Mbunge Tarimo ataka walioshindwa kuendeleza viwanda wanyang’anywe

Mbunge Tarimo ataka walioshindwa kuendeleza viwanda wanyang’anywe

Muktasari:

  • Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo ameitaka Serikali ya Tanzania kuwanyang'anya viwanda wawekezaji walioshindwa kuviendeleza.

Dodoma. Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo ameitaka Serikali ya Tanzania kuwanyang'anya viwanda wawekezaji walioshindwa kuviendeleza.

Amebainisha kuwa si jambo jema na halileti afya kuona viwanda vingi vipo mikononi mwao watu lakini havifanyi kazi wakati Watanzania wanahitaji kukuza uchumi na kupanua ajira.

Ametoa kauli hiyo  bungeni mjini Dodoma  leo Alhamisi Aprili 15,2021 wakati akichangia hotuba ya ofisi ya waziri mkuu kwa ajili ya mapendekezo ya maombi ya mapato na matumizi kwa mwaka 2021/22.

"Sipingi ubinafsishaji wa viwanda lakini tukubaliane kuwa waliochukua viwanda na wanashindwa kuviendeleza napendekeza wanyang'anywe mara moja," amesema Tarimo.

Mbunge huyo amependekeza nguvu kubwa ya uwekezaji ielekezwe katika kilimo hasa kwa zao la alizeti kwani viwanda bila kuwekeza kwenye kilimo haitasaidia kwa kuwa ni lazima malighafi ipatikane kwanza.

Tarimo alitolea mfano wa viwanda vya Moshi Mjini ikiwemo kiwanda cha magunia, viberiti.