Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ripoti: Watanzania milioni 1.7 wana uhaba wa chakula

Muktasari:

  • Wakati Wizara ya Kilimo ikijipanga kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo nchini ili ifikie asilimia 10 ifikapo 2030, ripoti ya utafiti ya Taasisi Jumuishi ya Usalama wa Chakula (IPC), imeonyesha watu milioni 1.7 Tanzania wanakumbwa na uhaba wa chakula.

Dar es Salaam. Wakati Wizara ya Kilimo ikijipanga kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo nchini ili ifikie asilimia 10 ifikapo 2030, ripoti ya utafiti ya Taasisi Jumuishi ya Usalama wa Chakula (IPC), imeonyesha watu milioni 1.7 Tanzania wanakumbwa na uhaba wa chakula.

Ripoti hiyo yenye jina la ‘Tanzania: Hali ya Uhaba wa Chakula Oktoba 2022 - Februari 2023 na Machi - Mei 2023’ ilihusisha sampuli ya watu milioni 1.8 kutoka Zanzibar na milioni 8.7 kutoka Tanzania bara.

Katika sampuli hiyo, watu wanaokumbwa na ukosefu wa chakula nchini, 740,812 wanatokea Zanzibar, huku wengine 964,000 wakitokea Tanzania bara.

Utafiti huo umeonyesha sababu mojawapo inayochangia uhaba wa chakula kwa Watanzania, ni mfumuko wa bei unaosababisha kupandisha bei za vyakula.

“Kwa upande wa Zanzibar hali ya kukosekana chakula inasababishwa na bei za bidhaa kuwa juu, ukame kwa baadhi ya maeneo, magonjwa ya mazao, wadudu na utunzaji mbovu wa chakula,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.

“Sababu za ukosefu wa chakula Tanzania Bara ni ukame wa muda mrefu, magonjwa ya mazao na wadudu na bei kubwa za bidhaa za chakula,” imeongeza kusema ripoti hiyo.

Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania bara, inaonyesha kati ya halmashauri za wilaya 28 zilizofanyiwa utafiti, tano ambazo ni Hai, Longido, Monduli, Mwanga na Same DC, zimeonekana kuwa na hali mbaya zaidi na tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua za dharura kunusuru wananchi.

“Kwa halmashauri za wilaya za Longido na Monduli, ukosefu wa chakula umesababishwa na ukame wa muda mrefu na mvua zisizokuwa na uhakika kwa misimu yote miwili ya vuli na masika kwa mwaka wa uzalishaji wa 2021/2022,” imesema ripoti hiyo.

Hata hivyo, akihutubia wananchi wilayani Kondoa mkoani Dodoma Novemba 22, 2022 kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa na tayari Serikali imeshasambaza chakula cha bei rahisi.

“Hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa, Serikali ina chakula cha kutosha, hivi sasa kupitia wizara, halmashauri zinaonyesha na kutuletea taarifa pale ambapo bei ya mahindi inakuwa imepanda sana.”

Ripoti ya IPC imeshauri mbinu mbalimbali za kumaliza tatizo hilo la uhaba wa chakula kwa wananchi, ikiwamo kushirikisha wahisani ili kutoa msaada wa chakula na wa kujikimu kimaisha kwa kaya zilizo hatarini.

Lakini pia imeshauri kutekeleza mbinu za kilimo cha kufuata hali ya hewa, kutoa pembejeo za kilimo na mbegu zinazokomaa mapema na zinazostahimili ukame.