Comesa yalenga kurahisisha biashara kupitia mfumo wa bima Kidijitali
Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Dk Baghayo Saqware, akizungumza katika Mkutano wa 64 wa Kamati ya Usimamizi wa Mpango wa Kadi ya Njano ya COMESA uliofanyika jijini Dar es Salaam, ukihusisha wawakilishi kutoka takribani nchi 15 wanachama.
Muktasari:
- Mpango wa Kadi ya Njano ya Comesa ni mfumo wa bima ya magari unaotumika katika nchi wanachama ambao huhakikisha fidia kwa wahusika wa tatu wanaopata madhara kutokana na ajali za barabarani zinazohusisha magari yanayosafiri kati ya nchi hizo.
Dar es Salaam. Matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika Mfumo wa Kadi ya Njano ya Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) yanatarajiwa kuongeza kasi ya biashara ya kikanda, kuboresha huduma za bima na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa.
Mpango wa Kadi ya Njano ya Comesa ni mfumo wa bima ya magari unaotumika katika nchi wanachama ambao huhakikisha fidia kwa wahusika wa tatu wanaopata madhara kutokana na ajali za barabarani zinazohusisha magari yanayosafiri kati ya nchi hizo.
Hayo yameelezwa katika Mkutano wa 64 wa Kamati ya Usimamizi wa Mpango wa Kadi ya Njano ya Comesa uliofanyika Juni 23, 2026 jijini Dar es Salaam, ukihusisha wawakilishi kutoka takribani nchi 15 wanachama.
Mkutano huo ulijadili njia za kuhuisha mfumo wa bima ya magari unaotumika katika nchi za Comesa, kupunguza changamoto za kiutendaji na kuboresha utaratibu wa fidia kwa waathirika wa ajali zinazotokea wakati wa safari za kuvuka mipaka.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi David Boucher kutoka Djibouti, amesema majadiliano yao yamejikita katika mageuzi yatakayoufanya mfumo huo kuwa wenye ufanisi zaidi na unaokidhi mahitaji yanayoongezeka ya biashara ya kikanda.
“Tunakutana mara mbili kwa mwaka na mikutano hii ni muhimu kwa sababu hutupa nafasi ya kuandaa mabadiliko kabla ya mkutano wa mwaka wa Baraza la Ofisi za Bima.
“Kwa sasa tunafanya kazi ya kuimarisha matumizi ya teknolojia na kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili mfumo huu,” amesema Boucher.
Boucher amesema nchi wanachama zimeanza kutambua umuhimu wa kutumia teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza imani kwa watumiaji wa barabara pamoja na waendeshaji wa shughuli za usafirishaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Bima (NIC), Kaimu Abdi Mkeyenge amesema mpango huo una mchango mkubwa katika kurahisisha biashara na usafirishaji kwa kuhakikisha kuwa madereva wanapata fidia bila kujali nchi ambayo ajali imetokea.
Amesema Tanzania inanufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na mpango huo kwa kuwa ni lango muhimu la biashara kwa nchi kadhaa zisizo na bandari ambazo hutegemea bandari ya Dar es Salaam kwa usafirishaji wa mizigo.
Akifungua mkutano huo, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) Dk Baghayo Saqware, amezitaka nchi wanachama kuongeza kasi ya mabadiliko ya kidijitali na kuunganisha mifumo ya usimamizi wa bima katika nchi zote za Comesa.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuboresha utoaji wa huduma, kuharakisha ulipaji wa madai na kuongeza urahisi kwa wateja.
“Tumehimiza kuongeza ufanisi kwa sababu ufanisi hauna mwisho. Wanapaswa kubadili huduma zao kidijitali ili wateja wapate huduma kwa urahisi zaidi,” amesema Dk Saqware.