Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fanya haya ili ufanikiwe mwaka 2026

Mwaka 2025 unapofikia tamati, ni wakati mzuri wa kujitathmini. Watanzania wengi tulianza mwaka tukiwa na malengo mazuri ya kifedha kama kuweka akiba, kupunguza madeni, kuanzisha biashara, kuwekeza au kusimamia fedha zetu kwa nidhamu.

Kwa baadhi ya watu, malengo haya yalitimia na kwa wengine yalipotea taratibu kutokana na changamoto za maisha ya kila siku.

Kujitathmini si kulaumu, bali ni kujifunza, kurekebisha mwelekeo na kuingia 2026 kwa umakini zaidi. Kwa wale waliofanikiwa kifedha mwaka 2025 kuna mambo ya msingi yanayoonekana wazi.

Kwanza, walikuwa na malengo thabiti na yanayotekelezeka. Badala ya kusema nitaweka akiba, waliweka lengo mahsusi kama kuweka akiba kiasi fulani kila mwezi au kulipa sehemu ya deni. Pili, walipanga kabla ya kutumia ambapo mapato yaligawanywa kwa kuzingatia mahitaji ya msingi, akiba na majukumu muhimu kabla ya matumizi ya hiari.

Tatu, nidhamu ilikuwa muhimu kuliko kiwango cha kipato. Hata watu wenye kipato kidogo waliweza kusonga mbele kwa kudhibiti matumizi na kuepuka mikopo isiyo ya lazima. Kwa upande mwingine, malengo mengi ya kifedha yalishindikana kwa sababu zinazoeleweka.

Sababu kubwa yaweza kuwa kutokufuatilia matumizi. Bila kujua fedha zinaenda wapi, matumizi madogo hugeuka kuwa tatizo kubwa. Changamoto nyingine yaweza kuwa kutegemea sana mikopo, hasa mikopo ya simu ambayo ni rahisi kuipata lakini ina gharama kubwa.

Shinikizo la kijamii pia laweza changia. Mfano michango ya sherehe mbalimbali kama harusi na kulinganisha maisha na wengine yaweza kuwa sababu ya matumizi kuzidi mipango, maradhi au ada za shule huenda zilituathiri kwa sababu hatukuwa na akiba ya dharura.

Je, nini kifanyike ili kufanikiwa 2026? Kwanza, fanya tathmini binafsi ya fedha zako. Kama ilivyo kwa taasisi kuandaa taarifa za mwaka, mtu binafsi anapaswa kuchambua mapato, matumizi, akiba, madeni na uwekezaji wake kwa uaminifu.

Je, uliweka akiba ya asilimia ngapi ya kipato chako? Madeni yalipungua kwa kiasi gani? Fedha zilipotelea wapi bila ulazima? Tathmini hii huleta uelewa na uelewa huleta mabadiliko. Pili, jenga akiba ya dharura, hata kama ni ndogo. Akiba hii inalinda juhudi zako pale changamoto zisizotarajiwa zinapotokea. Bila akiba, tukio moja linaweza kufuta maendeleo ya mwaka mzima.

Tatu, tenganisha mahitaji na tamaa. Mafanikio ya kifedha si kujinyima kupita kiasi, bali ni kupanga muda sahihi. Kuahirisha starehe leo kunaleta uhuru kesho, kuishi chini ya uwezo wako ni mkakati rahisi lakini wenye nguvu kubwa.

Nne, tumia mikopo kwa busara. Mikopo iwe kwa malengo yenye tija au manufaa ya muda mrefu, si kwa matumizi ya anasa au shinikizo la jamii. Ni muhimu kuelewa gharama halisi ya kukopa kabla ya kuchukua mkopo. Pia ni vizuri kufanya utafiti wa zaidi ya taasi moja za kutoa mikopo kufahamu ni taasisi ipi ina gharama nafuu.

Mwisho, weka malengo yako wazi na uyapitie mara kwa mara. Mipango hushindikana pale inapoandikwa mara moja kisha kusahaulika mapitio ya kila mwezi au robo mwaka husaidia kurekebisha mapema.

Tunapoelekea 2026, ujumbe ni mmoja kwamba mafanikio si ukamilifu, bali ni mchakato. Jifunze kutoka 2025, rekebisha nidhamu ya matumizi na songa mbele kwa kudhamiria. Mwaka bora kifedha hauanzi na kipato kikubwa bali unaanza na maamuzi bora.