Serikali yamaliza utata wa samaki

Muktasari:

  • Serikali imewaondoa hofu Watanzania kuhusu taarifa kuwa baadhi ya wavuvi wamekuwa wakitumia dawa ya kuoshea maiti kuhifadhia samaki.


Mwanza. Serikali imewaondoa hofu Watanzania kuhusu taarifa kuwa baadhi ya wavuvi wamekuwa wakitumia dawa ya kuoshea maiti kuhifadhia samaki.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma juzi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alisema jambo hilo halina hakika na kwamba hiyo ni hisia tu ya baadhi ya watu.

Alisema ndio maana Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alipokuwa jijini Mwanza aliagiza wizara ya afya ifanye utafiti ili kama ni kweli kinafanyika kitu kama hicho kizuiliwe mara moja.

“Nawaomba niwatoe hofu Watanzania . Tuchukue samaki kutoka Mwanza tulete Dodoma ama tupeleke Dar es Salaam kwa kuhifadhi na maji ya maiti? Hakuna kitu kama hicho,”alisema.

Kauli hiyo ya Serikali imekuja kufuatia hali ya taharuki na sintofahamu, kutokana na kusambaa kwa taarifa kuwa baadhi ya wavuvi na wafanyabiashara wa samaki, wanatumia dawa ya kuhifadhi maiti kuhifadhia samaki ili wasiharibike haraka.

Taarifa kwamba dawa hiyo iitwayo formalin inatumiwa na baadhi ya wavuvi, iliibuliwa na Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango, wakati wa hafla ya kuzindua jengo la wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Kanda Bugando Septemba 13.

Dk Mpango, alirudia kauli hiyo alipohutubia wananchi katika hafla ya uzinduzi wa stendi ya mabasi na maegesho ya magari makubwa eneo la Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela, huku akiagiza mamlaka na vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuchukua hatua.

Kutokana na maagizo hayo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel aliyeambatana na Makamu wa Rais katika ziara yake ya siku tatu mkoani hapa, aliujulisha umma kuwa uchunguzi wa madai hayo tayari umeanza, huku akionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.


Walichosema wavuvi

Katibu wa Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu), Jephta Machandalo alilieleza Mwananchi taarifa za wavuvi kutumia kemikali ya formalin kuhifadhia samaki, imeibua mshtuko na hofu kwenye jamii inayoweza kuathiri soko la samaki ndani na nje ya nchi na hivyo kusababisha madhara ya kiuchumi kwa wavuvi, wafanyabiashara na Taifa kwa ujumla.

“Kwa nafasi yangu ya uongozi wa wavuvi sijawahi kupata taarifa hizi kwa sababu barafu inayotumiwa na wavuvi na wafanyabiashara inatoka viwandani. Sasa tunajiuliza dawa hiyo inawekwa huko kiwandani au wapi,” alihoji.

Alisema licha ya kuanza uchunguzi wa suala hilo, Tafu inaamini samaki wa Tanzania wako salama ndiyo maana wanauzwa kwenye soko la nje ambako kabla ya kununuliwa hupimwa ubora na viwango.

Alisema chama hicho kinaendelea kufanya mawasiliano na mamlaka za Serikali ikiwemo Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupata taarifa za kina kuhusu jambo hilo ili kuondoa hofu iliyotanda miongoni mwa wavuvi na Watanzania kwa ujumla.

“Kusema kweli tumepatwa na taharuki, ndiyo maana tunafanya mawasiliano na mamlaka kutafuta majibu ya kina kama kweli madai haya yamechunguzwa na kuthibitishwa na vyombo husika,” alisema

Suleiman Rashid, mvuvi katika mwalo wa Mswahili jijini Mwanza alisema taarifa za matumizi ya kemikali ya kuhifadhia maiti kwenye samaki, ni pigo kwenye biashara ya samaki na itaathiri uchumi wao.

Mwenyekiti wa Tafu, Bakari Kadabi alisema chama hicho kimeunda timu maalum kufuatilia na kuchunguza suala hilo kwa lengo la kupata ukweli.

“Nawaomba wavuvi na wananchi watulie wakati huu tunaendelea kufuatilia jambo hili,”alisema Kadabi.


Kauli ya wafanyabiashara

Ali Juma, mfanyabiashara wa samaki jijini Mwanza alisema kwa kipindi cha miaka 10 aliyofanya shughuli hiyo, hajawahi kutumia kemikali yoyote kuhifadhi samaki.

“Kwanza samaki hawa tunaoouza ndio hata sisi tunakula kwenye familia zetu; kamwe hatuwezi kutumia dawa yenye madhara kwa afya ya biadamu kwa sababu tutakuwa tunajiangamiza wenyewe,” alisema Ali

Muuza samaki wa soko la Mbugani jijini Mwanza, Ashura Kulwa alisema iwapo ni kweli wapo wavuvi na wafanyabiashara wa samaki wanaotumia maji ya kuoshea maiti kuhifadhia samaki, basi watu hao wanafanya hivyo kutokana na imani za kishirikina.


Wataalam wa afya

Baadhi ya madaktari waliozungumza na Mwananchi walisema hadi sasa hakuna utafiti wala uchunguzi wa kisayansi, uliofanyika kuthibitisha madai hayo na kushauri jambo hilo lichukuliwe kwa makini, kwa sababu linahusu siyo tu afya ya watu, bali pia mustakabali wa uchumi kupitia sekta ya uvuvi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani na damu kutoka Hospitai ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC), Dk Heronima Kashaigil alisema licha ya kutothibitishwa matumizi ya dawa ya formalin kuhifadhia samaki, pia hakuna utafiti uliofanyika kuthibitisha kemikali hiyo inasababisha saratani.

“Ninachokijua ni kwamba formalin ni kemikali inayotumika kuhifadhi maiti, kwa sababu ina uwezo wa kubadilisha tishu za mwili na kuufanya usioze kwa haraka,” alisema Dk Kashaigil

Akijibu kwa kifupi na tahadhari swali iwapo kuna uwezekano wa formalin kutumika kuhifadhia samaki, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk Crispin Kahesa alisema: “Huwezi kutumia formaldehyde kuhifadhia chakula maana ina chocking smell.”

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, daktari bingwa katika moja ya hospitali za mkoa wa Arusha alisema, “Ingredients za Formalin ni maalum kwa ajili ya kuhifadhi maiti isiharibike kwa muda fulani; kwamba inaweza kutumika kuhifadhia samaki ni jambo linalohitaji utafiti wa kisayansi,”

Kuhusu ugonjwa wa saratani, daktari huyo alisema: “Kuna sababu au vyanzo vingi vya saratani; haiwezekani kutaja kitu kimoja kuwa chanzo cha ugonjwa huu. Kiujumla, saratani inaweza kusababishwa na mfumo wa maisha, aina ya vyakula, upungufu wa kinga mwilini, shughuli za kiuchumi, mila na desturi za jamii, kutofanya mazoezi na tabia ya kutopima afya,”

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk Julius Mwaiselage alisema suala la matumizi ya kemikali hiyo kwenye samaki, ni jambo linalohitaji utafiti huku akishauri kusubiriwa kwa taarifa ya uchunguzi aliosema unafanywa na wataalam wa Wiziara ya Afya.

Kuhusu upatikanaji wa formalin, daktari mmoja wa jijini Mwanza ambaye pia anamiliki duka la dawa muhimu, alisema kwa sharti la kuhifadhiwa kuwa: “Upatikanaji wa kemikali ikiwemo hiyo dawa ya kuhifadhia maiti ni jambo gumu kwa sababu hupatikana kwenye maduka maalum ya kemikali na huuzwa kwa wenye leseni, vibali na shughuli zinazowaruhusu kuwa nayo.”Pato sekta ya uvuvi

Ingawa juhudi za kumpata Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki kuzungumzia athari za taarifa hizi kwenye sekta ya uvuvi, hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 inaonyesha kwa mwaka 2021, sekta ya uvuvi ambayo mnyororo wake wa thamani unanufaisha watu zaidi ya milioni 4.5, ilikua kwa asilimia 2.5 na kuchangia asilimia 1.8 kwenye Pato la Taifa.

Hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu, jumla ya tani 34,841.72 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo vipande 169, 089 iliuzwa nje ya nchi na kuingizia Taifa kipato cha zaidi ya Sh475.01 bilioni.

Shughuli za uvuvi nchini zinafanywa zaidi na wavuvi wadogo kwenye maji ya asili ambao huchangia takriban asilimia 95 ya samaki wote wanaovuliwa nchini kupitia vyombo vya uvuvi vipatavyo 57, 991.

Licha ya kuchangia pato la mtu mmoja mmoja na familia, sekta ya uvuvi pia huongeza usalama wa chakula na lishe, huku kitoweo cha samaki kikichangia asilimia 30 ya protini inayotokana na wanyama.


Wachumi na wanasheria

Akizungumzia taarifa za wavuvi kutumia kemikali isiyostahili kuhifadhia samaki, mchumi mbobevu mkazi wa jiji la Arusha, Simon Mapolu alisema muda umefika wa kuhakikisha sekta zote za uzalishaji ikiwemo uvuvi zinakuwa rasmi na shughuli zake zinafanyika kwa mujibu wa sheria, sera na weledi.

“Uvuvi wetu, hasa uvuvi mdogo haufanyiki kiweledi. Wavuvi wetu wanachukulia shughuli zao kama sehemu ya kujikimu badala ya kazi na kwa bahati mbaya hakuna usimamizi na ufuatiliaji wa karibu ndio maana tunaweza kusikia taarifa za watu kutumia kemikali hatarishi kiafya,” alisema Mapolu na kuongeza

“Muda umefika sasa tuufanye uvuvi kuwa taaluma inayohitaji elimu maalum; tuwekeze kwenye elimu, teknolojia na miundombinu ya uvuvi, ili tuongeze siyo tu uzalishaji, bali pia ubora, thamani na soko la bidhaa ndani na nje ya nchi,’’ alisema.

Kuhusu hatua za kuchukua, alisema: “Serikali inapaswa kuchukua hatua mbili, mosi ifanye uchunguzi kubaini ukweli na kufanya operesheni ya muda mfupi kudhibiti matumizi hayo; na pili tuchukua hatua za muda mrefu kwa kutunga sheria, kuanda sera, kutoa elimu kwa umma na uwezeshwaji kimtaji kwenye sekta ya uvuvi.’’

Mchumi huyo alisema kuwapo kwa taarifa zinazodai matumizi yadawa hiyo, itasababisha athari ya kiuchumi kwa kupunguza mapato yatokanayo na bidhaa za uvuvi, athari aliyosema itawakumba wavuvi, wafanyabiashara na Taifa.

“Ongezeko la vitendo vya kihalifu ni athari nyingine inayoweza kuambatana na taarifa hizi kwa kundi la vijana wanaojihusisha na uvuvi kulazimika kutafuta njia mbadala ya mkato wa kujiingizia kipato,” alisema Mapolu


Viongozi kuchukua hadhari

Profesa Haji Semboja, mchumi mbobevu na mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDS) alisema matumizi ya dawa ya kuhifadhia maiti kwenye samaki, ni miongoni mwa taarifa zenye taharuki ambazo hazistahili kutolewa wala kutangazwa na viongozi kabla ya utafiti na uchunguzi wa kina.

“Mabenki yanaibiwa sana, lakini kwa maslahi yao hawatangazi wizi huo isipokuwa wanafanya uchunguzi na kudhibiti mianya ya wizi,” alisemaHatua kwa watakaobainika

Danstan Mutaggahywa, wakili wa kujitegemea mjini Bukoba alisema ikithibitika, wavuvi na wafanyabiashara wanaodaiwa kutumia dawa ya kuhifadhi maiti kwenye samaki, wanaweza kukabiliwa na mashtaka ya jinai ikiwemo uhujumu uchumi na kutakatisha fedha.

“Watu hawa pia wanaweza kushtakiwa kwa kukiuka sheria ya afya ya jamii ya mwaka 2009 inayotoa mwongozo kuhusu udhibiti, leseni na biashara ya bidhaa ya chakula inayosimamiwa kupitia ofisi za waganga wakuu wa wilaya ili kulinda afya ya jamii,” alisema wakili Mutagahywa.