Sababu zinazopunguza samaki Ziwa Victoria

Sangara mwenye uzito wa kilo sita ambaye ameuzwa Sh120,000 katika Mnada wa Gadala  uliofanyika katika Mwalo wa Butuja wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

Katibu wa Kamati ya Usimamizi wa Maeneo ya Fukwe (BMU), Mwalo wa Butuja, Maneno Malima amesema kwa uzoefu wake wa miaka 15 katika shughuli za uvuvi, amebaini kupungua kwa samaki ndani ya Ziwa Victoria

Mwanza. Wakati Serikali ikikiri kupungua kwa samaki ndani ya Ziwa Victoria kwa asilimia 35, wavuvi wametaja sababu zinazochangia kitoweo hicho kutoweka ikiwamo Serikali kufanya uamuzi bila kuwashirikisha.

Januari 30, 2024, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla bila kutaja idadi ya samaki waliokuwamo ziwani, alisema utafiti uliofanywa kati ya mwaka 2018 hadi 2022 unaonyesha kupungua kwa samaki ndani ya ziwa hilo.

Makalla alitoa kauli hiyo kwenye hafla ya kukabidhi zana za uvuvi zikiwamo boti 55 za uvuvi na vizimba 222 kwa wavuvi wa kanda ya ziwa huku Rais Samia Suluhu Hassan akikabidhi zana hizo katika hafla hiyo iliyofanyika Uwanja wa Nyamagana jijini humo.

Mwananchi imefika katika Mwalo wa Butuja na Kayenze, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza na kushuhudia sangara mwenye uzito wa kilo sita akiuzwa Sh120,000 katika mnada maarufu kama Gadala.


Samaki waliotoweka

Akizungumza na Mwananchi Digital, Katibu wa Kamati ya Usimamizi wa Maeneo ya Fukwe (BMU), Mwalo wa Butuja, Maneno Malima amesema kwa uzoefu wake wa miaka 15 katika shughuli za uvuvi, amebaini kupungua kwa samaki ndani ya Ziwa Victoria na kutoweka kwa baadhi ya aina ‘Species’ za samaki ziwani humo.

Malima ambaye amezaliwa mwambao wa ziwa hilo wilayani Bunda mkoani Mara, ametaja samaki waliopatikana ziwani miaka 15 iliyopita, sasa hawapatikani kabisa ambao ni Kuyu na Gobegobe.

Pia, ametaja samaki aina ya Hongwe, Ningu, Soga, Furu asilia, Gogogo na Nembe kuwa wanapatikana kwa kusuasua.

“Furu asilia walishapotea labda hawa ambao ni chakula cha sangara. Kuna athari na upungufu mkubwa wa samaki ndani ya ziwa letu, kwetu ni Bunda nimeenda nyumbani watu wanapata shida sana kupata kitoweo cha samaki,” amesema Malima.

Amesema katika Mwalo wa Butuja wenye wavuvi  takribani 1,200, awali ilikuwa kawaida kupata tani moja ya samaki kwa siku waliokuwa wanauzwa katika viwanda vya uchakataji na kusafirisha nje ya nchi, lakini sasa hata samaki wa kuuza sokoni kwa matumizi ya ndani hawatoshelezi.

Akitolea mfano mwaka 2009, Malima anasema ‘pisi’ 300 za sangara zilikuwa zinavuliwa kwa kutumia ndoano 600 pekee, kwa wastani wa kila ndoano mbili kupata samaki mmoja lakini sasa hivi, mvuvi anaweza kuzitandaza ndoano hizo na asipate ‘pisi’ 50 za sangara wenye uzito wa kilo moja moja.

Mkazi wa Capripoint, Agnes William (51) ambaye ni mchuuzi wa samaki katika mwalo huo kwa miaka 25, amesema endapo Serikali isipochukua hatua za haraka za kudhibiti kupungua samaki ndani ya ziwa hilo, litaishia kuhifadhi maji kwa matumizi ya kunywa, kuoga na umwagiliaji.

“Mwaka 2005, samaki mwenye uzito wa kilo moja katika Mwalo wa Butuja aliuzwa bei isiyozidi Sh1,000 lakini sasa hivi sangara au sato mwenye uzito huo huo anauzwa hadi Sh18,000; nina wasiwasi hata tuliojiajiri kwenye biashara kama tutaweza kuhudumia familia zetu miaka 10 ijayo,” amesema Agness.

Ushuhuda wa Agness unaungwa mkono na Milka Phinias, mchuuzi wa samaki anayeonekana kukata tamaa baada ya kukaa kwenye mtumbwi tangu saa 2 asubuhi hadi saa 10:32 asubuhi alipokuwa akihojiwa na Mwananchi Digital bila mafanikio wala matumaini ya kupata kitoweo kwa ajili ya wateja wake.

New Content Item (1)
New Content Item (1)


Sababu za kutoweka samaki

Katibu huyo wa BMU Mwalo wa Butuja, Malima alipoulizwa chanzo cha tatizo hilo ametaja ongezeko la wavuvi lililochangia kushamiri kwa uvuvi haramu na mabadiliko ya tabianchi yaliyochangia watu kuvamia kisha kuendesha shughuli za kilimo kando ya ziwa hilo.

Malima amesema uamuzi wa Serikali kuridhia matumizi ya ‘taa za sola’ katika uvuvi wa dagaa, umechangia kutoweka kwa kile anachodai wavuvi watumia nyavu za dagaa na taa hizo kuvua sangara na aina nyingine za samaki jambo linalosababisha kuzoa hadi mazalia.

Mvuvi wa Mwalo wa Kayenze, John Chacha ametaja uharibifu wa mazingira unaotekelezwa na jamii ya wavuvi kuzunguka ziwa hilo kuwa chanzo cha kutoweka kwa samaki.

Pia, amesema sababu nyingine ni mamlaka za utafiti na udhibiti nchini kutoshirikisha wavuvi wadogo katika mchakato wa utafiti wa vyanzo vya upungufu wa samaki, mbinu zinazosababisha na namna ya kukabiliana nazo.

“Wanachokifanya viongozi wetu wanajadiliana huko juu, kisha wanakuja kutekeleza huku chini lakini ukiangalia anayetungiwa hizo kanuni hajashirikishwa ipasavyo; inawezekana kuna viongozi wa wavuvi wanaoshiriki lakini je, ushirikishwaji huo umefika kwenye mialo walipo wavuvi wadogo wanaodhaniwa kuwa ndiyo waharibifu wa kwanza?” amehoji Chacha.


Ametahadharisha kwamba, huenda hata malengo ya kuongeza uzalishaji wa samaki kwa njia ya vizimba yasifanikiwe kama ilivyopangwa kwa sababu wavuvi wadogo katika mialo kuzunguka ziwa hilo hawana elimu ya kutosha kuhusu aina hiyo ya ufugaji endelevu.

“Serikali ilikabidhi zana kwa wavuvi ninaoamini sio wanaopatikana kwenye hii mialo yetu. Je, tutaweza kutokomeza uvuvi haramu kwa ufugaji wa samaki ziwani wakati wavuvi wadogo wanaotajwa kuendesha uvuvi haramu wakiwa hawana elimu wala uwezeshwaji,” amesema Chacha.


Hata hivyo, ameishauri Serikali kuangalia upya mfumo wa upatikanaji wa wavuvi wanaokabidhiwa zana na kujengewa uwezo kuhusu uvuvi endelevu ili kunusuru uhai wa Ziwa Victoria huku akisisitiza kutofanya hivyo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.

Mbali na kupungua kwa kitoweo katika jamii, athari nyingine ya kupungua kwa samaki ziwani ni ukosefu wa ajira na kupunguza pato la Taifa kunakochangiwa na kufungwa kwa viwanda 13 vya kuchakata na kusindika mazao ya samaki Mwanza na Mara.


Taarifa ya kufungwa kwa viwanda sita vya samaki mkoani Mara imetolewa jana Ijumaa Aprili 5, 2024, na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Kanda ya Ziwa (LVRLAC) nchini, William Gumbo wakati wa Mkutano Mkuu wa jumuiya uliofanyika mkoani Mwanza.

Gumbo amesema viwanda hivyo vilivyokuwa vinafanya kazi usiku na mchana kwa miaka zaidi ya 10 mfululizo, vilianza kufungwa miaka minne iliyopita tangu 2021 huku uhaba wa malighafi ya samaki ukitajwa kuwa sababu kuu za kufungwa kwake.

“Hali ya ulinzi wa Ziwa Victoria siyo nzuri, samaki wamepungua sana nikitolea mfano Manispaa ya Musoma tulikuwa na viwanda sita vyote vimefungwa kutokana na upungufu wa samaki kwa sababu ya uvuvi haramu, kuongezeka shughuli za kibinadamu kumesababisha ukataji holela wa misitu na utupwaji taka ziwani,”amesema Gumbo.

“Moja ya maazimio tuliyoweka kwenye Mkutano Mkuu wa LVRLAC ni kila halmashuri zinazozunguka ziwa kupitia BMU waende wakaimarishe ulinzi, watu wazingatie kanuni na sheria zilizowekwa. Pia, tunakwenda kuhamamisha uvuvi mbadala na endelevu kwenye maeneo hayo,” amesema Gumbo.


Taarifa ya Gumbo haitofautiani ya ile ya Makalla aliyoitoa Januari 30, mwaka huu akisema viwanda saba vya uchakataji wa mazao ya samaki kati ya 15 mkoani Mwanza vimefungwa huku chanzo kikitajwa kuwa ni uhaba wa malighafi ya samaki.

 Makalla alisema mkoa ulitoa mikakati na maelekezo 11 ili kuhakikisha wanadhibiti uvuvi haramu na kufanya uwe endelevu, akidokeza kutoa elimu ya ufugaji kwa njia ya vizimba ni miongoni mwa mipango hiyo.

“Mimi kama mwenyekiti wa mikoa ya kanda ya ziwa (wakati huo) hatutakuangusha (Rais Samia), tutaweka mikakati ya kuwa na uvuvi endelevu Kanda ya Ziwa,” aliahidi Makalla.