Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtambi ataka mapinduzi ya teknolojia Serengeti

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza kwenye kikao cha baraza maalumu la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Serengeti. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameagiza Halmashauri ya Serengeti kutumia vishkwambi badala ya makaratasi na kuwekeza katika hoteli za nyota tano pamoja na uchimbaji wa dhahabu ili kuongeza mapato, kuimarisha maendeleo na kuzalisha ajira kwa vijana.

Serengeti. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuachana na matumizi ya makaratasi katika vikao vya Baraza la Madiwani na kutumia vishkwambi (tablets) ili kuendana na teknolojia ya kisasa.

Kanali Mtambi alitoa maelekezo hayo leo Julai 9, 2026, katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichojadili hoja za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25.

"Nimeshangaa kuona bado mnatumia makaratasi katika karne hii. Hebu badilikeni. Baraza liwe la kisasa; wapeni madiwani vishkwambi. Matumizi ya teknolojia yana manufaa makubwa kuliko kuendelea kutegemea mfumo wa analojia," amesema.

Akizungumzia mapato, amesema Serengeti ina fursa nyingi za kiuchumi kutokana na uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, na kwamba ubunifu wa viongozi unaweza kuwezesha halmashauri kupata vyanzo vipya na endelevu vya mapato.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wakiwa kwenye kikao maalumu cha baraza kujadili hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2024/25. Picha na Beldina Nyakeke

"Hebu tufikirie nje ya boksi. Serengeti ina fursa nyingi sana za kiuchumi. Jengeni hoteli ya nyota tano; mradi huu utalipa sana. Kama changamoto ni mtaji, nendeni benki mkakope, kwa sababu mnakopesheka," amesema.

Amesema uwekezaji katika hoteli za hadhi ya juu na sekta ya madini utaongeza mapato ya halmashauri, kufungua ajira kwa vijana na kuchochea maendeleo ya uchumi wa eneo hilo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Dk Maulidi Madeni amesema maandalizi ya ununuzi wa vishkwambi yamekamilika na matumizi yake yataanza katika kikao kijacho cha Baraza la Madiwani.

"Tumepanga kununua vishkwambi katika mwezi huu wa kwanza wa mwaka wa fedha 2026/27. Hivyo, nawahakikishia kuwa katika kikao kijacho tutakuwa tumeachana na matumizi ya makaratasi na kuhamia kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa," amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ayubu Makuruma amesema maelekezo ya Mkuu wa Mkoa yatatekelezwa ili kuboresha ukusanyaji wa mapato na kuongeza uwezo wa halmashauri kutekeleza majukumu yake.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wakiwa kwenye kikao maalumu cha baraza kujadili hoja za CAG kwa mwaka wa fedha 2024/25. Picha na Beldina Nyakeke

Amesema mvua kubwa zilizonyesha Machi mwaka huu na kushuka kwa bei ya mazao ya biashara, hususan pamba na tumbaku, vilichangia halmashauri kutofikia malengo ya makusanyo ya mwaka wa fedha 2024/25.

"Haya maelekezo uliyoyatoa ni muhimu sana. Tukiyatekeleza ipasavyo, yatatusaidia kuondoa vikwazo vya kufikia malengo yetu. Endapo tutakutana na changamoto yoyote, tutakuja kwako kwa ushauri na msaada ili tuweze kufanikiwa," amesema.

Makuruma amesema halmashauri imeendelea kupata hati safi ya ukaguzi katika mwaka wa fedha 2024/25 na Baraza la Madiwani litaendelea kuisimamia menejimenti ili kudumisha uwajibikaji na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.