Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii hapa sababu bei ya nyama kupaa Tanzania

Muktasari:

  • Ripoti ya Takwimu Msingi za Tanzania zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa uzalishaji wa nyama ulitoka tani 738,166 mwaka 2020 hadi kufikia tani mwaka 1,054,114 mwaka 2024.

Dar es Salaam. Wakati uzalishaji wa nyama nchini ukiongezeka kwa asilimia 42.8 kati ya mwaka 2020 hadi 2024, soko la uhakika limetajwa kuwa sababu ya ukuaji huo.

Ripoti ya Takwimu Msingi za Tanzania zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) 2024, inaonesha kuwa uzalishaji wa nyama ulitoka tani 738,166 mwaka 2020 hadi kufikia tani mwaka 1,054,114 mwaka 2024.

Kwa mujibu wa NBS uzalishaji huo ni kwa nyama ya ng’ombe, mbuzi, kondoo kuku na nguruwe.

Akizungumza na Mwananchi, Said Mchanjama ambaye ni muuzaji wa ng’ombe kwa jumla amesema uwepo wa soko la uhakika ndani na nje ni sababu ya kuongezeka kwa uzalishaji unaofanywa katika maeneo mbalimbali.

“Soko lipo, sisi kama wauzaji wa mifugo tunaona kasi ya ununuaji inavyoongezeka tofauti na zamani, sasahivi kuna viwanda vinavyosindika pia kwa ajili ya soko la ndani na nje,” amesema.

Wakati Saidi akisema hayo, ujumbe wa wawekezaji kutoka Oman umekuja nchini kuangalia fursa za uwekezaji katika uzalishaji na usafirishaji wa nyama ili kusaidia kukidhi mahitaji ya soko lao.

Mbali na nyama, pia wameonesha nia ya kuwekeza katika usafirishaji wa nyama na bidhaa mbalimbali za kilimo kutoka Tanzania.

Akizungumza Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angela Ngalula amesema Oman ina mahitaji makubwa ya bidhaa za kilimo na katika ziara yao, wawekezaji wametembelea viwanda vya kuchakata nyama na tayari wameonesha nia ya kuwekeza.

Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi (TPSF), Angela Ngalula akizungumza katika mkutano na wawekezaji kutoka Oman,uliofanyika jijini Dar es Salaam, kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah. Picha na Michael Matemanga

“Wameonesha nia ya kuanza kusafirisha nyama kutoka Tanzania. Baadhi ya makubaliano tayari yameshasainiwa na tuna matumaini kuwa mikataba mingine mingi itafikiwa hasa katika sekta ya viwanda,” amesema.

Ujumbe huo, uliowasili nchini Jumapili, umetembelea maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa lengo la kuangalia fursa za biashara na uwekezaji.

Ziara hii imefanyika baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutembelea nchini Oman ambapo alialika wawekezaji wa Oman kuchunguza fursa za kibiashara zilizopo Tanzania.

“Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Serikali imefanya maboresho makubwa katika mazingira ya biashara. Ndiyo maana sasa tunashuhudia ongezeko la ujumbe kutoka nchi mbalimbali, ikiwamo Oman, unaokuja kuangalia fursa za uwekezaji nchini,” ameongeza.

Aidha, amebainisha kuwa ujumbe wa Oman pia umealika wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza nchini mwao.

Maeneo yaliyoainishwa kwa ushirikiano ni pamoja na kilimo, ujenzi, viwanda, usafirishaji na vifaa vya usafiri, utalii na usafiri wa anga, mbao na umeme wa maji, mbuga za viwanda na maeneo maalum ya kiuchumi, mifugo, utengenezaji wa chuma, madini, utalii wa kilimo na uchumi wa buluu.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Dk Godwill Wanga amesema wamejiandaa vizuri kusaidia shughuli za kiuchumi hasa katika kipindi hiki ambacho mvuto wa Tanzania kwa wawekezaji wa kigeni umeongezeka.

Dk Wanga amesema Tanzania imekuwa ikifanya midahalo ya mara kwa mara kati ya sekta ya umma na binafsi (PPDs) ili kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

“Tunalenga ongezeko la kila mwaka la asilimia 10 katika uwekezaji wa kigeni, ambalo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi. Tanzania ina maeneo maalumu ya kiuchumi katika mikoa mbalimbali, yakitoa fursa nyingi kwa wawekezaji,” amesema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda ya Tanzania, Dk Hashil Abdallah amesema Serikali ipo tayari kuwezesha kila fursa ya uwekezaji nchini Tanzania na pia nchini Oman.