Nishati ya petrol yaadimika kimyakimya

Gari Likijaza Mafuta
Muktasari:
MIKOA mbalimbali ya Tanzania Bara, inakabiliwa na uhaba wa nishati ya mafuta ya petroli ukiwemo mkoa wa Dar es Salaam na kuzua wasiwasi kuwa huenda bidhaa hiyo ikaadimika kabisa.
Waandishi Wetu
MIKOA mbalimbali ya Tanzania Bara, inakabiliwa na uhaba wa nishati ya mafuta ya petroli ukiwemo mkoa wa Dar es Salaam na kuzua wasiwasi kuwa huenda bidhaa hiyo ikaadimika kabisa.
Kwa muda wa wiki moja vituo kadhaa vilivyoko katika eneo la Sinza na Mwenge vimesimama kutoa huduma hiyo na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na wamiliki wake kutokana na hatua hiyo.
Baadhi ya madereva waliotembelea vituo hivyo kwa ajili ya kupata nishati hiyo walijikuta wakilazimika kuondosha magari yao na kwenda maeneo mengine ya mbali baada ya kukosekana wahuduma wala wahusika wake .
“ Nimefika hapa kujaza mafuta gari langu, lakini simwoni mhudumu yoyote, hata wamiliki wake hawapo, sijui kinachoendelea hadi dakika hii” alisema dereva mmoja baada ya kudai kukosa huduma hiyo katika kituo cha Bamaga.
Hali kama hiyo imejitokeza pia katika vituo kadhaa vilivyopo eneo la Mwenge ambavyo vimesimama kutoa huduma hiyo kwa kipindi cha siku nne. Taarifa za awali zilizopatikana toka kwa mashuhuda wa karibu na vituo hivyo zilisema kuwa vituo hivyo vimeishiwa mafuta.
Uhaba wa nishati hiyo imearifiwa pia kuyakumba maeneo kadhaa ya nchi ikiwemo mji wa Njombe ambao umelazimika kusimamisha kwa muda kufanya kazi magari ya serikali. Ripoti zinasema kuwa kwa sasa ni gari moja tu la Mkurugenzi wa Halmshauri ya Mji wa Njombe George Mkindo ndilo linalofanya kazi na kwamba hali hiyo imeathiri utendaji kazi wa watumishi wake.
Hivi karibuni gazeti hili lilimkariri Ofisa Uhusiano wa Halimashauri ya Wilaya ya Njombe Lukelo Mshauri akisema kuwa tatizo hilo limedumu kwa muda hata kusababisha usumbufu wa kufuata mafuta Makambako kwa ajili ya kufanikisha ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ( Mahusiano na Uratibu) aliyeifanya wiki iliyopita wilayani humo.
Meneja wa Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo alitaja chanzo cha kukosekana mafuta katika maeneo ya Njombe na Songea kuwa ni kutokana na kuchelewa kufika kwa meli za mafuta jijini Dar es salaam.
Alisema tatizo hilo linatokana na boti ya kuongozea meli za mafuta kuharibika kwa muda wa siku nne na kusababisha meli hizo kushindwa kutia nanga
MKOA wa Kilimanjaro umekumbwa na uhaba mkubwa wa mafuta ya taa, diesel na petrol na sasa baadhi ya miji imekuwa ikipokea mafuta ya taa yanayoingizwa kimagendo kutoka Kenya.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa jana na juzi, umebaini kuwa mafuta ya taa yamekuwa yakiingizwa mkoani humo kutoka Kenya kwa pikipiki na baiskeli kupitia njia za panya.
Mafuta hayo ya taa yanayoingizwa usiku wa manane,yanauzwa kwa dumu moja la lita 20 kwa bei ya jumla ya Sh40,000 huku bei ya rejareja ikiwa ni kati ya Sh2,000 na Sh2,800 kwa lita.
Mfanyabiashara wa Pasua mjini Moshi, Esther Mgonja alisema analazimika kununua mafuta ya taa kutoka Kenya kwa kuwa yanauzwa kwa bei ya chini ukilinganisha na yale ya Tanzania.
“Mimi wakiniletea dumu moja la lita 20 la mafuta ya taa kutoka Kenya nanunua kwa sh37,000 wakati kwenye shell nitauziwa kwa Sh44,000 kwanini nisinunue hayo ya Kenya?”alihoji.
Mfanyabiashara huyo anayemiliki duka la rejareja alisema vituo vya mafuta vya mkoani humo havina mafuta ya taa hivyo mafuta hayo yakizuiwa kuingia nchini hali itakuwa mbaya sana.
Baadhi ya pikipiki zinazobeba mafuta hayo ya taa zina nambari za usajili za nchini Kenya na huingia hadi katikati ya mji wa Moshi usiku wa manane bila kukamatwa na vyombo vya dola.
Wilaya za Rombo, Moshi Vijijini na Mwanga zinakadiriwa kuwa na njia za panya zaidi ya 300 ambazo ndizo zinazotumika kuingiza bidhaa hiyo katika miji mikubwa ya mkoa Kilimanjaro.
Mafuta hayo sasa yanauzwa waziwazi katikati ya mji wa Moshi na mitaa ya pembezoni huku kwa sehemu kubwa biashara hiyo ya mafuta ya taa ikifanywa na wafanyabiashara Wanawake.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara hukodi Taxi hadi Njiapanda ya Himo na kufaulisha mafuta hayo kutoka kwenye pikipiki ili kuwapiga chenga polisi.
“Shell (vituo vya mafuta) havina kabisa mafuta ya taa kwa muda mrefu sasa na mafuta ya taa yote unayoyaona tunatumia yanatoka Kenya”alidai mkazi mmoja wa Soweto mjini Moshi.
Meneja wa kituo kimoja kinachomilikiwa na kampuni ya Puma (BP zamani) aliliambia gazeti hili kuwa kampuni hiyo iliachana na biashara ya kuuza mafuta ya taa miaka saba iliyopita.
“Kwanza haina faida kwa sababu mafuta yanayouzwa kwa madumu kutoka Kenya yanauzwa kwa bei ya chini kwa hiyo unakuta sisi kwenye vituo yanatudodea”alisema Meneja huyo.
Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz alipoulizwa jana alisema hana taarifa juu ya kuibuka kwa biashara hiyo huku akiitupia lawama Mamlaka ya Mapato (TRA).
“Mimi ndio kwanza nasikia hizo taarifa lakini kama yanaingia kimagendo hilo ni jukumu la TRA…nitawasiliana nao kujua kama hayo mafuta yanaingia kihalali ama la”alisema Boaz.
Hata hivyo Meneja wa TRA mkoa Kilimanjaro, Patience Minga alipotafutwa jana simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila majibu na hata alipoipokea alisema yupo kwenye kikao.
Katika hatua nyingine, Mji wa Moshi na vitongoji vyake umekumbwa na uhaba mkubwa wa mafuta ya Petrol na dizeli huku vituo vichache tu ndivyo vikionekana kuuza bidhaa hiyo.
Uhaba huo wa mafuta ulianza kujitokeza juzi mchana ambapo vituo mbalimbali vilidai kukosa bidhaa hiyo huku vile vilivyopo pembezoni ya mji pekee ndivyo vilivyokuwa na mafuta.
Kumekuwepo na hisia kuwa huenda baadhi ya wamiliki wa vituo hivyo wamekula njama kuficha bidhaa hiyo kutokana na kuwapo kwa tetesi kuwa huenda bei ya mafuta ikapanda.
Meneja wa kituo kimoja mjini Moshi aliyeomba jina lake lihifadhiwe, aliyedai amewasiliana na makao makuu Jijini Dar na wamemweleza mafuta yataadimika kwa wiki mbili.
Kwa upande wake Meneja wa kampuni ya Panone inayomiliki vituo mbalimbali nchini, Gido Marandu alikiri kuadimika kwa mafuta ya taa,petrol na dizeli akiitupia lawama Ewura.
“Tatizo ni Depoti huko Dar hawataki kuuza mafuta baada ya Ewura kuyumbisha bei mimi nimetuma magari huko yana siku ya tatu leo (jana) hatujapata mafuta”alisema Marandu.
Marandu alitahadharisha kuwa baada ya shehena ya mafuta inayouzwa sasa katika vituo mbalimbali mkoani Kilimanjaro kumalizika hakutakuwa tena na biadhaa hiyo sokoni.
Wakati huo huo, wananchi wa Manispaa ya Songea wamejikuta wakishindwa kwenda katika shuguli zao za maendeleo kutokana na kukosena kwa mafuta ya petrol, hali ambayo imewasababishia adha ya kukosa usafiri na wengine kulazimika kutembea umbali mrefu kutokana na kukosa usafiri.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Mfanyabiashara wa Mafuta Kisumapai amesema, bado hali ya upatikanaji wa mafuta ni mbaya na amelazimika kusafiri kwenda Dar es salaam kwa ajili ya kufuatilia mafuta .
Amesema, tatizo kubwa ni wauzaji wakubwa wa mafuta hawataki kuwauzia mafuta hali ambayo imesababisha wafanyabiashara wa mikoani kushindwa kupata mafuta hivyo kusababisha adha kwa watumiaji .
“Nipo Dar es salaam nahangaika kutafuta mafuta kwa wauzaji wakubwa ili niweze kutuma japo gari moja ,na huenda nikafanikiwa, ,najua hali ni mbaya na ndiyo maana nimeamua kuja mwenyewe ili kufuatilia”alisema Kisumapai
Naye Suleiman Said mkazi wa Songea amesema hadi sasa hali ni mbaya hakuna mafuta mjini, petroli wanauziwa Sh2200 -2500 kwa watu binafsi ,wanahangaika kutafuta kwa watu binafsi ili waweze kuendelea na shuguli za maendeleo lakini nayo yanauzwa kwa bei ya juu na kwa kificho .
Amesema, anaiomba serikali isaidie kutatua tatizo hilo kwani hali ni mbaya na watu wengi wamejikuta wakichelewa na wakishindwa kwenda kazini kutokana na kukosa usafiri na wengine kushindwa kwenda safari zao kutokana na magari kukosa mafuta.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amekiri kuwepo kwa tatizo la kuadimika mafuta katika mkoa wa Ruvuma, ambapo ameongeza kuwa hali ni mbaya zaidi kwa Manispaa ya Songea pamoja na wilaya ya Tunduru.
Imeandikwa na Daniel Mjema, Moshi, George Njogopa Dar na Joyce Joliga, Songea.