Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Faida za malipo kidijitali nchini, yakianza Julai Mosi

Dar es Salaam. Wakati mtandao ukiwa ni moja ya njia ya uwezeshaji kiuchumi, kuanza kwa malipo ya kidijitali katika baadhi ya huduma Julai Mosi mwaka huu nchini inatajwa na wataalamu wa uchumi kama moja ya njia ya kuongeza uwazi wa miamala.

Akiwasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 bungeni, Waziri wa Fedha, Dk Khamis Mussa Omar alisema mageuzi hayo yanalenga kuimarisha ajenda ya mabadiliko ya kidijitali nchini, kuongeza ufanisi wa miamala, kudhibiti uhalifu wa kifedha, kuimarisha uwazi na kupunguza gharama za kushughulikia fedha taslimu.

“Maboresho yanayofanyika katika mifumo ya malipo yatachangia jitihada za Serikali za kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika uchumi kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuzuia shughuli za kihalifu pamoja na gharama zisizo za lazima,” alisema.

Kwa mujibu wa Serikali, malipo ya kidijitali yatakuwa ya lazima katika sekta mbalimbali ikiwamo usafiri wa umma kama mabasi ya mwendokasi, vivuko, reli, usafiri wa anga na huduma za usafiri kwa kutumia programu za kidijitali.

Mfumo huo pia utatumika katika maegesho ya magari, vituo vya mafuta, kumbi za mazoezi, sinema, hoteli, migahawa, kumbi za mikutano, viwanja vya michezo pamoja na maonesho makubwa kama Sabasaba na Nanenane.

Pia taasisi za elimu kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu nazo zitalazimika kutumia malipo ya kielektroniki, sambamba na mifumo ya masoko ya mazao kupitia vyama vya ushirika na AMCOS zinazoshughulika na mazao ya kimkakati kama kahawa, pamba, korosho, chai, tumbaku na mkonge.

Miamala ya mali isiyohamishika pia itaathirika ambapo kuanzia Julai Mosi, 2026 uthibitisho wa malipo ya kielektroniki utakuwa sharti katika uhamishaji wa ardhi, majengo na magari. Wizara ya Ardhi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) zitapaswa kuthibitisha kumbukumbu za malipo ya kidijitali kabla ya kuridhia mabadiliko ya umiliki.

Serikali inaeleza kuwa hatua hiyo itaboresha ufuatiliaji wa miamala, kuongeza ulipaji wa kodi na kuimarisha uwajibikaji katika biashara za mali.

“Ili kusaidia mabadiliko hayo, Serikali imepanga kupanua matumizi ya mifumo ya Lipa Namba na misimbo ya QR kwa wafanyabiashara wadogo, wakiwamo mama lishe, waendesha bodaboda na wafanyabiashara wa masokoni. Wafanyabiashara watakaotumia mifumo hiyo watapewa kipaumbele katika upatikanaji wa mikopo kutoka programu za Serikali na taasisi za fedha,” alisema Balozi Omar.

Akizungumzia hatua hizi, Mhadhiri Mwandamizi wa Fedha katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Tobias Swai alisema mwelekeo huo ni mzuri kwani Tanzania imekuwa ikielekea kwenye matumizi ya malipo ya kidijitali kwa takribani muongo mmoja.

“Ni hatua chanya. Tulianza safari hii takribani miaka 10 iliyopita na watu wengi tayari wanatumia mifumo ya malipo ya kielektroniki,” alisema.

Alisema matumizi ya mifumo hiyo hupunguza utegemezi wa fedha taslimu na kurahisisha ufuatiliaji wa fedha katika uchumi.

“Hupunguza haja ya kuchapisha fedha nyingi na kupunguza hatari zinazotokana na fedha kutoka nje ya mfumo rasmi wa kifedha. Pia ni rahisi kufuatilia mtaji na mzunguko wa fedha,” alisema.

Hata hivyo, alibainisha kuwa gharama za miamala bado ni kikwazo kikubwa kwa matumizi mapana ya huduma hizo. Alitolea mfano tofauti za gharama kati ya miamala ya benki na ile ya fedha za simu na kusisitiza umuhimu wa kupunguza ada hizo.

Pia alitaka kuimarishwa kwa muunganiko wa mifumo ya malipo kupitia Tanzania Instant Payment System (TIPS) ili kupunguza gharama na kuongeza ufanisi.

Kwa upande wake, Profesa Mshiriki wa Uchumi wa Maendeleo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kampasi ya Elimu (DUCE), Abel Kinyondo alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uwazi na kudhibiti uhalifu wa kifedha.

“Mfumo usiotumia fedha taslimu ni mzuri kwa sababu unaipa Serikali uwezo wa kufuatilia matumizi ya fedha na kusaidia kudhibiti utakatishaji fedha, rushwa na ufadhili wa ugaidi,” alisema.

Hata hivyo, alisema changamoto ya ujumuishaji wa kifedha bado ni kubwa kwani wananchi wengi hawana akaunti za benki wala huduma za malipo ya kidijitali kama Visa na Mastercard.