Dijitali kuzidi kuongeza matumizi ya bima

Muktasari:

  • Kupitia ubunifu wa kidijitali unaofanywa na watoa huduma mbalimbali akiwemo VodaBima wanaleta njia nafuu ya kupata huduma na kupunguza muda unaotumika kwa mtu, kupata huduma hiyo kutokana na matumizi ya simu.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) Dk Baghayo Saqware amesema watumiaji wa huduma za bima nchini wameongezeka kutokana na urahisi ulioletwa na maendeleo ya teknolojia.

Amesema hayo katika uzinduzi wa kampeni ya Vodacom ijulikanayo kama Bima kidijitali inayolenga kuongeza ujumuishi wa huduma za bima katika bidhaa tofauti.

 “Kupitia urahisi wa upatikanaji wa huduma za bima nina uhakika kwamba idadi ya watumiaji itaongezeka zaidi, maana kwa mwaka 2022, watumiaji wa bima walikuwa milioni 17.8 ambayo ni sawa na asilimia 28.9 ya Watanzania wote,” amesema Dk Saqware.

Amesema kupitia ubunifu wa kidijitali unaofanywa na watoa huduma mbalimbali akiwemo VodaBima wanaleta njia nafuu ya kupata huduma na kupunguza muda unaotumika kwa mtu, kupata huduma hiyo kutokana na matumizi ya simu.

 Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni amesema tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miaka miwili iliyopita, VodaBima imeuza zaidi ya bima milioni 1.5 kwa zaidi ya wateja 200,000 ikiwa ni jumla ya huduma za bima za magari, afya na maisha.

 "Huduma za bima ni muhimu kwa kila mtu kwa sababu inatuandaa kwa matukio ambayo hatukuyatarajia na kutuondolea wasiwasi tunapokutana na matatizo. Hakuna anayejua ni lini atakumbana na matatizo. Kwa hiyo, suluhisho pekee ni kuwa na bima ya kujilinda wewe na wapendwa wako," amesema Mbeteni.