Hawa ndiyo mabilionea 10 wa Soko la Hisa Dar es Salaam

Dar es Salaam. Wakati kampeni ya kuvutia wawekezaji wa rejareja wengi katika soko la hisa za ndani ikiendelea, uchambuzi uliofanywa na gazeti hili umebaini matajiri 10 vinara kwa kuwa na kiwango kikubwa cha mitaji sokoni.

Uchambuzi huo unatokana na ripoti za kila mwaka za kampuni zilizojiorodhesha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) pamoja na taarifa zinazopatikana mtandaoni.

Ripoti zilizorejewa ni zile za mwaka 2021 na mwaka 2022, ambapo makampuni huonyesha mchanganuo wa wanahisa wake na kiwango cha hisa wanachokimiliki.

Thamani ya uwekezaji ilikokotolewa kwa kuzingatia jumla ya mtaji wa soko wa kampuni husika kwa kiwango kilichokuwepo hadi Ijumaa ya Julai 21, 2023.

Hadi siku hiyo, wawekezaji hao 10 walikuwa na uwekezaji wenye thamani ya Sh208.2 bilioni, sawa na asilimia 1.37 ya mtaji wa jumla wa Soko la Hisa wa Sh15.12 trilioni.

Chanzo cha kuaminika ndani ya DSE kililithibitishia gazeti hili ukweli wa taarifa zilizokusanywa.

Miongoni mwa wanaotajwa katika orodha hiyo ni maarufu kutokana na biashara zao lakini wengine hawana umaarufu kibiashara, licha ya kuwa wana uwekezaji mkubwa katika kampuni mbalimbali.

Kwa mara ya kwanza orodha kama hii hii ilichapishwa na mtandao wa  unaofuatilia ukwasi wa watu maarufu, Billionaires.Africa.


Orodha yenyewe

 1. Patrick Schegg (Sh55.94 bilioni)

Kulingana na machapisho kadhaa ya mtandaoni na utafiti uliofanywa na gazeti hili, Patrick Schegg ambaye ni mfanyabiashara mbobezi wa masuala ya usimamizi wa mitaji na fedha, ndiye mwenye ukwasi mkubwa DSE.

Ripoti ya mwaka ya Benki ya NMB Plc (mwaka 2022) ilifichua kuwa Schegg ana asilimia 1.8 ya hisa katika taasisi hiyo kubwa ya kifedha ambayo ni sawa na hisa 9,000,390.

 NMB Plc mtaji wake katika soko hilo una thamani ya Sh1.73 trilioni kufikia Ijumaa wiki jana, ambayo inamaanisha thamani ya uwekezaji wa Schegg katika benki hiyo ni takriban Sh31.14 bilioni.

  Mwekezaji huyo pia ana hisa 50,754,057 katika benki ya CRDB, sawa na asilimia 2 ambazo zina thamani ya Sh24.8 bilioni. Thamani ya hisa za CRDB DSE ni Sh1.24 trilioni.


2. Aunali Rajabali (Sh53.8 bilioni)

Namba mbili inashikiliwa na mwenyekiti na mbia wa Kampuni ya Megapipes Solutions Ltd ya nchini Kenya ambaye  pia ni mwenyekiti na mbia wa Plasco Ltd ya Tanzania, ambayo inajihusisha na uzalishaji wa vifaa vya ujenzi na uhifadhi wa maji.

Mfanyabiashara huyo anamiliki asilimia 3.11 ya hisa za Benki ya NMB Plc ambazo ni sawa na hisa 15,533,731. Kulingana na thamani ya sasa uwekezaji huo unakadiriwa kuwa Sh53.8 bilioni.


3. Sajjad Rajabali (Sh53.8 bilioni)

Mwingine ni mwanahisa na mkurugenzi asiye mtendaji wa Megapipes Solutions Ltd nchini Kenya ambaye pia ni mwanahisa na Mkurugenzi wa Plasco Ltd nchini.

 Sajjad anamiliki asilimia 3.11 kwenye Benki ya NMB Plc, sawa na hisa 15,534,030,  hivyo uwekezaji wake sokoni unakadiriwa kuwa na thamani ya Sh53.8 bilioni.


4. Hans Macha (Sh16.12 bilioni)

Huyu ni mfanyabiashara mzawa ambaye kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2022 ya Benki ya CRDB Plc anamiliki hisa 32,764,200 sawa na asilimia 1.3.

 Kwa kiwango hicho cha hisa, thamani ya uwekezaji wake katika CRDB unakadiriwa kuwa Sh16.12 bilioni.


5. Sayeed Kadri na familia yake (Sh8.36 bilioni)

Yeye na watu wengine wanne wa familia ya Kadri (/Basharat Kadro/Mehboob Kadri/ Khalid/Muzammil Kadri) wanamiliki 0.59 ya hisa za kampuni ya Tanzania Portland Cement Company Limited (Twiga Cement), hii ni kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2021 ya kampuni hiyo.

Kampuni ya Twiga imeweka sokoni mtaji wa jumla wa Sh741.28 bilioni, hivyo thamani ya uwekezaji wa Sayeed na familia yake katika Twiga Cement ni takriban Sh4.37 bilioni.

 Ripoti ya mwaka 2021 ya Swissport Tanzania pia ilionyesha kuwa Sayeed Kadri na Basharati Kadri wanamiliki asilimia moja ya kampuni.

Kwa kuzingatia mtaji wa Swissport sokoni ambao ni Sh59.04 bilioni, uwekezaji wa Kadri katika kampuni hiyo ya kuhudumia ndege ni takriban Sh590.4 milioni.

Vilevile, yeye na familia yake wanamiliki asilimia 0.2 ya Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) kwa ripoti ya mwaka 2022. Mtaji wa TCC sokoni ni Sh1.7 trilioni, hivyo jumla ya uwekezaji wa Kadris unakadiriwa kuwa thamani ya Sh3.4 bilioni.6. Murtaza Nasser (Sh6.67 bilioni)

Nasser yeye anamiliki asilimia 0.9 ya Kampuni ya Saruji ya Tanzania Portland Cement Limited (Twiga Cement), kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2021.

 Hivyo thamani ya uwekezaji wa Murtaza Nasser katika Twiga Cement ni takriban Sh6.671 bilioni.


7. Ernest Massawe (Sh5.65 bilioni)

Huyu anamiliki asilimia 15.86 katika kampuni ya Kitanzania ya utengenezaji na usambazaji wa gesi za viwandani na hospitalini (TOL), hii ni kwa mujibu wa ripoti ya kampuni hiyo hadi mwishoni mwa mwaka 2022.

Jumla ya mtaji wa TOL sokoni ni Sh35.65 bilioni, hivyo uwekezaji wa Massawe katika kampuni hiyo unatajwa kuwa takriban Sh5.65 bilioni.


8. Said Bakhresa (Sh3.78 bilioni)

Huyu ni tajiri maarufu nchini kutokana na umaarufu wa chapa zake, hususan bidhaa za viwandani na huduma za usafiri na televisheni na uwekezaji katika timu ya soka.

Hata hivyo, Bakhresa yupo kote, katika soko la hisa anashikilia namba nane kwa mujibu wa taarifa zilizopo.

Taarifa hizo zinaonyesha hadi mwaka 2021 alikuwa anamiliki asilimia 0.51 ya hisa za kiwanda cha saruji cha Twiga.

Kwa kuzingatia kuwa mtaji wa Twiga Cement ulioko sokoni, uwekezaji wa Bakhresa katika kampuni hiyo una thamani ya takriban Sh3.78 bilioni.


9. Arnold Kilewo (Sh2.53 bilioni)

Kulingana na ripoti ya mwaka ya TOL Gases ya 2022, anamiliki hisa 3,264, 144 sawa na asilimia 5.68 za kampuni hiyo ya usambazaji wa gesi nchini.

 Kwa uwekezaji wake ndani ya TOL, Kilewo hisa zake zina thamani ya takriban Sh2.122 bilioni.

 Vilevile yuko kwenye bodi ya wakurugenzi ya Kampuni ya bia ya Tanzania Breweries Limited (TBL) akiwa na hisa 37,641 kwa mujibu wa ripoti ya kampuni hiyo ya mwaka 2022.

Kwa bei ya soko ya Sh10,900 kwa kila hisa, uwekezaji wake katika TBL ni takriban Sh409.64 milioni.


10. Harold Temu (Sh1.55 bilioni)

Huyu ana hisa 2,507,740 katika kampuni ya TOL sawa na asilimia 4.36 kulingana na ripoti ya mwaka ya 2022.

Kwa thamani ya soko, uwekezaji huo wa Temu una thamani ya takriban Sh1.55 bilioni.

Hata hivyo, mchambuzi wa uwekezaji wa soko la hisa wa kampuni ya udalali ya Orbit Security, Ammi Julian anasema nchini Tanzania mabilionea wachache wanaweka fedha zao DSE kwa sababu ya utamaduni wa kibiashara nchini.

“Hata hao wachache waliopo wana mitaji kiduchu katika soko, ni kwa kuwa kwa asili wafanyabiashara wetu wakihitaji mtaji wanatafuta mkopo binafsi, tofauti na wenzetu ambao huweka sokoni sehemu ya umiliki wa uwekezaji wao,” alisema Julian.

Anasema ili kuongeza ushiriki wa wazawa na kuongeza mabilionea wengi zaidi sokoni, kinachotakiwa ni kupunguza ugumu wa kuorodhesha kwa kampuni sokoni ili kuvutia wajasiriamali wachanga wanaosaka mitaji.

“Hizi startup ni mabilionea wa kesho, tukikua nao sokoni tutaongeza mabilionea katika soko la hisa. Wanasaka mitaji, wakiwekewa urahisi wa kuingia sokoni na biashara zao zikakua manufaa yake ni makubwa.”