Makali bei ya vyakula kupungua Machi
Dododma. Serikali imesema bei ya vyakula nchini zitashuka kuanzia Machi mwaka huu ili kuwapunguzia wananchi gharama za maisha.
Kauli hiyo ya serikali imekuja wakati kukiwa na malalamiko kuhusu upandaji wa bei za vyakula nchini, ambapo bei ya kilo moja ya unga imefikia kati ya Sh2000 hadi Sh2500 huku bei ya kilo moja ya maharage imefikia Sh4000 hadi Sh4500.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari leo Januari 10, 2022 mkoani Dodoma.
“Nikiri kwamba ni kweli tuna changamoto ha bei za vyakula lakini ni kipindi cha mpito na baadaye bei zitashuka, na siyo kwamba wizara ya kilimo hatuelewi upandaji bei za vyakula,”
“Kama waziri naweza kusema kwamba bei ya chakula itashuka kuanzia Machi hadi April kwani vyakula vitakuwa vingi,” amesema Bashe akitaja gharama za usafirishaji kama moja ya sababu za kupaa bei za vyakula.