Mbunge adai SGR itajengwa kwa miaka 81

Mbunge adai SGR itajengwa kwa miaka 81

Muktasari:

  • Mbunge  wa Handeni Mjini  CCM, Reuben Kwagilwa,   ameishauri Wizara ya Fedha na Mipango,  waangalie namna ya kufadhili miradi mikubwa  kwa mfumo wa  dhamana ya miundombinu ‘infrastructure bond’ ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma za wananchi kila siku.

Dar es Salaam. Mbunge  wa Handeni Mjini  CCM, Reuben Kwagilwa,   ameishauri Wizara ya Fedha na Mipango,  waangalie namna ya kufadhili miradi mikubwa  kwa mfumo wa  dhamana ya miundombinu ‘infrastructure bond’ ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma za wananchi kila siku.

Amesema isipofanya hivyo mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa wa SGR utachukua miaka 81 kukamilika kwakuwa mpaka sasa hata kilometa 300 bado hazijakamilika.

Kwagilwa ametoa ushauri huo  Ijumaa Aprili 9, 2021 bungeni wakati akichangia mjadala wa mpango wa tatu wa maendeleo wa kitaifa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021/22 - 2025/26,

“Standard Gauge Railway tunayoijenga ukijumlisha zile njia  tunazotakiwa kujenga ni kilomita 4886 hapo naongelea zile njia tu, siongelei mahala ambapo reli huwa zinapishana. mpaka sasa tumeshajenga kipande kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kilometa 300 na tunaendelea kipande cha Morogoro Makutupora kilometa 422 lakini tuko upande mwingine wa Isaka na Mwanza kilometa kilometa 249,  

Kwa namna tunavyohudumia mradi huo kama tukiendelea kwa mfumo huo tutajenga kwa miaka 81 kwa nchi nzima ikiwa miaka mitano tumejenga kwa kilameta 300 na kilometa zilizosalia tutazijenga kwa miaka  81 hii katika nchi ambayo inapambana kujenga uchumi kasi hiyo haikubaliki na imegharimu Sh11 trilioni ambazo  ni ‘idle investment’ kwa sababu hatutaanza kutumia leo.,”amesema

Ameongeza “Serikali inatakiwa kujifunza na kuondokana na  mfumo wa kizamani  wa kufadhili  miradi mikubwa  kwa sababu  inajipa pressure kubwa halafu inashindwa kupeleka huduma za kila siku kwa wananchi wake” amesema