Madini ya Sh13 bil yakamatwa ndani ya miezi 10 nchini

MKurugenzi wa Fedha na Utawala wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Bruno Mteta, akiwaonyesha waandishi wa habari, madini aina ya Amber yalikamatwa kutoka kwa kigeni Agosti 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA)wa Dar es Salaam, yakiwa njiani kutoroshwa nje ya nchi. Kulia ni Mkurugenzi wa uthamini wa madini, huduma na maabara, Dominic Rwekeza. Picha na Juliana Malondo
Muktasari:
NI kuanzia Septemba mwaka jana hadi Julai mwaka huu kwenye Viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza yakitoroshwa kwenda nchi za nje
Dar es Salaam. Katika kipindi cha miezi 10 Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) imewakamata watoroshaji 23 wa madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya Sh13.17 bilioni katika viwanja vya ndege vilivyopo Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, huku 20 kati yao wakiwa raia wa kigeni.
TMAA imesema matukio hayo ni tofauti na yale mawili yaliyotokea Agosti 20 mwaka huu ambapo raia wawili wa kigeni walikamatwa maeneo tofauti, ambapo mmoja akikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiwa na madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya Sh25 milioni.
Mwingine alikamatwa nyumbani kwake maeneo ya Jangwani Beach, Dar es Salaam akiwa na aina mbalimbali ya madini na vito aina ya Amber, ambavyo bado vinafanyiwa tathimini ili kubaini thamani yake, kwamba watu hao watafikishwa mahakamani wiki ijayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TMAA, Bruno Mteta alisema madini hayo yalikamatwa kuanzia Septemba mwaka jana hadi Julai mwaka huu, kwenye viwanja vya ndege vya JNIA, Kilimanjaro (KIA) Arusha na Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
“Katika matukio yote, tumekamata watu 25 ila 20 kati yao walikuwa raia wa kigeni na wengine waliobaki walikuwa Watanzania, mpaka sasa kesi tatu zimeshakamilika na wahusika wamechukuliwa hatua’’ alisema. Alisema madini ambayo hutoroshwa zaidi kwenda nje ya nchi ni Tanzanite, Green garnet, Red garnet, Moonstone, Greentomaline, Safaya na Rubi.
Alisema ili kukomesha utoroshaji huo, TMAA imeweka maofisa wake katika viwanja vikubwa vya ndege nchini ambao hukagua abiria kwa kushirikiana na maofisa usalama wa viwanja vya ndege na polisi na kusisitiza kuwa changamoto inayowakabili ni kutokuwa na mtambo wa kuweza kubaini waliobeba madini, na kusisitiza kuwa pamoja na kuwa na mipango hiyo, kumekuwa na njia za panya nyingi za kupitisha madini mbalimbali kwenda nje ya nchi, huku akitolea mfano mkoani Kilimanjaro na Arusha kwamba kuna njia za panya 430.
“Watu wamekuwa wakipitisha madini kwa kiasi kikubwa kwenda nje ya nchi kwa kutumia njia hizi, hata wakifika katika nchi hizo kuwabaini ni ngumu kwani huwezi kuwa na uhakika kama madini hayo yametokea nchini ama laa” alisisitiza.
Alisema katika migodi mikubwa 10 iliyopo nchini, TMAA imeweka maofisa wake ambao wanakagua uzalishaji wa kila siku wa kampuni hizo na kutuma ripoti makao makuu ya wakala huyo.
Ulipaji kodi kampuni za madini
Alisema kuanzia mwaka 2009 hadi Machi mwaka huu Kampuni kubwa zinazomiliki migodi mikubwa ya dhahabu nchini zimelipa Sh474 ya kodi ya mapato.
“Kampuni ya Geita Gold Mining inayomiliki Mgodi wa Dhahabu wa Geita imelipa Sh299.4bilioni, Kampuni ya Resolute Tanzania inayomiliki Mgodi wa Dhahabu wa Golden Pride umelipa Sh97bilioni na Kampuni ya Pangea Minerals inayomiliki Mgodi wa Dhahabu wa Tulawaka imelipa Sh77.4bilioni” alisema
Alisema migodi hiyo imelipa ushuru wa mafuta kiasi cha dola2milioni(Sh3bilioni), kwamba zilikuwa hazijalipwa mpaka mwaka 2010.
“Migodi hiyo imelipa Sh4.8bilioni za kodi ya zuio kutokana na kushindwa kujumuisha kodi hiyo katika malipo yaliyofanywa kwa watoa huduma mbalimbali kwa migodi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2009 hadi 2012.
Pia wamelipa Sh2.41bilioni za ushuru wa serikali za mitaa, na malipo hayo yalikuwa hayajafanywa kwa kipindi cha mwaka 2004 hadi 2011” alisema.