Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Omar: Bajeti 2026/27 kuwanufaisha wananchi

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27, itakayowasilishwa bungeni kesho jijini Dodoma. Picha na Said Khamis.

Muktasari:

  • Kesho Juni 11, 2026 Serikali inatarajiwa kuwasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema bajeti ya mwaka 2026/27 itakayowasilishwa bungeni jijini Dodoma kesho Alhamisi, Juni 11, 2026, imejikita kuwanufaisha zaidi wananchi kupitia vipaumbele vipya vya maendeleo na uboreshaji wa ukusanyaji mapato.

Kauli hiyo ya Serikali, inakuja siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27. Bajeti hiyo inatarajiwa kuwa Sh61.93 trilioni.

Hayo yameelezwa leo, Jumatano, Juni 10, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alipokuwa akitoa maelezo ya awali kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali yenye thamani ya Sh62.3 trilioni, jijini Dodoma.

Amesema bajeti hiyo imezingatia mikakati ya muda mrefu ya maendeleo pamoja na mazingira ya uchumi wa ndani na kimataifa.

Balozi Omar, amesema uwasilishaji wa bajeti hiyo unakwenda sambamba na makubaliano ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayowataka mawaziri wa fedha kuwasilisha mapendekezo ya bajeti kwa siku na muda mmoja, kila Alhamisi ya pili ya mwezi Juni.

Pia, amesema mchakato huo unalenga kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Amesema Bajeti ya 2026/27 ni ya kipekee kwa kuwa inaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025.

Akizungumzia utekelezaji wa bajeti inayoendelea, Balozi Omar amesema Serikali imepata mafanikio katika ukusanyaji wa mapato ya ndani yaliyofikia lengo, huku akibainisha kuwa matumizi yamekabiliwa na changamoto zilizohitaji uangalizi wa karibu.

Kwa mwaka 2025/26, amesema sehemu kubwa ya matumizi yatagharamiwa na mapato ya ndani yanayokadiriwa kufikia Sh46.8 trilioni.

Amesema kipaumbele kimewekwa katika miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR, miundombinu ya barabara, sekta ya maji, nishati na maendeleo ya rasilimali watu.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27, itakayowasilishwa bungeni kesho jijini Dodoma. Picha na Said Khamis.

Katika hatua ya kuimarisha mfumo wa kodi, amesema Serikali ilipokea jumla ya mapendekezo 727 kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu, asasi za kiraia na wananchi. Mapendekezo hayo yalihusu maboresho ya kodi, ada na tozo mbalimbali.

Kati ya mapendekezo hayo, amesema 125 yalikubaliwa kama yalivyowasilishwa, 121 yakaboreshwa kabla ya kupitishwa, 295 yakakataliwa, 107 yakapelekwa kwa taasisi husika kwa uchambuzi zaidi, 47 yakabaki bila uamuzi kutokana na upungufu wa takwimu, huku 32 yakiwa katika hatua za utekelezaji.

Amesema Serikali inaendelea kupokea ushauri kupitia Kamati ya Kiufundi ya Maboresho ya Kodi inayojumuisha wataalamu kutoka sekta za umma na binafsi pamoja na taasisi za utafiti.

Amesisitiza lengo la maboresho hayo ni kuongeza wigo wa kodi, kuvutia uwekezaji, kupunguza mzigo kwa walipa kodi na kuongeza ajira.

Amesema Serikali itaweka mkazo katika matumizi yenye tija na kuziba mianya ya upotevu wa mapato.

Kabla ya kuwasilishwa kwa bajeti kuu, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, atawasilisha taarifa ya hali ya uchumi itakayoonyesha mwenendo wa ukuaji wa Pato la Taifa, mfumuko wa bei, sekta ya nje na kiwango cha akiba ya fedha za kigeni.