Maabara zinazotembea jinsi zilivyodhibiti uchakachuaji mafuta
Mkurugenzi wa Kampuni ya SICPA, Alfred Mapunda
Muktasari:
- Kauli hiyo ilimetolea na Mkurugenzi wa Kampuni ya SICPA Tanzania, Alfred Mapunda wakati wa sherehe ya kilele cha miaka 50 ya Shirika la viwango Tanzania (TBS) zilizofanyika katika Mtaa wa Njedengwa mahali yalipo makao ya Shirika.
Dodoma. Uchakachuaji wa mafuta nchini umetajwa kupungua kwa kiwango kikubwa kufuatia kuanzishwa kwa mifumo ya kisasa ya udhibiti ikiwemo matumizi ya maabara zinazotembea, ingawa wakwepa kodi na wahalifu wa kiuchumi wameendelea kubuni mbinu mpya za kukwepa sheria.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Kampuni ya SICPA Tanzania, Alfred Mapunda, wakati wa maadhimisho ya kilele cha miaka 50 ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) yaliyofanyika katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma ambako ndipo yalipo makao makuu ya shirika hilo.
SICPA ni kampuni inayojihusisha na teknolojia za ufuatiliaji na uthibitishaji wa ubora wa bidhaa, ikiwemo kemikali maalumu zinazowekwa kwenye mafuta ili kusaidia kubaini ubora wake na kuhakikisha yanakidhi viwango vinavyotakiwa kabla ya kuingia sokoni.
Katika maadhimisho hayo, kampuni hiyo ilitajwa kuwa miongoni mwa taasisi zilizofanya vizuri katika kuunga mkono juhudi za kudhibiti bidhaa zisizokidhi viwango.
Mapunda amesema miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto kubwa katika kudhibiti uchakachuaji wa mafuta na vitendo vya ukwepaji kodi, huku baadhi ya wafanyabiashara wakijihusisha na udanganyifu wa mafuta au kuyachepusha kwenda nje ya nchi kinyume cha taratibu.
Amesema maendeleo ya teknolojia yameimarisha uwezo wa Serikali na wadau wengine kufuatilia ubora na usafirishaji wa mafuta, jambo ambalo limechangia kupunguza vitendo hivyo.
“Hata hivyo, wahalifu wa kiuchumi nao wanaendelea kubuni mbinu mpya na kutumia teknolojia kukwepa mifumo ya udhibiti, hivyo mapambano dhidi ya uchakachuaji wa mafuta na ukwepaji kodi yanahitaji kuendelea kuimarishwa kila wakati,” amesema Mapunda.
“Tumedhibiti uchakachuaji kwa kiasi kikubwa,najua huenda tatizo hatujamaliza lakini Watanzania waamini kuwa wako salama wao na vyombo vyao na haya tumeyafanya kwa kushirikiana na Serikali, wananchi na watu wenye nia na mapenzi mema na nchi yao,” amesema Mapunda.
Anasema vita ya kwenye biashara ya mafuta ni kubwa na ina mbinu nyingi lakini kwa ushirikiano mkubwa wa TBS na wadau wengine wamekuwa wakiwakamata na kuwadhibiti watu wanaotamani kujihusisha na biashara hiyo kwa kupata utajili wa haraka.
Amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kutumia bidhaa halali lakini wakumbuke kulipa kodi kwa ajili ya kujenga nchi yao kwani mapato yatokanayo na kodi hayawezi kupatikana ikiwa wapo wanaokwepa na wakati mwingine wanakuwa na bidhaa feki.
Awali, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga alisema ili Taifa liweze kuendelea ni lazima nguvu itumike kudhibiti bidhaa feki kwani hizo ndizo zinapelekea kupotea kwa mapato ya Serikali.
Waziri Kapinga anasema ameagiza wafanyabiashara kuendelea kushirikiana kwa karibu na na TBS na wajenge udugu usiokuwa na mashaka kwani itasaidia kwenye ushauri na hata kwenye changamoto wanaweza kuzibainisha.
Kwa upande wa TBS, Waziri aliwaagiza kuhama kwenye utendaji kazi wa mazoezi badala yake watambue kuwa wanatakiwa kukimbizana na dunia ilivyo ikiwemo kutoa stika za kielekroniki lakini wazingatie kuwa hawatakiwi kuongeza gharama kwa watumiaji.
“Kingine sitamani kuona tunakuwa na mgambo wa biashara badala yake tuhakikishe biashara za watu zinakuwa na kuongezeka huku zikiwa na ubora unaotakiwa kwani tunajua kuwa Dira ya Taifa inataka asilimia 70 izalishwe kutokana na sekta binafsi,” amesema Kapinga.
Mkurugenzi wa TBS, Dk Ashura Katunzi alisisitiza usimamizi wa ubora wa bidhaa na mpango wa kuhama katika mageuzi ya kiteknolojia kuwa unakwenda kuongeza mahusiano baina ya wafanyabiashara wenye viwanda na Shrika hilo.
Dk Katunzi pia alimkabidhi Waziri kuzindua kitabu ambacho kinaonyesha mafanikio ya waliko toka, walipo na wanaokoelekea ambacho ndani yake pia kimejaa maelekezo na ushauri wa nini kifanyike kwa mtu anayetaka stika za biashara.