CRDB yapata faida ya Sh236 bilioni aka 2020

CRDB yapata faida ya Sh236 bilioni aka 2020

Muktasari:

  • Licha ya changamoto za corona zilizojitokeza, Benki ya CRDB imetangaza faida kabla ya kodi kiasi cha Sh236 bilioni mwaka 2020.

Dar es Salaam. Licha ya changamoto za corona zilizojitokeza, Benki ya CRDB imetangaza faida kabla ya kodi kiasi cha Sh236 bilioni mwaka 2020.

Faida hiyo, ni sawa na ongezeko la asilimia 35 ikilinganisha na Sh172 bilioni iliyopata mwaka 2019, kabla janga la corona halijafika Afrika na kuathiri biashara kwa kiasi kikubwa.

Baada ya kodi, faida ya benki hiyo ni Sh165.18 bilioni iliyoongezeka kutoka Sh122.64 bilioni iliyopata mwaka juzi.

Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela ufanisi huo umetokana na maboresho ya mifumo na mkakati wao wa kupunguza gharama za uendeshaji.

“Licha ya corona, biashara ilienda vizuri na mapato yetu yaliongezeka. Tuliijiimarisha katika maeneo tuliyokuwa na udhaifu,” alisema Nsekela.

Mapato ya benki hiyo yaliongezeka kutoka Sh774 bilioni mwaka 2019 na kufika Sh854 bilioni mwaka 2020 wakati akiba za wateja zikipanda kutoka Sh200 bilioni mpaka Sh5.4 trilioni katika kipindi hicho.

Faida ya benki hiyo pia ilichangiwa kwa takriban Sh15 bilioni na kampuni tanzu zake ambazo ni CRDB Burundi iliyopata faida ya Sh11.2 bilioni na CRDB Insurance Broker Limited iliyoingiza faida ya Sh3.6 bilioni.

“Mkakati wetu wa kuwasikiliza wateja na kuwaaidia kurejesha mikopo yao kipindi cha corona ulisaidia kwani ulituwezesha kuendana na mazingira yaliyokuwapo,” alisema Nsekela.

Mwaka jana benki hiyo ilikopesha zaidi ya Sh3.9 trilioni ambazo ni sawa na ongezeko la Sh500 bilioni ikilinganishwa na mwaka 2019 huku ikipunguza uwiano wa mikopo isiyolipika kutoka asilimia 5.5 mpaka 4.4.

Mkurugenzi wa fedha wa benki hiyo yenye zaidi ya wateja milioni tatu nchini wanaohudumiwa kwenye matawi yake 268, Fredrick Nshekanabo, alisema “tutaendelea kushirikiana na wateja wetu hasa waliopo kwenye sekta zilizoathirika zaidi na corona.”

CRDB ambayo mwezi uliopita iliboresha programu yake ya Simbanking ili kuwaruhusu wateja wapya kujifungulia akaunti mahali popote walipo au kwa mawakala wao 18,542 waliopo, in amtandao wa mashine 550 za kutolea fedha pamoja na vituo 1,900 vya mauzo vinavyofanya kazi kwa saa 24 wiki nzima.