Kamati ya Bajeti: Hatua za kubana matumizi Bajeti 2026/27 hazitekelezeki
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mashimba Ndaki, akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Juni 15, 2026 wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Picha na Said Khamis.
Muktasari:
- Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, imeonyesha mashaka kwenye utekelezaji wa hatua zilizotajwa na Serikali katika kubana matumizi.
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, imesema imebaini hatua za kubana matumizi zilizowasilishwa na Serikali katika bajeti yake ya mwaka 2026/27, zinafanana na ambazo inazitaja miaka yote na zimekuwa hazitekelezeki.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mashimba Ndaki, amesema kamati hiyo pia, imebaini baadhi ya hatua hizo hazilengi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Maoni hayo ya kamati yanakuja siku tano tangu Serikali iwasilishe bajeti yake ya Sh62.3 trilioni kwa ajili ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Katika bajeti hiyo, Serikali imesema itafanya mageuzi ya kidijitali na kudhibiti matumizi ya safari za nje na ndani, kupunguza semina, warsha na makongamano yenye gharama kubwa ili kubana matumizi.
Ndaki, ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma leo, Jumatatu Juni 15, 2026 alipowasilisha mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema kamati imefanya uchambuzi wa aya ya 67 ya hotuba ya bajeti hiyo inayoonyesha dhamira ya Serikali katika kusimamia matumizi ya fedha za umma na kubana matumizi.
Baada ya uchambuzi huo, amesema kamati imebaini hatua za kubana matumizi zilizowasilishwa ni zilezile ambazo Serikali imekuwa ikizitaja miaka yote na baadhi hazitekelezeki.
“Baadhi ya hatua hizo hazilengi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, baadhi ya maofisa masuuli kutotekeleza vema sheria ya usimamizi wa fedha na umma, maandalizi hafifu ya miradi ya maendeleo inayosababisha gharama za miradi kutoendana na thamani ya fedha,” amesema.
Hata hivyo, amesema uzoefu unaonyesha kubana matumizi yasiyo ya lazima ni njia bunifu na ya uhakika inayotumika na nchi nyingi ili kuweka nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.
Aidha, ameeleza njia hiyo inawezesha kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo endapo kuna upungufu wa rasilimali fedha.
“Mifano ya nchi zilizotumia mkakati wa kubana matumizi ni pamoja na Afrika Kusini, Zambia na Ivory Coast. Kamati inaitaka Serikali kupitia upya bajeti ya matumizi ya kawaida na kupunguza matumizi ambayo hayawezi kuathiri utekelezaji wa bajeti,” amesema.
Hatua hiyo, Ndaki ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi amesema itasaidia kupata fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.