Umeme ni shida, Uchunguzi wabaini mikoa mingi iko kwenye hali tete
Mwanafunzi akijisomea kwa kutumia mwanga wa mshumaa kutokana na tatizo la mgawo wa umeme. Picha na Maktaba
Muktasari:
Wakati jiji hilo likiwa gizani kwa nyakati tofauti, baadhi ya mikoa, hususan iliyoko pembezoni, imekuwa ikipata nishati hiyo kwa uhakika kutokana na kuunganishwa na umeme wa nchi jirani.
Mikoani na Dar. Wakati Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Tanesco wakikanusha kuwepo kwa mgawo wa umeme, imebainika kuwa sehemu kubwa ya nchi imekosa umeme kwa siku kadhaa, likiwemo Jiji la Dar es salaam.
Wakati jiji hilo likiwa gizani kwa nyakati tofauti, baadhi ya mikoa, hususan iliyoko pembezoni, imekuwa ikipata nishati hiyo kwa uhakika kutokana na kuunganishwa na umeme wa nchi jirani.
Mikoa ya Mtwara, Iringa, Rukwa, Katavi, Kigoma na Kagera imebainika kutokuwa na katizo la umeme kama ile iliyoungashwa katika gridi ya Taifa kutokana na kutumia umeme wa jenereta nyakati za mchana na usiku hutumia umeme wa kawaida.
Mkoa wa Kigoma hutegemea zaidi jenereta wakati sehemu ndogo ya umeme wa mikoa ya Rukwa na Katavi huzalishwa kwa jenereta na sehemu kubwa hutoka Zambia.
Juzi gazeti hili lilimkariri Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele akisema kuwa hakuna mgawo wa umeme unaoendelea nchini.
Masele alisema tatizo hilo linasababishwa na marekebisho na uboreshaji wa mitambo ya Tanesco na mifumo ya kusambaza umeme na adha hiyo alidai kuwa itaisha hivi karibuni.
Akisisitiza hayo, Meneja Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanesco, Adrian Severin alisema hakuna mgawo wa umeme nchini ila kuna matengenezo ya nguzo yanayoendelea katika maeneo mbalimbali.
Alisema kama kungekuwa na mgawo wasingesita kuutaarifu umma.
Hata hivyo, imebainika kuwa Mkoa wa Arusha, ambao unatembelewa na wageni wengi wanaotoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya utalii, umekuwa na tatizo kubwa la kukatika kwa umeme kila mara na juzi ulikatika kutoka alfajiri na kurejea usiku wa manane.
Mkoa wa Kagera, ambao hutumia umeme wa jenereta na ule wa kutoka nchi jirani ya Uganda, nao unaonja adha hiyo hususan kwa wakazi wa Wilaya ya Muleba ambako inadaiwa kuna matengenezo yanaendelea.
Wakati mikoa mingine ikilalama, mikoa ya Rukwa na Katavi imebainika kutokumbwa na tatizo hilo kwa kuwa wanapata umeme wa uhakika unaozalishwa na jenereta linalotumia mafuta. Umeme unaozalishwa ni megawati 2.5 ambao hutumika kwa matumizi ya kawaida na ya viwandani.
Hata hivyo, uchunguzi umebaini wanaonufaika na umeme huo ni wakazi wa wilaya za Sumbawanga Mjini na Nkasi, wakati wilaya za Kalambo na Sumbawanga Vijijini bado zina tatizo kubwa.
Kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Manispaa ya Dodoma kumeelezwa kuwa kunasababishwa na umeme wa gridi ya taifa kushindwa kufanya kazi. Msemaji wa Tanesco mkoani humo, Innocent Lupenza alisema suala hilo liko juu ya uwezo wao.
Mkoani Morogoro Msemaji wa Tanesco, Esther Msaki amesema tatizo hilo linasababishwa na kuanguka kwa nguzo sita katika maeneo ya Chamwino na kukatika kwa nyaya kunakosabishwa na upepo mkali.
Alisema umeme uliokatika kwa siku mbili mfululizo uliathiri wananchi wa maeneo ya Chuo Kikuu cha Sokoine na Kilimo, Chamwino, Magadu, Chuo Kikuu cha Mzumbe na Kihonda.
Kwa siku saba sasa wakazi wa Mkoa wa Tanga wako gizani huku kaimu ofisa uhusiano wa Tanesco mkoa, Johnson Mwikune akidai kuwa tatizo hilo limesababishwa na hitilafu katika gridi ya Taifa na kudai kuwa jitihada za kuurejesha umeme zinaendelea.
Uchunguzi pia umebaini kuwa tatizo hilo kwa Mkoa wa Geita ni kubwa kwa kuwa kwa takriban wiki tatu sasa umekuwa ukikatwa bila mpangilio na hudumu kwa muda mrefu bila kurudishwa.
Kaimu meneja wa Tanesco wa Mkoa wa Geita, Charles Budodi alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.
Imebainika pia ubovu wa mfumo wa njia za umeme mkoani Singida ni moja ya sababu kubwa inayochangia kukatika mara kwa mara kwa umeme mkoani humo kwa muda wa wiki mbili sasa.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Tanesco Singida, kilidai kuwa ubovu huo unaelemewa na mzigo wa mahitaji makubwa ya matumizi ya umeme, ikilinganishwa na mfumo uliopo sasa.
Nako mkoani Tabora imebainika kuwa chanzo ni matengenezo makubwa ya njia ya umeme yaliyokuwa yakifanyika mkoani Shinyanga na kuathiri eneo lote la Kanda ya Ziwa linalopata umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa.
Kaimu meneja wa Tanesco wa Tabora, Mhandisi Mahenda Nyalika alidai kuwa ofisi yake ilitoa taarifa kwa umma kupitia magari ya matangazo. Alisema juzi na jana adha hiyo ilisababishwa mashine moja ya Kidatu iliyozimika ghafla.Akizungumzia kukosekana umeme siku ya Jumatano, Nyalika alisema kulitokana na dharura ya kuzimika kwa mashine ghafla Kidatu.