Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbegu bora za mpunga zabadilisha uchumi wa wakulima Mbarali

Baadhi ya wataalamu wa kilimo wakitembelea mashamba ya mpunga yaliyolimwa kwa kilimo shadidi.

Muktasari:

  • Mbegu za zamani zilizalisha wastani wa gunia 15 za mpunga kwa ekari, lakini mbegu mpya zilizosambazwa nchini na Wizara ya Kilimo zinafikia wastani wa gunia 30 bila kuathiri ubora wa mchele.



Dar es Salaam. Mabadiliko ya matumizi ya mbegu bora za mpunga zinazokomaa mapema na kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi yamechangia ukuaji wa mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kutoka wastani wa Sh1 bilioni hadi takribani Sh12 bilioni kwa mwaka.

Mbali na kuongeza makusanyo ya halmashauri, teknolojia hiyo imeboresha maisha ya maelfu ya wakulima waliokuwa wakitumia mbegu za asili, kwa kuongeza uzalishaji, kipato na uwekezaji katika shughuli nyingine za kiuchumi.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Mbarali, Yobu Mlomo amesema mafanikio hayo yamechangiwa na usambazaji wa mbegu bora kupitia maofisa ugani na wazalishaji wa mbegu waliopo katika kata mbalimbali.

Kauli yake imekuja baada ya Mwananchi kufanya mahojiano na Valentine Moi (25), maarufu Vale Nafaka, mfanyabiashara wa mazao, mkulima na mhamasishaji wa vijana aliyeeleza mafanikio aliyoyapata kwa kutumia mbegu bora. Pia vijana wengi, akiwemo mchekeshaji Emanuel Mgaya (Masanja Mkandamizaji), wamewekeza katika kilimo hicho.

Mlomo amesema wilaya hiyo ina wazalishaji wa mbegu za msingi wapatao 70 wanaouza kwa wakulima kwa wastani wa Sh1,500 kwa kilo, chini ya bei ya soko ya Sh2,500 hadi Sh3,000.

Amesema mbegu hizo zimebuniwa kuhimili mabadiliko ya tabianchi na zinaendana na teknolojia ya umwagiliaji unaotumia maji kwa ufanisi zaidi kwa kuingiza na kuyaondoa kwa awamu shambani, hatua inayopunguza matumizi ya maji huku ikiongeza idadi ya wanufaika.

Amesema mbegu za zamani zilikuwa zikizalisha wastani wa magunia 15 kwa ekari, wakati mbegu bora huzalisha wastani wa magunia 30 bila kupunguza ubora wa mchele.

Ongezeko hilo limewawezesha wakulima kuongeza mitaji, kujenga nyumba bora, kununua magari na kuanzisha biashara nyingine. Amesema mafanikio hayo yamechangiwa pia na mbinu mpya za maofisa ugani zinazotumia vikundi vya wakulima, mashamba darasa na mashamba ya maonyesho badala ya kutembelea shamba moja moja.

Kupitia mfumo huo huzalishwa wakulima viongozi wanaopewa mafunzo na baadaye kuwafundisha wenzao, huku maofisa ugani wakiendelea kutembelea skimu za umwagiliaji kwa ratiba maalumu kutoa ushauri wa kitaalamu.

Mlomo amesema kampeni za matumizi ya mbegu bora zilianza kwa nguvu mwaka 2010 lakini zilipata upinzani kutokana na hofu ya kukosekana soko. Hata hivyo, baada ya wakulima kuona matokeo, zaidi ya asilimia 90 sasa wanatumia mbegu bora.

Amesema changamoto iliyobaki ni baadhi ya wakulima kutumia mbegu zisizoidhinishwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji. Mbarali ina zaidi ya skimu 140 za umwagiliaji, lakini mahitaji ya uwekezaji bado ni makubwa licha ya Serikali kuendelea kutenga fedha.

Mkazi wa Rujewa, Joshua Mwayupa amesema zamani alikuwa akitumia mbegu za asili zilizokuwa zikikomaa kwa muda mrefu, kushambuliwa na magonjwa na kutoa mavuno duni. Baada ya kutumia mbegu bora zinazokomaa ndani ya siku 90 hadi 120, mavuno yake yameongezeka kutoka wastani wa magunia 28 hadi 40-45 kwa ekari.

Amesema sasa analima ekari tano badala ya 10 na kupata karibu mavuno yaleyale, huku akieleza kuwa maofisa ugani wamekuwa msaada mkubwa kwa kuwapa elimu ya maandalizi ya shamba, matumizi ya mbolea, usimamizi wa maji, udhibiti wa magugu na wadudu hadi uvunaji.

Kwa upande wake, mkulima wa Kijiji cha Lujewa, Hawa Mayele amesema kabla ya kupata mafunzo alikuwa akitumia mbegu za kawaida zilizokuwa zikitoa mavuno yasiyotabirika. Baada ya kutumia mbegu bora na kufuata ushauri wa maofisa ugani, mavuno na kipato vimeongezeka, jambo lililomwezesha kusomesha watoto na kuwekeza katika shughuli nyingine za maendeleo.

Amesema wanawake wengi wa Lujewa sasa wanashiriki kikamilifu katika vikundi vya wakulima, jambo lililowaongezea uwezo wa kujifunza teknolojia mpya, kubadilishana uzoefu na kushiriki zaidi katika maamuzi ya kiuchumi ya familia.