Fanya haya kuepuka kuibiwa fedha zako mtandaoni

Muktasari:

  • Taarifa ya (BOT) iliyotolewa hivi karibuni kuhusu mwenendo wa upotevu wa fedha sekta ya benki mwaka 2023, imebainisha kuwa jumla ya Sh4.89 bilioni zimeibwa kupitia vitendo vya ulaghai au udukuzi uliofanyika kupitia huduma za benki kwa njia ya simu au benki mtandao (mobile & internet banking).

Fedha nyingi zimeibwa kimtandao kupitia huduma za benki kwa simu na benki mtandao.

Taarifa ya (BOT) iliyotolewa hivi karibuni kuhusu mwenendo wa upotevu wa fedha sekta ya benki mwaka 2023, imebainisha kuwa jumla ya Sh4.89 bilioni zimeibwa kupitia vitendo vya ulaghai au udukuzi uliofanyika kupitia huduma za benki kwa njia ya simu au benki mtandao (mobile & internet banking).

Njia nyingine ni upotevu uliosababishwa na wafanyakazi, ambapo Sh2.47 bilioni ziliibwa, upotevu kupitia mashine za ATM ilikuwa ni Sh741 milioni. Ulaghai wa hundi Sh1.01 bilioni, na upotevu mwingine ulikuwa Sh1.15 bilioni. Kwa ujumla, Sh10.2 bilioni.

Kuongezeka kwa visa hivyo ni ishara kuwa uhalifu wa kifedha umejibadili sura, kutoka ujambazi na utengezaji noti feki kwenda kwenye mifumo ya mtandaoni, Usalama utoaji wa huduma za kifedha kidijitali inapaswa kuwa jambo nyeti zaidi kwa miaka ya sasa.

Kuna mambo muhimu watumiaji wa huduma za kifedha mtandaoni kuzingatia ili kuweza kutambua vitendo vya uhalifu mtandaoni, itaisaidia pia kuepuka mianya inayoweza kupelekea kupoteza fedha.

Mtumiaji wa huduma kimtandao anapaswa kuweka neno siri au ‘password’ katika kifaa chake anachokitumia, ikiwa ni simu, kampyuta na kifaa kingine cha kielektroniki, pia, kuweka neno siri kwenye akaunti za fedha kimtandao mathalan za kibenki, au zile za mitandao ya simu.

Kuweka neno siri maana yake ni kulinda kifaa chako dhidi ya mwingine na ambaye hana nia nzuri inamzuia asiweze kupata taarifa zako kwa haraka. Kuna mazoea yetu kuweka neno siri kwa mfano tarehe yako ya kuzaliwa, jina lako, jina la mwenza, na mengine. Mtindo huu si mzuri, ni rahisi kuotewa kwa sababu wengi wanafanya hivyo.

Kwa upande mwingine, mtumiaji wa huduma za kifedha mtandaoni anatakiwa kutambua kuwa si salama kuweka taarifa zake katika kila kifaa. Kwa mfano; kuingia kwenye akaunti yako ya benki mtandao kupitia simu ya mtu, au compyuta ya ofisini.

Kufanya hivyo unaweza kuacha taarifa ambazo kwa mjuzi akiwa na nia mbaya anaweza kuzitumia kufanikisha lengo lake na ukapoteza fedha zako, hivyo ni muhimu mtu afanye hivyo kwa kifaa chake tu. Aidha, kama unatumia applikesheni (Mobile App) iwe ya benki au mitandao ya simu, ni vyema kuihuisha mara kwa mara, inasaidia kuongeza usalama wa akaunti yako (update).

Vilevile, mtumiaji wa huduma za kifedha mtandaoni asitoe taarifa zake muhimu kwa watu ambao hajawahakiki ili kuzuia kufichua taarifa binafsi. Kwa mfano, baadhi ya wakati inatokea wengine kujifanya wahudumu wa makampuni au taasisi za kifedha na kuomba taarifa kama jina lako, anuani yako, namba yako, taarifa zako za miamala, na mengine.

Hali kadhalika, mtumiaji awe makini kujibu baadhi ya jumbe kwa mfano, kuna “code” imeingia kwenye simu yako naomba nitumie, na mengine. Hiyo inaweza kuwa mitego, ambayo ukiingia kifaa chako kinaweza kudukuliwa mwishowe kupelekea kupoteza fedha zako.

Mtumiaji wa huduma za kifedha aepuke pia kufuata au kufungua kila kiunganisho (link), sambamba na kuepuka kuunganisha kifaa chako na kila huduma ya Wifi intaneti. Njia hizo si muda wote zinaweza kuwa salama, ni upenyo unaoweza kutumika na wenye nia ovu kuingilia taarifa za kifaa chako.

Kwa kumalizia, hifadhi taarifa za kadi yako ya benki ATM, hususani namba tatu za siri zilizo nyuma ya kadi yako (CVV), na tarehe ya kadi kuisha muda wake (expiry date), kwa mfano mtu yeyote akijua nambari ya akaunti yako ya benki, sambamba na hizo mbili nilizotaja kwa pamoja, anaweza kuzitumia kulipia huduma mtandaoni, kama unalo salio, fedha itakatwa kutoka kwenye akaunti yako.