Kiwanda chapunguza uzalishaji mafuta kwa kukosekana alizeti

Singida. Kiwanda cha mafuta ya kula cha Singida Fresh Oil Mill kimepunguza uzalishaji kutokana na uhaba wa alizeti katika mkoa huo na mikoa mingine nchini.

Hayo yamebainishwa leo Machi 4, 2023 mjini Singida na uongozi wa kiwanda hicho wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kwenye kiwanda hicho kujionea uzalishaji.

Msimamizi wa kiwanda hicho, Jamal Juma amesema kilikuwa kikizalisha tani 90 za alizeti kwa siku ambazo zinaweza kuzalisha lita 23,300. Amebainisha kwamba kwa mwaka walikuwa wakitumia tani 32,400 za alizeti lakini sasa wanapata tani 7,920 za alizeti kwa mwaka zinazozalisha lita milioni 2.37.

"Kiwanda chetu kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa malighafi ya alizeti. Tumekuwa tukinunua alizeti katika mikoa ya Singida, Manyara, Dodoma na kwingineko," amesema Juma.

Akieleza changamoto wanazopitia, Juma amesema wanakutana na vizuizi vingi wakati wakisafirisha mazao na bidhaa zao, wanatozwa ushuru kwenye kila halmashauri wanayopita.

Amesema utaratibu huo umekuwa ukiwafanya watumie fedha nyingi kulipa ushuru hasa wanaposafirisha mazao kutoka mbali. Ameomba walipe ushuru mara moja kwenye halmashauri wanayotoka.

"Changamoto kubwa ni vizuizi vingi vya mazao wakati wa kusafirisha bidhaa. Tunaomba utusaidia kuondoa vizuizi hivi hasa kile cha Longido. Tunaishauri serikali kuwe na kizuizi kimoja hasa katika halmashauri yetu ili kuiongezea mapato," amesema.

Akizungumzia suala hilo, Chongolo amesema wakati umefika kwa halmashauri kubuni vyanzo vyake vya mapato badala ya kuvizia wanaosafirisha mazao yao.

"Hatuwezi kuwa tunavizia kila kinachopita kwenye halmashauri zetu. Halmashauri zinatakiwa kuwa sehemu ya uwekezaji kwa kutengeneza mazingira mazuri badala ya kuvizia wanaosafirisha bidhaa," amesema.

Amesisitiza kwamba sheria ndogo zinazotungwa na halmashauri husika, zifanye kazi kwa mazao yanayozalishwa katika eneo husika.