Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

GGML yaahidi ajira zaidi kwa Watanzania

Ofisa Utumishi kutoka mgodi wa GGML, Ramadhan Burude akizungumza kuhusu mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi endelevu na umuhimu wa kulinda maslahi ya watumishi.

Muktasari:

  • Yasema kipaumbele ni kutoa ajira kwa wazawa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sheria

Geita. Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeahidi kutekeleza kwa vitendo Dira ya Taifa 2050 kwa kuweka kipaumbele cha asilimia 70 kwa sekta binafsi kufikia maendeleo endelevu kwa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa sambamba na elimu ya usalama kwa wakazi wanaozunguka mgodi huo.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa utumishi wa GGML, Ramadhan Burude mwishoni mwa wiki katika sherehe za Mei mosi mkoani Geita akisema mgodi huo unajivunia kuajiri zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania huku wengine wakiwa katika ngazi ya menejimenti ya kampuni hiyo.

“Kipaumbele chetu ni kutoa ajira kwa wazawa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya kutoa kipaumbele kwa wazawa na tutaendelea kufanya hivyo,” amesema Burude.

Amesema mbali na kutoa ajira kwa wazawa, kampuni hiyo pia imejikita katika matumizi ya teknolojia ya kisasa kwa ajili ya usalama mahala pa kazi na maeneo yanayozunguka mradi.

“Mgodi wa GGML hauhusiki tu na uchimbaji madini, bali pia kujali masilahi ya wafanyakazi kwa kutoa motisha na tuzo kwa watumishi mbalimbali ili kuongeza ushindani na uzalishaji kwa ajili ya maendeleo ya nchi,” amesema.

Burude amebainisha kuwa, GGML imekuwa ikitoa vifaa vya kisasa kwa wafanyakazi sambamba na elimu pindi anapoajiriwa na hata anapotoka likizo, ili kumwezesha mfanyakazi kutekeleza majukumu yake katika hali ya usalama.

Baadhi ya wafanyakazi kutoka idara tofauti waliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya vifurushi vya intaneti ili kuwawezesha kutuma taarifa na madokezo kwa waajiri wao kwa wakati.

Kutokana na kupanda kwa gharama za maisha nchini na baadhi ya watumishi kuishi mazingira ya vijijini, wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwenye kununua bando la intaneti huku vipato vyao vikiwa havikidhi uhitaji wao.

Ombi hilo lilitolewa na Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Geita, Pauline Tinda wakati akisoma risala kwa niaba ya Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi (Tucta).

Katika taarifa yake, Tinda amesema mifumo ya utendaji kwa watumishi wa Serikali Pepmis, imekuwa na changamoto wakati wa ujazaji wa taarifa na madokezo ya kiutendaji huku baadhi ya maeneo hasa ya vijijini, yakikabiliwa na mifumo duni ya intaneti.

"Watumishi huingia gharama kununua bando kwa kuwa wanalazimika kuingia kwenye mifumo kila siku ili kujaza taarifa na madokezo mbalimbali, pia baadhi ya maeneo kukosa mtandao kunasababisha watumishi kushindwa kuwazilisha taarifa zao kwa wakati,"amesema Tinda.

Akijibu risala hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela aliwaagiza wakurugenzi na maofisa utumishi mkoani humo, kutenga bajeti ya posho na motisha kwa wafanyakazi ili kuwarahisishia wafanyakazi utumaji wa taarifa kwenye mifumo kwa wakati huku Serikali ikiendelea kuboresha upatikanaji wa intaneti maeneo ya vijijini.

"Serikali imejipanga vizuri, mwezi wa nne ilizindua minara zaidi ya 700 katika maeneo yenye changamoto ya mtandao,lakini pia itaendelea kuboresha upatikanaji wa mtandao pamoja na nishati ili kila wilaya ifikiwe na mkongo wa Taifa wa mawasiliano," amesema Shigela.

Amewataka waajiri mkoani humo kudumisha mazungumzo na wafanyakazi kupitia uchambuzi wa mara kwa mara, kuhusu taasisi zao ili kutatua kero zibazowakabili watumishi wao kupitia uwazi.

Katika hatua nyingine, Shigela ametoa rai kwa wakurugenzi kutoa kipaumbele kwa watumishi wanaoomba vibali vya kwenda masomoni ili kuwapa motisha ya kufanya kazi zao kwa weledi kuendana na mabadiliko ya teknolojia.