Kamati ya Bunge: Ushuru bodaboda, magari chakavu kuwaumiza vijana na maskini
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mashimba Ndaki, akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Juni 15, 2026 wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Picha na Said Khamis.
Muktasari:
- Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeitaka Serikali kutafakari upya mapendekezo yake matatu katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27.
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, imeitaka Serikali kutafakari upya mapendekezo yake ya ongezeko la ushuru wa bidhaa katika pikipiki na magari chakavu yenye umri wa miaka minane hadi 10 na 10 hadi 20.
Aidha, kamati hiyo, imeitaka Serikali itafakari upya pendekezo lake la mabadiliko ya sheria nne zinazohusiana na kodi katika madini, ikisema yanarejesha utaratibu wa mikataba ya makubaliano iliyoliingiza Taifa kwenye hasara.
Katika bajeti hiyo ya Sh62.3 trilioni, Serikali ilipendekeza mabadiliko katika Sheria ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Sura ya 147, Sheria ya Kodi ya Mapato Sura ya 332, Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta Sura ya 220 na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura ya 148.
Mapendekezo hayo, Serikali ilisema yanalenga kuondoa matumizi ya sheria hizo kwenye kampuni za madini ambazo Serikali itaingia nazo mikataba, badala yake makubaliano yaliyo kwenye mikataba ndiyo yatatumika katika utozaji kodi.
Pia, Serikali ilipendekeza kuongeza ushuru wa bidhaa kwa asilimia tano katika bodaboda na ushuru wa magari chakavu kutoka asilimia 15 hadi 20 kwa magari yenye umri wa miaka nane hadi 10 na kutoka asilimia 30 hadi 40 kwa magari yenye miaka 10 hadi 20 na yanayozidi 20 asilimia 50.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma leo, Jumatatu Juni 15, 2026 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mashimba Ndaki, alipowasilisha mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema Serikali itafakari upya mapendekezo yake ya kuongeza ushuru wa bidhaa kwa asilimia tano kwenye pikipiki za matairi mawili na kupandisha ushuru wa magari chakavu kutoka asilimia 15 hadi 20 kwa magari yenye umri kati ya miaka minane hadi 10.
“Kamati inaitaka Serikali kwenda kutafakari upya mapendekezo yake kwa sababu kuu mbili kwanza pikipiki zimetoa fursa ya ajira kwa vijana wengi na zinanunuliwa zikiwa mpya,” amesema.
Sababu ya pili, amesema wananchi wa kipato cha chini ndio wanunuzi wakubwa wa magari chakavu, kiwango kinachopendekezwa cha ushuru ni kikubwa kitaathiri sio tu bei ya pikipiki hizo, bali ajira za vijana wanaojiajiri kupitia biashara ya kusafirisha abiria na uwezo wa mwananchi mwenye kipato cha chini kumiliki gari.
“Kamati bado inataka Serikali kutafakari zaidi mapendekezo hayo,” amesema.
Aidha, ameitaka Serikali kutafakari upya mapendekezo yake kwa sababu yanarejesha utaratibu wa mikataba ya makubaliano ambayo iliingiza hasara katika Taifa, kwani baadhi ilikuwa na vifungu vya mwendelezo wa kutolipa kodi.
“Madini ni rasilimali inayokwisha tusipokuwa makini tutabaki na mashimo ya madini bila kupata kodi ya aina yoyote. Uamuzi huu ni vyema ukaangaliwa upya,” amesema Ndaki, aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Ametaka Bunge litambue kwamba kwa kupitisha mabadiliko hayo ni wazi kwamba linakasimu mamlaka yake ya kutunga sheria za kodi kama ilivyoelekezwa katika ibara ya 138 ya Katiba kwa Baraza la Mawaziri.