Dk Mwinyi akagua bei za vyakula madukani

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akiangalia mchele unaouzwa dukani alipofanya ziara za kushtukiza kwenye maduka ya vyakula ya rejareja, Chake Chake, Pemba jana. Picha na Ikulu Zanzibar

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi jana alifanya ziara ya kushtukiza kwa wafanyabiashara wa maduka na vyakula ya rejareja kujionea hali halisi ya bidhaa hizo Chakechake kisiwani Pemba.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kuzungumza na wafanyabiashara mbalimbali Ikulu Zanzibar Januari 31, mwaka huu ambapo aliwasihi wapunguze bei za bidhaa za vyakula ili kuwapunguzia makali ya maisha wananchi.

Katika mkutano huo alisema licha ya Serikali kutofanya biashara, iwapo wafanyabiashara wataendelea kuongeza bei za bidhaa itaagiza yenyewe vyakula na kuwauzia wananchi kwa bei nafuu.

Kauli hiyo aliirudia Februari 3, 2023 alipowahutubia wananchi baada ya sala ya Ijumaa katika msikiti Masjid Shifaa - Mwembetanga, Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Nimewaambia wafanyabiashara si vyema Serikali ikafanya biashara lakini mkitufikisha sehemu lazima tufanye biashara,” alisema.

“Nitawaambia Shirika la Biashara (ZSTC) watoe fedha walete wao chakula wauze, kwa sababu hatuwezi kuwavumilia wafanyabiashara wanaoongeza bei kwa makusudi kwa kupenda wao huku wanaumiza watu,” alisema.

Jana wakati akielekea Uwanja wa Ndege wa Pemba, Rais Mwinyi aliwatambelea na kuzungumza na wafanyabiashara wa kisiwa hicho huku akiwauliza jinsi wanavyouza bidhaa zao hususani vyakula.

“Sisi tunataka bidhaa zipungue bei kidogo, vile mnavyonunua basi tunataka na wananchi wapate unafuu kidogo,” alisema Dk Mwinyi wakati akielezwa kuhusu bei ya vyakula na mmoja wa wafanyabiashara wa nafaka ambaye hakufahamika jina lake mara moja.

Mfanyabishara mwingine, alimueleza Rais Mwinyi kuwa wanauza kilo moja ya mchele kati ya Sh3,000 na Sh3,300 huku maharage yakiuzwa kati ya Sh3,000 na Sh3,500 kulingana na ubora wa nafaka hizo.

Baadhi ya wananchi walizoungumza na gazeti hili kuhusu hali ya vyakula walisema pamoja na jitihada hizo anazozifanya Rais Mwinyi bado unahitajika mkakati maalumu kwa sababu bado hali ni tete, hivyo Serikali itafute njia mbadala kumaliza tatizo hilo ili kuwanusuru wananchi hususani masikini ambao wanaumizwa na bei hizo.

Halima Saleh Talib, alisema kwa mwananchi wa hali ya chini anashindwa kumudu gharama hizo kwa kuwa bado zipo juu na watu wengi hawana uwezo kuzimudu.

“Maisha magumu bado bei za vyakula zipo juu, mheshimiwa Rais anajitahidi lakini kwa kweli bado bei zipo vilevile, wananchi tunaendelea kuteseka hatujaona unafuu wowote. Kununua mchele kilo moja kwa zaidi ya Sh3,000 sio kazi ndogo,” alisema.

Naye Talib Khamis alisema “mimi naona mpango wa Serikali kuagiza vyakula yenyewe ndio litakuwa suluhisho kwa wananchi na haitakuwa mara ya kwanza, maana huko nyuma ilishawahi kuagiza kutokana na njaa iliyojitokeza.”

Kwa upande wao wafanyabiashara madai yao changamoto iliyosababisha bidhaa kupanda bei ni mkwamo wa utoaji mizigo bandarini pamoja na gharama kubwa za mizigo zinazotozwa.

Pia wanaiomba Serikali na Shirika la Bandari kufanya juhudi za ziada kupunguza ucheleweshaji wa utoaji mizigo wakitoa kipaumbele kwa bidhaa zenye mahitaji ya haraka kwa wananchi.