Mbinu mpya kwa wavuvi nchini kukabili majanga

Muktasari:

  • Serikali imewataka wavuvi nchini kuchangamkia fursa kwa kukata bima ili kuwasaidia pindi wanapopatwa na majanga mbalimbali kwenye shughuli zao.

Mwanza. Serikali imewataka wavuvi nchini kuchangamkia fursa kwa kukata bima ili kuwasaidia pindi wanapopatwa na majanga mbalimbali kwenye shughuli zao.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki wakati akizindua bima maalumu kwa wavuvi uliofanyika jijini Mwanza.
Bima hiyo mpya imezinduliwa kwa ushirikiano wa benki ya NMB na kampuni ya bima ya Britam inahusisha wavuvi wakubwa na wadogo.
Ndaki alisema miaka ya nyuma taasisi nyingi za bima zilikuwa zinawaangalia wavuvi wakubwa pekee na sasa NMB na Britam wamekuja na mkakati mpya wa kuwasaidia wavuvi wadogo na wa kati.
Aliwataka wavuvi kuendelea kupatiwa elimu kuhusu bima ili waifahamu na kufanya maamuzi sahihi kwani, itakuwa kimbilio katika shughuli zao za kila siku.
“NMB imedhamiria kuwainua kiuchumi wakulima, wafugaji na sasa ni zamu ya wavuvi na Serikali inatambua mchango wao katika kuhakikisha makundi hayo yananufaika na mikopo inayotolewa na benki hiyo,” alisema Ndaki.

Alisema sekta ambazo zilikuwa zinaonekana kuwa na hatari kwa sasa zianze kufikiwa na kukatiwa bima kwa kuwa zina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Waziri Ndaki alisema sekta ya uvuvi inaajiri watu milioni 4.5 na kwamba inachangia asilimia 1.7 ya pato la taifa hivyo ni kundi muhimu ambalo linatakiwa kusaidiwa ili liweze kupiga hatua.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema bima hiyo iliyopewa jina la Jahazi inawalenga wavuvi wadogo na wa kati hapa nchini.
Alisema wavuvi watakata bima ya asimilia 3 ya chombo husika cha shughuli ya uvuvi na wataweza kukingwa na majanga ya ajali, kuungua mitumbwi ama boti pamoja na watu watakaokuwa ndani ya vyombo hivyo.
Aliongeza kuwa faida nyingine za bima hiyo ni pamoja na familia ya mvuvi ama mtu aliyekuwa ndani ya chombo hicho kupewa mkono wa pole endapo kutatokea kifo pamoja na kupata ulemavu wa kudumu.
Aidha, bima hiyo itatoa gharama za matibabu kwa mvuvi pamoja na kulipwa fidia kutokana na ajali itakayompata atakapokuwa majini kwa shughuli za uvuvi ama kando kando ya ziwa, mto, bwawa ama bahari.
Naye Meneja wa kampuni ya Bima ya Britam Kanda ya Ziwa, Said Kadabi alisema  bima hiyo itawasaidia wavuvi katika kuinuka kiuchumi kwa kuwa sasa watanya kazi zao kwa kujiamini.
Alisema wanalenga kuyafikia makundi mbalimbali ya kijamii na kuyakatia bima ikiwamo mama lishe ili waweze kufanya shughuli zao kwa kujiamini zaidi.