Shabiby ataka chombo maalumu kuchunguza matumizi ya Serikali
Muktasari:
- Pamoja na umuhimu wa kuongeza ukusanyaji wa mapato, Serikali inapaswa kuweka nguvu sawa katika kusimamia matumizi ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Wizara ya Fedha kwenda kwenye wizara nyingine au taasisi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Dar es Salaam. Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby ameishauri Serikali kuanzisha chombo maalumu cha kuchunguza matumizi ya fedha katika wizara, taasisi na miradi ya maendeleo kabla ya kuendelea kutoa fedha zaidi, akisema hatua hiyo itasaidia kudhibiti matumizi yasiyo na tija na kuongeza ufanisi wa fedha za umma.
Wakati Shabiby akieleza hayo, Mbunge wa Bariadi Vijijini (CCM), Massanja Kadogosa amesema ili kufikia ukuaji wa uchumi wa asilimia 10 ni lazima kuwa na ukuaji mdogomdogo huku akisema vipaumbele vilivyowekwa ni moja ya njia ya kufikia ukuaji huo.
Wabunge hao wamesema hayo wakati wakichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 ya Sh62.3 trilioni sambamba na Hali ya Uchumi wa Tanzania 2025 bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu, Juni 15, 2026.
Shabiby amesema pamoja na umuhimu wa kuongeza ukusanyaji wa mapato, Serikali inapaswa kuweka nguvu sawa katika kusimamia matumizi ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Wizara ya Fedha, kwenda kwenye wizara nyingine au taasisi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Amesema kuna haja ya kuwa na mfumo utakaofuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi kabla ya fedha mpya kutolewa.
“Lazima kuwe na chombo maalumu kinachokwenda kujiridhisha kwanza. Muangalie hili daraja, kweli Sh10 bilioni zimetumika? Kama Sh5 bilioni zimetumika kweli tupeleke nyingine, msipoangalia itakuwa hela zinachukuliwa lakini matumizi yatakuwa mengine,” amesema.
Mbunge huyo amesema bila kuwa na mfumo madhubuti wa kudhibiti matumizi, Serikali inaweza kujikuta ikiongeza makusanyo ya mapato huku fedha nyingi zikipotea kupitia matumizi yasiyo ya lazima.
Alitolea mfano wa matengenezo ya magari binafsi na ya Serikali, akisema wakati gari inayomilikiwa na mbunge inaweza kutumia kati ya Sh20 milioni hadi Sh30 milioni katika matengenezo ndani ya miaka mitano.
Mbunge wa Gairo (CCM), Ahamed Shabib akizungumza wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027 bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis
“Ni mfano, lakini gari hiihii kipindi hichohicho likiwa linamilikiwa na Serikali gharama za matengenezo zinaweza kuwa karibu nusu ya thamani ya gari lenyewe. Zipo sehemu nyingi ambazo matumizi yake yanakuwa makubwa, tunapokusanya fedha, tunapotoa ushauri wa mapato na matumizi yake yawe yanaangaliwa kiasi cha kutosha,” amesema.
Shabiby amesema mjadala wa mapato haupaswi kuishia katika namna ya kukusanya fedha pekee bali pia namna ya kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo amehoji uamuzi wa Serikali kuendelea kutoza ushuru wa asilimia tano kwenye pikipiki huku akitaka jambo hilo kuangaliwa upya, kwani vyombo hivyo vimekuwa nyenzo muhimu ya usafiri na shughuli za kiuchumi hasa vijijini.
Katika bajeti iliyosomwa Juni 11, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar alipendekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia tano kwenye pikipiki isipokuwa (motorcycle za wagonjwa wa dharura ambulances), pikipiki zinazotumia gesi asilia pamoja na za umeme.
Lengo la hatua hiyo ni kuendana na malengo ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwenye vyombo vya moto nchini, huku ikitarajiwa kuongeza mapato ya Serikali Sh30.40 bilioni.
Akizungumzia suala hili, Shabiby amesema kwa hali ya sasa pikipiki si bidhaa za anasa kama ilivyokuwa miaka iliyopita bali zimekuwa sehemu muhimu ya uchumi wa wananchi.
“Huko vijijini pikipiki ndiyo gari la wagonjwa, ndiyo usafiri wa kubeba mazao na mizigo. Leo hii pikipiki ndiyo mbadala wa baiskeli kwa wananchi wengi ni vyema Serikali kufikiria kuondoa ushuru huo ili kupunguza gharama kwa wananchi na kuongeza upatikanaji wa vyombo hivyo,” amesema.
Pia alionyesha wasiwasi juu ya misamaha ya kodi inayotolewa kwa viwanda vya kuunganisha pikipiki nchini akisema manufaa yake kwa wananchi bado hayaonekani kwa sababu bei za zimeendelea kubaki juu licha ya motisha hizo za kikodi.
“Kwa kawaida pikipiki kila kitu kinakuja kwenye boksi kutoka nje ya nchi na inaunganishwa hapa, hili linafanyika wakati ambao hakuna tairi wala spoku inayotumika ambayo imetengenezwa Tanzania,” amesema.
Katika hatua nyingine, Shabiby aliitaka Serikali kupitia upya utaratibu wa utoaji wa leseni kwa waendesha bodaboda akisema gharama za sasa ni kubwa na zinachangia idadi kubwa ya waendesha pikipiki kutokuwa na leseni.
Kwa sasa bodaboda analazimika kulipa takribani Sh183,000 kuanzia mafunzo, mitihani na ada mbalimbali kabla ya kupata leseni.
“Hii inafanya asilimia 90 ya waendesha bodaboda hawana leseni. Si kwa sababu hawataki, bali kwa sababu gharama ni kubwa na mchakato ni mrefu. Tukirahisisha utaratibu na kupunguza gharama, Serikali inaweza kukusanya mapato mengi zaidi,” amesema.
Mbunge wa Bariadi Vijijini, Masanja Kadogosa akizungumza wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027 bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis
Alichokisema Kadogosa
Kwa upande wake mbunge wa Bariadi Vijijini (CCM), Massanja Kadogosa amesema ili kufikia ukuaji wa uchumi wa asilimia 10 ni lazima kuwa na ukuaji mdogomdogo huku akisema vipaumbele vilivyowekwa ni moja ya njia ya kufikia ukuaji huo.
Akizungumza moja ya jambo zuri lililofanyika ni msamaha wa kodi kwa mwaka mmoja kwa watu wanaofungua biashara, huku akisema nchi nyingi zilizoendelea uchumi wake unategemea kwa kiasi kikubwa biashara ndogo.
Amesema licha ya umuhimu wake ni lazima kuwa na sera nzuri ili kuhakikisha biashara hili zinapoanza zisife kwani asilimia 95 ya biashara hizo hufa ndani ya miaka mitano.
“Ni muhimu sana kuangalia mazingira ya wafanyabiashara hawa madogo kule kwenye halmashauri, lazima kuwe na mazingira ya kuziwezesha kifedha,” amesema.
Amesema ili kufanikisha hilo ni vyema serikali ikaangalia namna ya kutengeneza sera za kuwezesha wafanyabiashara.
Amesema ili kufanikisha hilo ni vyema kuwapo na taasisi za kufadhili mawazo hayo kulingana na sekta yaliyopo kama ni biashara au kilimo.