DET yaitaja Tanzania moja ya masoko yake ya kimkakati ya utalii Afrika
Meneja msaidizi wa Operesheni za Kimataifa wa Shirika la Dubai la Utalii na Masoko ya Biashara, Khalaf Alaleeli akizungumza wakati wa maonesho ya kibiashara ya utalii Dubai yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, kulia ni mkuu wa kitengo cha mawasiliano DET Kanda ya Afrika, CIS na Ulaya ya Kati na Mashariki, Milo Radonjic
Muktasari:
- Dubai imeeleza Tanzania ni moja ya masoko yake muhimu zaidi barani Afrika, ikisema ongezeko la safari za ndege na mahitaji ya usafiri vinafungua fursa mpya za utalii na biashara.
Dar es Salaam. Idara ya Uchumi na Utalii ya Dubai (DET) imeitaja Tanzania kuwa moja ya masoko yake muhimu na ya kimkakati barani Afrika, ikisema ongezeko la safari za ndege na mahitaji ya usafiri vinafungua fursa mpya za utalii na biashara kati ya pande hizo mbili.
Kwa mujibu wa tathmini ya DET, wageni 897,000 kutoka Afrika walitembelea Dubai mwaka 2025, ikiwa ni karibu asilimia tano ya watalii wote wa kimataifa waliowasili humo, huku Tanzania ikitajwa kuendelea kuwa nguzo muhimu katika ukuaji huo.
Akizungumza leo Julai 10, 2026, Meneja Msaidizi wa Operesheni za Kimataifa wa Shirika la Dubai la Utalii na Masoko ya Biashara (DCTCM), Khalaf Alaleeli, amesema Tanzania ni moja ya masoko muhimu zaidi na ya kimkakati kwa Dubai barani Afrika.
Alaleeli amebainisha hayo wakati wa maonyesho ya kibiashara ya utalii jijini Dar es Salaam yaliyokwenda sambamba na kueleza mkakati mpya kwa wasafiri, wafanyabiashara na watalii kutoka Tanzania kwenda Dubai.
Amesema katika mkakati huo, DET imepanua wigo wa vivutio na huduma za utalii vinavyoendana na bajeti za makundi mbalimbali yanayotaka kufanya utalii Dubai.
Alaleeli amesema pamoja na utalii wa mapumziko, Dubai inaendelea kujitangaza kama kitovu cha biashara, mikutano na uwekezaji, hivyo kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuitumia kama lango la masoko ya kimataifa.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DET Kanda ya Afrika, CIS na Ulaya ya Kati na Mashariki, Milo Radonjic
Amesema kwa sasa kuna safari kadhaa za moja kwa moja kwa wiki kutoka Dar es Salaam na Zanzibar kwenda Dubai, jambo ambalo limeifanya safari kuwa rahisi zaidi kwa watalii na wafanyabiashara wa Tanzania.
"Tumefanya hivi katika kipindi ambacho mahitaji ya safari za kimataifa yanaongezeka, ushirikiano imara wa kibiashara na uwepo wa muunganiko thabiti wa usafiri wa anga," amesema.
Katika maonyesho hayo yaliyowakutanisha wadau zaidi ya 130 wa sekta ya usafiri na utalii, wakiwamo mawakala wa usafiri, waendeshaji wa ziara za utalii (tour operators) na mashirika ya ndege, Alaleeli amesema lengo ni kuimarisha ushirikiano na kuwapa wadau wa Tanzania uelewa mpana wa bidhaa za utalii za Dubai.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DET Kanda ya Afrika, CIS na Ulaya ya Kati na Mashariki, Milo Radonjic, amesema maonyesho ya mwaka huu ni fursa ya kuthibitisha dhamira yao katika soko la Tanzania na kuimarisha ushirikiano na sekta ya usafiri.
Amesema Dubai inatoa huduma zinazoendana na kila bajeti, akibainisha kuwa utafiti uliofanywa na DET unaonyesha kuwa wasafiri wengi wa Kitanzania wanaokwenda Dubai kwa sasa wanazidi kutafuta maeneo ya likizo na biashara yenye unafuu wa gharama, muda mzuri wa kifamilia, maeneo ya ununuzi (shopping), utamaduni na burudani katika eneo moja.
"Ili kukidhi mahitaji hayo, Dubai imepanua wigo katika huduma hizo, ikiwemo vivutio vya utalii vinavyotembelewa bila malipo," amesema.