Hizi hapa fursa magari ya umeme kuanza kuja Tanzania
Muktasari:
- Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27, imependekeza punguzo la kodi katika magari ya umeme yanayoingizwa nchini.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikipendekeza punguzo la kodi katika magari yanayotumia umeme, wadau wa sekta ya magari ya umeme wameonyesha dalili za kuwa miongoni mwa wanufaika wa mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2026/27.
Kampuni ya Zera inayoingiza magari ya umeme nchini, imetangaza mpango wa kupanua matumizi ya magari hayo nchini, sambamba na kuongeza vituo vya kuchajia magari hayo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Akizungumzia hilo, Meneja wa Masoko wa Zera inayoingiza magari ya umeme nchini, Samuel Masawe, amesema tayari wameingiza zaidi ya magari 2,000 katika soko la Dar es Salaam na sasa wanalenga kupanua huduma katika mikoa mingine.
Amesema changamoto inayobaki ni upatikanaji wa miundombinu ya kuchajia magari hayo, lakini kampuni hiyo inaendelea kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuongeza vituo vya huduma hiyo.
“Tunataka kuona vituo vya kuchajia magari ya umeme vinapatikana kwa urahisi kama ilivyo kwa vituo vya mafuta. Hii itasaidia kuondoa hofu ya watumiaji kuhusu uwezo wa magari hayo kusafiri umbali mrefu,” amesema Masawe.
Amesema mipango yao kwa sasa ni kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari ya umeme nchini, jambo litakalopunguza gharama za umiliki wa magari hayo, kuongeza ajira kwa vijana, kukuza ujuzi wa teknolojia na kuimarisha sekta ya viwanda.
“Tunataka kuwapa Watanzania chaguo la usafiri linalopunguza gharama za uendeshaji. Umeme unapatikana kwa wingi nchini na una gharama nafuu ikilinganishwa na mafuta, hivyo kufanya matumizi ya magari ya umeme kuwa ya manufaa zaidi,” amesema.
Masawe amesema magari hayo hutumia umeme pekee bila kuhitaji mafuta, jambo linalopunguza kwa kiasi kikubwa gharama za matengenezo na uendeshaji.
Ameeleza gari moja linaweza kusafiri hadi kilomita 320 baada ya kuchajiwa kikamilifu.
Akizungumzia hilo, Mtaalamu wa Nishati Safi ya Magari, Manala Mbumba, amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje, huku ikichochea matumizi ya umeme unaozalishwa nchini.
“Mbali na kupunguza gharama za uendeshaji kwa watumiaji, magari ya umeme yatapunguza uzalishaji wa hewa chafu inayochangia mabadiliko ya tabianchi,” amesema.