Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bei ya sukari yapaa, wananchi walalama, sababu yatajwa

Muktasari:

  • Wananchi wameiomba Serikali kuingilia kati kudhibiti bei na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hiyo unaimarika katika maeneo mbalimbali ili kupunguza mzigo wa gharama za maisha.



Dar es Salaam/mikoani. Wakati bei ya sukari ikipanda kunatokana na upungufu wa bidhaa kwa wasambazaji wakubwa na kusimama kwa uzalishaji viwandani, wananchi wameeleza wasiwasi wao wakisema ongezeko hilo linaongeza ugumu wa maisha na kuathiri matumizi ya kila siku.

Katika maeneo mbalimbali nchini, bei ya sukari imeongezeka kutoka kati ya Sh2,800 na Sh3,000 kwa kilo hadi kufikia Sh5,000 katika baadhi ya mikoa. Ongezeko hilo limejitokeza siku chache kabla ya kuanza kutumika kwa bajeti mpya ya Serikali Julai 1, 2026, ambapo ushuru wa sukari inayoingizwa kutoka nje utaongezeka kwa Sh10 kwa kila kilo.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wameiomba Serikali kuingilia kati kwa kudhibiti bei na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hiyo unaimarika ili kupunguza mzigo wa gharama za maisha.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi leo Ijumaa, Juni 26, 2026 katika mikoa ya Simiyu, Mbeya, Kilimanjaro, Pwani, Dar es Salaam, Manyara, Mwanza, Morogoro na Zanzibar umebaini kuwepo kwa ongezeko hilo, huku wafanyabiashara wakieleza changamoto ya upatikanaji wa sukari na wananchi wakihofia hali hiyo itaongeza makali ya maisha.


Simiyu

Mkoani Simiyu, bei ya sukari imeongezeka kutoka Sh3,000 hadi Sh3,500 kwa kilo katika wilaya za Maswa, Meatu na Itilima.

Mfanyabiashara wa bidhaa za chakula mjini Maswa, John Magesa, amesema ongezeko hilo limetokana na kupungua kwa kiwango cha sukari kinachowafikia kutoka kwa wasambazaji wakubwa.

"Awali tulikuwa tunapata sukari kwa urahisi, lakini siku hizi mzigo unakuja kwa kiwango kidogo na gharama zimeongezeka, hivyo nasi tumelazimika kuongeza bei," amesema.

Naye mfanyabiashara wa Meatu, Rehema Mollel, amesema baadhi ya wafanyabiashara wameanza kununua sukari kwa wingi kwa hofu ya bei kuendelea kupanda, jambo ambalo limeongeza mahitaji sokoni na kuchangia shinikizo la bei.


Mbeya

Mkoani Mbeya, hali ni mbaya zaidi ambapo bei ya sukari katika baadhi ya maeneo imefikia kati ya Sh4,000 na Sh5,000 kwa kilo.

Mfanyabiashara Rachael Mbagala amesema hapo awali sukari inayozalishwa na viwanda vya Mtibwa, Kagera na Kilombero iliuzwa kwa Sh3,000 kwa kilo, huku ile iliyoagizwa kutoka Zambia na Brazil ikiuzwa kati ya Sh2,500 na Sh2,700 kwa kilo.

Amesema kwa sasa bei hizo zimebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na changamoto ya upatikanaji wa bidhaa.

Mfanyabiashara mwingine, Simba Jerome, amesema licha ya kupanda kwa bei, biashara ya sukari inaendelea kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya vinywaji vya moto wakati huu wa baridi.


Mwanza

Jijini Mwanza, bei ya sukari imeongezeka kutoka Sh3,000 hadi Sh3,500 kwa kilo kutegemea eneo.

Mfanyabiashara wa Soko la Buhongwa, Chris Mushi, amesema awali kilo moja ya sukari ilikuwa ikiuzwa kwa Sh2,800, lakini gharama za usafirishaji zimeongezeka kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta, hali iliyochangia ongezeko la bei kwa watumiaji wa mwisho.

Manyara

Katika mji mdogo wa Mirerani mkoani Manyara, mfanyabiashara Julius Kimario amesema wameelezwa kuwa baadhi ya viwanda vya sukari vimesimamisha uzalishaji kwa ajili ya matengenezo.

Amesema kwa sasa sukari imekuwa adimu katika maeneo kadhaa, jambo linalowalazimu wafanyabiashara kuinunua kwa gharama kubwa zaidi.

Kilimanjaro

Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, bei ya sukari imeongezeka kutoka Sh2, 800 hadi kati ya Sh3, 200 na Sh3,500 kwa kilo.


Baadhi ya wafanyabiashara wamesema bidhaa hiyo imekuwa ikipatikana kwa shida ikilinganishwa na miezi iliyopita, hali inayowalazimu kuuza kwa bei ya juu zaidi ili kufidia gharama walizotumia kuinunua.

Pwani

Mkoani Pwani, bei ya sukari imeongezeka kutoka Sh3, 000 hadi Sh3, 500 kwa kilo.

Wafanyabiashara wanasema wasambazaji wameongeza bei ya bidhaa hiyo kutokana na upungufu wa sukari unaojitokeza katika kipindi hiki cha mpito kabla ya baadhi ya viwanda kurejea katika uzalishaji.


Dar es Salaam


Jijini Dar es Salaam, bei ya sukari imeongezeka kutoka Sh2,500 hadi kati ya Sh3,000 na Sh3,600 kwa kilo kulingana na eneo.

Katika eneo la Tabata, kilo moja imeongezeka kutoka Sh2,500 hadi Sh3,500. Manzese bei imeongezeka kutoka Sh3,000 hadi Sh3,600, huku Mbezi Louis kilo moja ikiuzwa kwa Sh3,500 kutoka Sh3,000.

Baadhi ya wafanyabiashara wamesema ongezeko hilo linatokana na kupanda kwa gharama za upatikanaji wa sukari kutoka kwa wasambazaji wa jumla.


Morogoro

Mkoani Morogoro, bei ya sukari imeongezeka kutoka kati ya Sh2,700 na Sh2,800 hadi Sh3,200 kwa kilo.

Aidha, mfuko wa kilo 50 umeongezeka kutoka Sh137,000 hadi Sh140,000.

Mfanyabiashara wa eneo la Tushikamane Lukobe, Vitus Nkelego amesema amelazimika kuongeza bei baada ya wauzaji wa jumla kupandisha gharama za bidhaa hiyo.


Zanzibar

Visiwani Zanzibar, hali inatofautiana kati ya eneo na eneo. Katika baadhi ya maeneo sukari inauzwa kwa Sh3,000 kwa kilo kutoka Sh2,800 ya awali, huku maeneo mengine ikiendelea kuuzwa kwa bei ya zamani licha ya hofu ya kuendelea kupanda.

Machi mwaka 2025, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitangaza bei elekezi ya Sh2,500 kwa kilo ya sukari ili kulinda masilahi ya walaji.

TPC na Bodi ya Sukari waeleza sababu

Akizungumza na Mwananchi, Mwanasheria wa Kampuni ya Sukari ya TPC, David Shillatu amesema changamoto ya upatikanaji wa sukari hujitokeza karibu kila mwaka katika kipindi cha Juni kwa sababu viwanda vingi husimamisha uzalishaji kwa ajili ya matengenezo ya kawaida.

Hata hivyo, amesema baadhi ya wafanyabiashara wanatumia hali hiyo kama fursa ya kuongeza bei isivyo halali.

"Upungufu wa sukari katika baadhi ya maeneo unatokana pia na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu.

“TPC ilisimamisha uzalishaji tangu Machi kwa ajili ya ukarabati wa kawaida unaofanyika kila mwaka lakini kuanzia kesho Juni 27, 2026, kiwanda kitaanza tena uzalishaji," amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Profesa Kenneth Bengesi, amesema kuchelewa kwa baadhi ya viwanda kuanza uzalishaji ndiko kulikosababisha changamoto ya muda ya upatikanaji wa sukari.

Amesema hali hiyo si ya kudumu na tayari uzalishaji umeanza kurejea katika baadhi ya viwanda huku tani 34,000 za sukari zinatarajiwa kuwasili bandarini ili kuongeza upatikanaji wa bidhaa hiyo sokoni.

"Hatutegemei tatizo hili kuendelea. Kulikuwa na watu waliotaka kutumia hali hiyo kama fursa ya kupandisha bei. Kwa sasa kuna tani 34,000 za sukari zinatarajiwa kushuka bandarini na viwanda tayari vimeanza uzalishaji, hivyo hakuna sababu ya wananchi kuwa na hofu," amesema.

Profesa Bengesi amesema Bodi ya Sukari itaendelea kufuatilia mwenendo wa soko na kuingilia kati pale inapobaini changamoto ili kuhakikisha upatikanaji wa sukari unaendelea kuwa wa uhakika na kuzuia ongezeko lisilo la lazima la bei.


Wananchi walia makali

Wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wameeleza kuwa kupanda kwa bei ya sukari kunaongeza mzigo wa gharama za maisha, wakisema bidhaa hiyo ni muhimu katika matumizi ya kila siku ya familia nyingi.

Mkazi wa Moshi, James Kanje amesema kwa siku kadhaa amekuwa akizunguka katika maduka mbalimbali akitafuta sukari bila mafanikio kutokana na upungufu wa bidhaa hiyo.

Naye Jumanne Ndege wa Maswa amesema ongezeko la bei limeongeza gharama za matumizi ya familia wakati bidhaa nyingine muhimu nazo zimeendelea kupanda bei.

Mkazi wa Mbeya, Victoria Deus amesema kupanda kwa bei ya sukari ni sehemu ya mfululizo wa ongezeko la gharama za maisha unaowaathiri wananchi wengi, hivyo Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kurejesha utulivu wa soko.

Florida Paul wa Mkuyuni jijini Mwanza amesema familia nyingi sasa zinalazimika kununua sukari kwa vipimo vidogo vya Sh500 badala ya kilo nzima ili kupunguza matumizi.

"Zamani tulikuwa tunanunua kilo moja kwa wakati mmoja, lakini sasa tunanunua kidogo kidogo kulingana na uwezo wa siku hiyo," amesema.

Athari hizo zimeanza pia kuonekana kwa watoa huduma za vyakula na vinywaji.

Mama lishe anayefanya biashara katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu mkoani Morogoro, Rahma Juma, amesema amelazimika kuongeza bei ya kikombe cha chai ya rangi kutoka Sh200 hadi Sh500, huku bei ya andazi ikiongezeka kutoka Sh300 hadi Sh500 kutokana na kupanda kwa gharama za sukari na bidhaa nyingine.

Kwa upande wake, mama lishe wa Kibaha mkoani Pwani, Neema Shayo, amesema tayari ameongeza bei ya kikombe cha chai ya rangi kutoka Sh500 hadi Sh700 na kwamba endapo hali itaendelea, atalazimika kuongeza bei ya baadhi ya vyakula ili kuendana na gharama za uendeshaji wa biashara.

Wakati Serikali ikieleza kuwa hali hiyo ni ya muda na uzalishaji wa viwanda pamoja na ujio wa tani 34,000 za sukari utaimarisha upatikanaji wa bidhaa hiyo, wananchi na wafanyabiashara wanaendelea kusubiri hatua hizo zianze kuonekana sokoni.

Hata hivyo, kwa sasa ongezeko la bei limeendelea kuathiri kaya nyingi pamoja na biashara ndogo zinazotegemea sukari kama malighafi muhimu, huku matarajio yakielekezwa katika hatua za Serikali za kurejesha utulivu wa soko na kudhibiti ongezeko la gharama za maisha.

Imeandikwa na Imani Makongoro (Pwani), Baraka Loshilaa (Dar),  Saddam Sadick (Mbeya), Samwel Mwanga (Simiyu), Joseph Lyimo (Manyara), Saada Amir (Mwanza), Janeth Joseph (Kilimanjaro), Hamida Shariff (Morogoro) na Jesse Mikofu (Zanzibar)