Boti za kisasa zaongeza uvuvi wa samaki Ziwa Victoria
Muktasari:
- Wavuvi hao sasa wanaingizia Sh3 milioni kutoka Sh200,000 kwa wiki baada ya kuanza kutumia boti za kisasa walizokopeshwa na Serikali.
Mwanza. Uzalishaji wa samaki kwa baadhi ya wavuvi wa Ziwa Victoria umeongezeka kutoka kilo 20 kufikia kilo 300 kwa wiki, baada ya kuanza kutumia boti za kisasa walizokopeshwa na Serikali.
Hiyo imefanya uzalishaji huo kuwaingizia Sh3 milioni kutoka Sh200,000 baada ya kuuza kilo moja ya samaki kwa Sh10,000.
Januari 30, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan alizindua na kukabidhi boti 160 za uvuvi wa kisasa, zilizokopeshwa kwa wanufaika 989, huku vizimba 222 vikigawiwa kwa wanufaika 1,213 katika mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Geita.
Mradi huo wa mkopo wa zana na vifaa vya uvuvi bila riba kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), utawanufaisha wavuvi katika mikoa yote yenye shughuli za uvuvi katika maziwa makuu ya Nyasa, Victoria na Tanganyika ambapo wavuvi walianza kulipa marejesho baada ya miezi mitatu ya kufanya kazi tangu wakabidhiwe boti hizo.
Wakizungumza na Mwananchi jana Juni 21, 2024 baadhi ya wanufaika wa boti hizo zenye ukubwa wa mita tano hadi 14, uwezo wa kubeba tani 9.5 ya samaki pamoja na zana nyingine zilizoko ndani yake ikiwemo mashine, pampu ya kuvuta maji, nyavu, GPS na maboya ya kujikolea; wamesema licha ya changamoto ndogondogo, uzalishaji umeongezeka ikilinganisha na matumzi ya boti za kienyeji.
Mnufaika wa mkopo wa boti ya mita 10 na 7.06 kutoka kisiwa cha Buchosa, Robert Rwanga amesema boti hizo zinazowawezesha kufika kina kirefu cha maji kutokana na uimara na kasi ndio sababu ya kuvua samaki wengi na kufanya kuingiza zaidi ya Sh3 milioni kutoka Sh200,000 kwa wiki.
“Pato linaongezeka kwa sababu tunakwenda deep sea (kina kirefu)…sisi kwenye kikundi chetu hatuendi na kurudi kwa sababu tunatumia mashine kubwa, tunaenda ziwani na kukaa siku saba ndio tunarudi, kwa hiyo pato limeongezeka,” amesema.
Mwenyekiti wa mwalo wa Mswahili jijini Mwanza wenye wavuvi na wachakataji wa mazao ya samaki zaidi ya 600, Robert Charles amesema katika mwalo huo, vikundi vinne vya BMU, Uwamwa, Tuinuane na Tunza Mazingira vilipata boti hizo na kila kikundi kina wavuvi zaidi ya 20 wanaonufaika na mkopo huo pamoja na familia zao.
Rwanga amesema boti hizo zimeleta tija kwa wavuvi akidai kuwa zimetatua baadhi ya changamoto ikiwemo ya wavuvi kuogopa kwenda kina kirefu kutokana na boti zao za awali kuwa na uwezo mdogo pamoja na hofu ya kupoteza maisha kutokana na vyombo kusombwa na mawimbi au upepo mkali ziwani.
“Sasa hivi tumeondokana na changamoto nyingi tulizokuwa tukizipata kwenye shughuli zetu za uvuvi, ikiwemo kutokwenda mbali kutokana na uimara wa vyombo, kusombwa na upepo na mawimbi hasa wakati wa upepo mkali.
“Kutokana na faida, mahitaji yetu ni makubwa kiasi kwamba tumeweka zamu ya watu wanne kwenda ziwani kuvua…wanakaa siku saba wakirudi wengine wanafuata, kwa hiyo idadi inayosubiri foleni kwenda ziwani ni kubwa. Hivyo, tungependa kuongezwa boti hata tano,” amesema
Wavuvi waiangukia Serikali
Miongoni mwa changamoto zilizokuwepo kwenye boti hizo ambazo hata hivyo wavuvi wanadai wamezitatua, ni uchache wa nyavu za kuvulia, wakiiomba Serikali angalau ifikirie kuwaongezea nyavu za nchi saba na nane zitakazotumika kipindi cha kiangazi ambacho samaki wanaopatikana ni wakubwa kuanzia nchi saba.
“Changamoto zilikuwepo za kawaida ambazo tulizitatua. Kwa mfano, boti yetu ilikuwa na changamoto ya sehemu ya kuhifadhia samaki haikuwa vizuri lakini changamoto hiyo tumeitatua kazi inaendelea. Changamoto ya pili ni nyavu chache, kama tungepata nyavu 300 za aina tofauti tofauti tuwe tunavua majira tofauti tofauti ingependeza zaidi,” amesema.
Mvuvi wa mwalo wa Mswahili jijini Mwanza, Charles Lulinga amesema ni kweli baadhi yao walipata boti kubwa zenye injini kubwa, hivyo kufanya matumizi ya mafuta mengi lakini wamepata suluhisho kwa kuwa wameongeza muda wa kuvua ili kufidia gharama za uendeshaji.
“Pia, Serikali ituongezee nyavu za dagaa ili wakati hali ikiwa ngumu samaki hawapatikani tuvue dagaa, lakini pia tupewe mashine ndogo na injini zenye nguvu ya 15 au 99 ili tufanye uvuvi wa moja kwa moja,” amesema.
Kauli ya Wizara
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi), Edwin Mhede amesema mradi huo una tija na kama Serikali haitorudi nyuma bali kuuendeleza, huku akiahidi itashugulikia changamoto na marekebisho yanayopendekezwa na wavuvi.
“Kama kuna mambo mbalimbali ya kurekebisha ambayo yanarekebishika na wavuvi wenyewe maana yapo pia, lakini kama yapo mengine ambayo yapo nje ya uwezo wao ambayo yanahitaji utaalamu zaidi, nimeshatoa maelekezo kwa niaba ya Serikali kwa chuo chetu cha elimu, Wakala wa Elimu ya Uvuvi (Feta), watafiti wa uvuvi (Tafiri) waliopo Mwanza kwamba tushirikiane na taasisi za Serikali hususani Shirika la Uwakala wa meli nchini (Tasac), halmashauri na TADB kuzitatua.
“Lakini kwa ufupi, Wizara tumeyabeba, tutaendelea kuwa karibu nao, kuwasikiliza, pia kuna masuala mengine tumejifunza na pengine tutaendelea kujifunza yana sura ya marekebisho ya kanuni zinazosimamia usajili au uundaji wa boti pamoja na kuimarisha upatikanaji wa masoko ya samaki wanaofugwa,” amesema.