Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Meli mpya, maboresho ya bandari kuleta mageuzi Ziwa Tanganyika

Muktasari:

  • Baada ya kukamilika kwa mradi huo, uwezo wa Bandari ya Kigoma utaongezeka kutoka kuhudumia tani 800,000 za mizigo kwa mwaka hadi tani milioni mbili.

Dar es Salaam. Usafirishaji wa mizigo kupitia meli nne zinazojengwa katika Ziwa Tanganyika unatajwa kuwa kichocheo cha biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku ukifungua fursa za kiuchumi, ajira na kuongeza mapato ya Serikali.

Ujenzi wa meli hizo unakwenda sambamba na maboresho ya Bandari ya Kigoma, ikiwamo ujenzi wa gati la mizigo na abiria pamoja na kuongeza kina cha maji.

Hayo yameelezwa leo, Jumatatu, Julai 20, 2026, wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya uzinduzi wa meli hizo na uboreshaji wa Bandari ya Kigoma katika hafla iliyofanyika mkoani Kigoma.

Akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amesema kuongezeka kwa meli katika Ziwa Tanganyika kutaifanya Tanzania kuwa njia muhimu ya usafirishaji wa mizigo ya DRC kwenda kwenye masoko ya kimataifa, hususan China.

Mbossa amesema Serikali iliingia makubaliano na kampuni ya Zijin Mining Group Co. Ltd kwa ajili ya kuendeleza usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Kigoma, ikiwa ni mmiliki wa migodi mitatu mikubwa ya madini nchini DRC yenye makadirio ya kuendelea kuzalisha kwa zaidi ya miaka 50.

“Watatengeneza Bandari ya Kigoma na pia watajenga kilomita 500 kutoka Manono hadi Bandari ya Kalemie ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo,” amesema Mbossa.

Amesema uwekezaji huo utafungua njia mpya ya kaskazini mashariki mwa DRC, ambapo mizigo ya madini itasafirishwa kupitia Ziwa Tanganyika hadi Bandari ya Kigoma, kisha kuelekea Bandari ya Dar es Salaam, tofauti na zamani ambapo mpaka wa Tunduma ulikuwa ukitumika.

 “Tunafungua njia mpya ya biashara ambayo itasaidia DRC kufikisha mizigo yake kwenye masoko ya kimataifa kupitia Tanzania,” amesema.

Mbossa amesema kampuni hiyo tayari imetengeneza meli nne za mizigo ambazo kila moja ina uwezo wa kubeba tani 2,000 kwa safari moja, zikiwa na urefu wa mita 70 na upana wa mita 15.

Amesema kampuni hiyo inatarajia kutengeneza meli nyingine mbili, huku Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tashico) ikiendelea na mpango wa kuongeza uwezo wa kutengeneza meli nchini.

Amesema meli hizo nne zitaongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa usafirishaji katika Ziwa Tanganyika, ambalo kwa sasa lina meli kubwa nne za mizigo.

“Kuna meli kubwa nne sasa, tatu zina uwezo wa kubeba tani 2,000 na moja tani 3,000. Kuongezeka kwa meli nne kutafanya kuwa na meli nane, hivyo kuongeza uwezo wa kusafirisha mizigo kutoka Congo kuja Tanzania na maeneo mengine,” amesema.

Mbossa amesema mbali na ongezeko la meli, Serikali pia inaendelea kuboresha Bandari ya Kigoma ili kujiandaa na ongezeko la mizigo.

Amesema mradi wa ukarabati wa gati lenye urefu wa mita 310 unaendelea, ambapo mita 190 zinafanyiwa kazi huku mita 120 zikiwa zimefungwa ili kuruhusu shughuli nyingine kuendelea na kuhudumia wananchi.

Rais Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa meli nne za mizigo zitakazo hudumu katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.

Baada ya kukamilika kwa mradi huo, amesema uwezo wa Bandari ya Kigoma utaongezeka kutoka kuhudumia tani 800,000 za mizigo kwa mwaka hadi tani milioni mbili.

Amesema pia kina cha bandari kitaongezwa kutoka mita 3.5 hadi mita 6 ili kuruhusu meli kubwa kutia nanga, huku gati jipya la kisasa la abiria lenye urefu wa mita 170 likijengwa.

“Gati la abiria litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 400 kutoka uwezo wa sasa wa watu 40. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2027,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema meli hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha usafiri wa majini na kutumia fursa za kibiashara zinazopatikana katika nchi jirani.

Amesema meli hizo zilizojengwa na Golden Logistics Company Limited zitasaidia kurahisisha usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na DRC pamoja na nchi nyingine zinazozunguka Ziwa Tanganyika.

Amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa karakana ya Tashico, ambapo mkandarasi tayari amepatikana na amelipwa dola za Marekani milioni 8.8 kama malipo ya awali, huku bado wakidai dola 8.8 milioni kama malipo ya kumalizia.

“Mkandarasi wa ujenzi wa meli nyingine ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 kutoka Kigoma kwenda DRC amepatikana na taratibu za kumpatia malipo ya awali zinaendelea,” amesema.

Amesema uwekezaji huo utaongeza ajira kwa Watanzania, kuchochea biashara katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa, pamoja na kuongeza mapato ya Serikali kutokana na kuongezeka kwa shughuli za usafirishaji na biashara.