Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Benki ya Azania yaidhinisha gawio la Sh18.36 bilioni kwa wanahisa wake

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Azania, Mhandisi Julius Ndyamukama (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Dk Esther Mangenya (kushoto) wakikabidhi hundi ya gawio la Sh18.36 bilioni kwa wawakilishi wa wanahisa wa benki hiyo, Paulo Kijazi aliyekuwa alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii  kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Wanahisa Wadogo, Charles Singili katika mkutano mkuu wa 33 wa wanahisa wa Benki ya Azania 2026 uliofanyika jana, jijini Dar es Salaam. Na Mpigapicha Maalumu

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa uamuzi wa mkutano, wanahisa watapokea gawio la Sh98.62 kwa kila hisa, sawa na asilimia 30 ya faida baada ya kodi ya Sh61.4 bilioni iliyopatikana mwaka ulioishia Desemba, 2025

Dar es Salaam. Benki ya Azania Plc imeidhinisha malipo ya gawio la Sh18.36 bilioni kwa wanahisa wake katika Mkutano Mkuu wa 33 wa Wanahisa (AGM) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo inaelezwa kuakisi utendaji mzuri wa kifedha wa benki hiyo kwa mwaka ulioishia Desemba, 2025.

Kwa mujibu wa uamuzi wa mkutano huo, wanahisa watapokea gawio la Sh98.62 kwa kila hisa, sawa na asilimia 30 ya faida baada ya kodi ya Sh61.4 bilioni iliyopatikana katika kipindi hicho.

Mkutano huo umewakutanisha wanahisa, wajumbe wa bodi ya wakurugenzi, menejimenti na wadhibiti wa sekta ya fedha kwa lengo la kupitia utendaji wa benki na kujadili mwelekeo wake wa kimkakati kwa mwaka ujao.

Akizungumza baada ya mkutano huo mwishoni mwa wiki, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo, Injinia Julius Ndyamukama  amesema uidhinishwaji wa gawio hilo unaonesha uimara wa kifedha wa benki pamoja na dhamira yake ya kuendelea kutoa thamani kwa wanahisa.

“Uidhinishwaji wa gawio la Sh18.36 bilioni unaonesha uthabiti wa benki na usimamizi mzuri wa kifedha. Tutaendelea kuwekeza katika teknolojia, kupanua shughuli zetu na kuboresha huduma kwa wateja huku tukidumisha faida ya benki,” amesema Ndyamukama.

Amesema mafanikio yaliyopatikana mwaka 2025 yalitokana na ukuaji katika maeneo muhimu ya biashara, kuongezeka kwa ufanisi wa kiutendaji pamoja na kuimarika kwa imani ya wateja kwa huduma zinazotolewa na benki hiyo.

“Wanahisa wetu ni sehemu muhimu ya mafanikio yetu. Gawio hili linaakisi imani waliyoendelea kuionesha kwa benki pamoja na uimara wa mfumo wetu wa biashara,” amesema.

Katika mkutano huo, wanahisa walipatiwa taarifa kuhusu utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya maendeleo ya benki, ikiwamo upanuzi wa mtandao wa matawi, maboresho ya huduma za kidijitali na ongezeko la utoaji wa mikopo kwa sekta za biashara ndogo na za kati (SMEs), kilimo, pamoja na wanawake na vijana.

Azania imesema inaendelea kuimarisha nafasi yake katika sekta ya benki nchini, ikisaidiwa na msingi imara wa wanahisa wake wakubwa, ikiwamo mifuko ya hifadhi ya jamii kama PSSSF, NSSF, NHIF, WCF na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), pamoja na wanahisa wadogo na wafanyakazi wa benki hiyo.

Kwa mujibu wa benki hiyo, mafanikio yaliyofikiwa yanatokana na utekelezaji wa mkakati wa muda mrefu unaolenga kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuunda thamani endelevu kwa wadau wake.

Benki ya Azania imesema itaendelea kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa, huku ikiendelea kulinda na kukuza masilahi ya wanahisa wake.