge.
“Walioua ni sisi wanasiasa. Tukamdanganya Rais Dk John Magufuli, Dk Bashiru (aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally), na Waziri Mkuu akaenda kuita vikao pale Mwanza mpaka saa 7.00 usiku. Tubadilikeni wanasiasa tulioko katika ukanda wa pamba,” amesema na kuongeza;
“Huo ndio ukweli mchungu. Lazima tubadilike. Kukubali kuwa kilimo ni sayansi. Tunajificha katika kichaka kuwa tunaibiwa. Mtu atakayemleta mnunuzi wa pamba atakayenunua kilo moja kwa Sh3,000, nitampa pamba yote,” amesema.
Bashe amesema haliwezekani hilo kwa sababu bei katika soko la dunia kilo moja ni Dola za Marekani senti 64.
Amesema pamoja na kutoa ruzuku ya mbegu, mbolea na kulima, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wanajenga kiwanda cha kuongeza thamani ya zao la pamba.
Amesema wamepata ekari 1,000 mkoani Simiyu ambapo watatoa ruzuku ya umeme na kupeleka maji katika eneo hilo.
Aidha, Bashe amesema wana uwezo wa kupeleka kila wilaya zaidi ya trekta 50 zitakazokwenda kulima kwa ruzuku na si kwa bei ya soko na kuwa wanaanza mwaka huu utaratibu huo.
Bashe amesema wataanza kuchimba visima kwa ruzuku kwa kuwa wao watapata fedha kupitia mazao yatakayozalishwa.
“Wakulima wadogo maskini watachimbiwa bure kwa sababu ndio wameibeba hii nchi kufikia hapa ilipo. Tutaujenga ushirika kwa nguvu. Wezi tutawafunga. Ushirika hatuufuti, tutaendelea kuujenga polepole ili uweze kushikilia uchumi wa nchi hii,” amesema.
Amesema watatumia sheria kuchukua mashamba yaliyoshindwa kuendelezwa kwa maslahi ya umma.
Amesema mashamba hayo ni pamoja na ya chai yaliyopo wilayani Rungwe ambayo watanunua kiwanda cha chai na kuwakabidhi wakulima wadogo.
“Wakulima wadogo watamilikishwa viwanda vile. Tumeshanunua viwanda viwili vitakavyokuja kufungwa Rungwe (Mbeya) na Kilolo (Iringa) kwa ajili ya kuchakata chai. Tunazo changamoto, tutakuja kuzimaliza. Tutaendelea kukabiliana nazo,” amesema.
Bunge limeidhinisha wizara hiyo bajeti ya Sh1.2 trilioni kwa mwaka 2025/26, huku Sh702.27 bilioni zikienda katika miradi ya maendeleo.
Mbunge amjibu
Akizungumzia madai hayo, Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Contsantine Kanyasu amesema hakubaliani na hoja ya Bashe kwa kuwa kila kinachofanyika duniani hupangwa na wanasiasa na wataalamu ni washauri katika mipango hiyo.
“From political (kutoka kwa wanasiasa) ndio mipango inapangwa, mawaziri nao ni wanasiasa hakuna waziri ambaye si mwanasiasa, siwezi kukubaliana naye (Bashe).
“Mwanasiasa hauwezi kumkabidhi kwenda kumkamata mtu, hata mimi siwezi kukubali kwenda kumkamata mtu wangu bali nitamtetea, mamlaka sijivue jukumu lake,”amesema.
Kanyasu amesema vyama vya ushirika awali vilikuwa vikihusika na kupeleka pembejeo, maofisa ugani na kununua mazao ya wakulima, lakini sasa jukumu hilo limekwenda kwa kampuni zinazonunua zao hilo.
Amesema kutetereka kwa vyama vya ushirika kumevifanya kubaki kukusanya kodi za majengo na kuacha majukumu yake ambayo yalikuwa yakileta ustawi kwa zao hilo.
Mbunge huyo amesema pamoja na uwepo wa BBT, lakini ili kusaidia kuinua kilimo cha pamba ni kuimarisha block ambazo zitawakusanya wakulima katika maeneo yao na kuwapa mbegu, wataalamu (maofisa ugani) na soko.
“Sasa hivi katika eneo la ekari 20, hapa utakuta wakulima wanalima mahindi, wanalima pamba wengine wanalima zao lingine, wengine hawapigi dawa ya kuua wadudu ni rahisi magonjwa kwenda katika zao la pamba na kusababisha tija kuwa ndogo,”amesema.