Mambo matatu ili kupata rasilimali watu yenye tija Tanzania

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Phillip Mpango. Picha na mtandao.

Muktasari:

  • Mapendekezo hayo yanakuja wakati ambao, nchi za Afrika zinatajwa kuwa na hali ngumu ya kufikia lengo la kuwa na rasilimali watu yenye tija, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu.

Dar es Salaam. Uwekezaji katika sekta ya elimu, ufadhili wa taasisi za fedha, kujenga uwezo wa ndani na ushirikishwaji wa sekta binafsi ni miongoni mwa mapendekezo ya Tanzania katika kuwezesha nchi za Afrika kuwa na rasilimali watu yenye tija.

Mapendekezo hayo yanakuja wakati ambao, nchi za Afrika zinatajwa kuwa na hali ngumu ya kufikia lengo la kuwa na rasilimali watu yenye tija, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu.

Hali hiyo ndiyo iliyosababisha haja ya Wakuu wa nchi za Afrika kukutana na kujadili ili kutoka na kauli moja juu ya namna ya kutengeneza rasilimali watu yenye tija.

Mkutano huo ulioanza jana kwa kukutanisha Mawaziri wa kisekta waliojadili hilo, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, na unafuatiwa na ule wa Wakuu wa nchi unaofanyika leo.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo uliohusisha mawaziri wa kisekta Afrika, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto ya kifedha kufikia lengo tarajiwa.

Kwa kutambua changamoto hiyo, amesema kuna haja taasisi za kifedha za kikanda na Afrika, kubuni mbinu za kuzifadhili nchi zake, kuhakikisha zinakuwa na maendeleo ya rasilimali watu.

“Uwekezaji katika rasilimali watu unachukua muda mrefu na hivyo inahitaji gharama nafuu lakini uvumilivu wa muda mrefu,” amesema Dk Mpango.

Pendekezo la lingine, alisema kwa kuwa sekta binafsi ni mnufaika mkubwa wa maendeleo ya rasilimali watu, na kwamba mkutano huo utumike kutafuta mbinu za kuivutia ili ishirikiane na Serikali katika kufanikisha hilo.

Amezitaka taasisi za mafunzo katika bara la Afrika ziwe chachu ya kujenga uwezo wa rasilimali watu itakayotumika na kusaidia kuimarisha rasilimali za nchi.

“Kwa bahati mbaya Afrika inatumia sehemu kubwa ya fedha zake, kuhakikisha inaagiza ujuzi kutoka nje kwa ajili ya kutumika kutumia utajiri wa rasilimali zetu za ndani,” amesema.

Hata hivyo, Dk Mpango amesema ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu imebainisha mazingira magumu zinayopitia nchi za Afrika katika kufikia lengo la maendeleo ya rasilimali watu.

Kilichoelezwa na Dk Mpango kinasisitizwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliye elezea juu ya haja ya sekta ya elimu kufanywa kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya rasilimali watu.

“Kwa kutambua umuhimu wa kuwapa vijana wetu ujuzi wa vitendo, Tunasisitiza sana kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi,” amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolfu Mkenda, amesema maendeleo ya rasilimali watu si wingi wa binadamu katika taifa, bali ni kile kilichowekezwa ndani ya watu ili wawe wa tija.

“Kwenye haya elimu ni muhimu, afya, lishe na mengine lukuki lakini haya ndiyo muhimu zaidi,” ametanabaisha.

Aidha, waziri huyo mwenye dhamana ya elimu amema ili kuimarisha sekta ya elimu ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya rasilimali watu, ni muhimu kuwekeza zaidi kwenye elimu kuanzia kwa watoto wadogo.

Akichangia mjadala huo, Waziri wa Hazina nchini Kenya, Profesa Njuguma Ndung’u, amesema kuna haja ya kuwa na lishe bora kwa nchi za Afrika, ili kuwa na vijana wenye nguvu na uwezo wa kuwa rasilimali watu yenye tija.

Hata hivyo, waziri huyo amezitupia mzigo taasisi za elimu barani Afrika kwa kusema kuwa zinazalisha wataalamu wasio na sifa za kutumika kama rasilimali watu.

Akizungumzia uwezeshaji wa wanawake katika maendeleo ya rasilimali watu, Waziri wa Jinsia, Watoto na Jamii kutoka Ghana, Lariba Abudu amesema elimu, afya na ujasiriamali ndiyo msingi muhimu katika hilo.

“Naweza kuthibitisha kwamba wanawake wote waliopo humu ni wasomi na wanaendelea kusoma kwa sababu kusoma ni mchakato,” amesema.

Katika hilo, amebainisha kuwa pale mtot wa kike anapoelemishwa, ni vema kuwaeleimisha pia wakubwa kwa wazee, kwa mantiki kwamba wote wanategemeana.

Waziri Abudu amesisitiza umuhimu wa kuifanya elimu ifikiwe na wote bila kujali ulemavu, jinsia na jambo lolote linalotazamwa kama kikwazo cha elimu kwa mtu.

“Tunapaswa kuanzisha Tehama kwenye shule zetu, sisi Ghana tuna vyumba maalum vya Tehama kwenye shule zetu nyingi, hii itasaidia kuzalisha watu wa ujuzi mbalimbali,” amesema.