Maboresho ya miundombinu iliyoharibiwa na mvua Serengeti yaanza
Mwonekano wa sehemu ya barabara ya kutoka Geti la Ndabaka hadi Seronera yenye urefu wa kilomita 121.5, ikiwa katika hatua za ukarabati baada ya kuathiriwa na mvua kubwa za masika zilizonyesha mwanzoni mwa mwaka.
Muktasari:
- Maboresho hayo yanahusisha ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja na vivuko, yakilenga kuhakikisha watalii na watumiaji wengine wa hifadhi wanaendelea kupata huduma za usafiri kwa urahisi katika misimu yote ya mwaka.
Serengeti. Serikali imeanza kuboresha miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti inayogharimu zaidi ya Sh8.1 bilioni, kufuatia uharibifu uliosababishwa na mvua za masika zilizonyesha mwaka huu.
Maboresho hayo yanahusisha ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja na vivuko, yakilenga kuhakikisha watalii na watumiaji wengine wa hifadhi wanaendelea kupata huduma za usafiri kwa urahisi katika misimu yote ya mwaka.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 28, 2026 katika hifadhi hiyo wakati maboresho hayo yakiendelea, Mhifadhi Daraja la Pili, Mhandisi Musa Nzuki alisema mvua za masika ziliharibu sehemu za miundombinu, hali iliyosababisha Serikali kutoa fedha kwa ajili ya maboresho hayo.
Alisema kwa sasa kazi zinaendelea, ikiwemo ujenzi wa barabara kutoka geti la Ndabaka hadi Seronera yenye urefu wa kilomita 121.5 ambapo inatarajiwa kukamilika baada ya miezi sita.
“Mvua za masika zilisababisha uharibifu wa miundombinu katika maeneo mbalimbali ya hifadhi. Barabara hii itagharimu Sh4.5 bilioni. Kati ya fedha hizo, Sh1.2 bilioni ni sehemu ya Sh8.1 bilioni zilizotolewa na Serikali huku Sh3.3 bilioni zikitokana na vyanzo vingine vya fedha. Lengo ni kuhakikisha barabara inapitika mwaka mzima,” alisema.
Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Charles Mkara alisema ujenzi unaendelea vizuri na tayari wamekamilisha hatua ya awali ya uundaji wa msingi wa barabara (formation) kwa kilomita 41.4 kutoka geti la Ndabaka hadi Kirawira B. Alisema kwa sasa wanaendelea na hatua ya kuinua tuta la barabara katika maeneo yenye miinuko ya chini.
“Lengo ni kuhakikisha hata mvua kubwa zikinyesha barabara inapitika kama ilivyo wakati wa kiangazi,” alisema.
Alisema kazi ya kuinua tuta inafanyika katika eneo la takribani kilomita 18 na hadi sasa imefikia asilimia 10.
Aliongeza kuwa madaraja pia yatajengwa katika maeneo yanayokatwa na maji ili kuruhusu maji kupita bila kuharibu barabara na hivyo kupunguza athari zinazojitokeza wakati wa masika.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Catherine Mbena alisema maboresho hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha uwekezaji katika sekta ya utalii unaenda sambamba na kuboresha miundombinu.
“Tumefanya kazi kubwa kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania duniani. Sasa tunahakikisha miundombinu inakwenda sambamba na juhudi hizo ili watalii wanaokuja wakute mazingira bora ya kutembelea hifadhi zetu,” alisema.
Kwa mujibu wa Mbena, maboresho hayo yatasaidia watalii kufika kwa urahisi katika maeneo mbalimbali ya hifadhi, ikiwemo maeneo yanayoshuhudia uhamaji mkubwa wa nyumbu, ambao ni kivutio kikubwa cha utalii katika hifadhi hiyo.
Alisema takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 35 ya watalii wanaotembelea Tanzania huvutiwa kuja baada ya kusikia maoni mazuri kutoka kwa watalii wengine waliowahi kutembelea nchi hiyo.
Mbena alisema msimu wa watalii wengi tayari umeanza na idadi ya wageni wanaoingia nchini inaendelea kuongezeka licha ya mashindano ya Kombe la Dunia yanayoendelea katika bara la Amerika.
Mmoja wa waongoza watalii mwenye uzoefu wa miaka mingi, Semle Michael alisema maboresho ya barabara ya Ndabaka hadi Seronera yataongeza ubora wa huduma za utalii, hususan katika kipindi cha uhamaji wa nyumbu.
Alisema watalii wengi hutumia barabara hiyo kufika maeneo ya magharibi mwa Serengeti kushuhudia uhamaji wa nyumbu, hivyo ubovu wa barabara ulikuwa ukisababisha changamoto kwa wageni na waongoza watalii.
“Tunamshukuru Serikali na Tanapa kwa kuanza kuboresha barabara hii. Kwa sasa hali imeanza kuwa nzuri na mashimo yamepungua. Hii itarahisisha safari za watalii na kuongeza ubora wa huduma wanazopata wanapotembelea Serengeti,” alisema.
Mhandisi wa Idara ya Miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, Abubakar Havanda alisema Tanapa inatarajia kujenga madaraja sita katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo.
Alisema madaraja hayo yatajengwa katika maeneo ya Mto Banagi, Orangi, Bokasi, Viboko vya Nabi na Kwa bona.
“Kazi za awali za uchunguzi wa kijioteknolojia (geotechnical investigation), upimaji wa topografia (topographic survey) na uchunguzi wa hidrologia (hydrological survey) zilianza Mei 15, 2026 na kukamilika Juni 20, 2026.”
“Kwa sasa wataalamu wapo katika hatua ya kuandaa michoro ya usanifu (design phase), kabla ya kuanza mchakato wa kutangaza zabuni na baadaye kuanza ujenzi wa madaraja hayo,” alisema.