Mfumo wa GePG ulivyoziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali

Friday February 12 2021
MFUMOPIC
By Elias Msuya

Tangu Julai mosi Serikali ilipoanza kukusanya mapato yake yasiyo ya kodi kwa mfumo wa kidijitali (GePG), mianya mingi iliyokuwa inavujisha mapato imezibwa.

Kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo huo, Serikali ilikuwa inakusanya wastani wa Sh800 bilionikwa mwaka lakini sasa hivi, mapato hayo ni zaidi ya Sh2.1 trilioni.

Wakati unaanza, mfumo huo ulikuwa na taasisi saba ambazo zimeongezeka mpaka zaidi ya 670 huku lengo likiwa kuzifikia taasisi na mamlaka zote za umma.

Akiuzungumzia mfumo huo, mchumi mwandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Neema Maregeli anasema makusanyo ya baadhi yameongezeka kwa kiasi kikubwa.

Anatoa mfano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambao makusanyo yake yameongezeka kutoka Sh95 bilioni hadi Sh115 bilioni kwa mwaka baada ya kuanza kutumia mfumo huo wakati Wakala wa Vipimo (WMA) ukiongezeka kutoka Sh1 bilioni mpaka Sh2.5 bilioni kwa mwezi.

Pia anasema kuna Neema pia alisema zipo taasisi zilizopunguza gharama zilizokuwa zinawalipa mawakala waliokuwa wanakusanya fedha za umma.

Advertisement

“Shirika la Umeme (Tanesco) lilikuwa likilipa zaidi ya Sh38 bilioni kwa mwaka kwa mawakala wa kuuza umeme lakini baada ya kufunga mfumo wa GePG kwa sasa shirika halilipi chochote,” anasema Neema.

GePG inavyofanya kazi

Kwa kutumia mfumo huu, mapato ya Serikali sasa yanalipwa kupitia namba ya kumbukumbu (control number) kwani hakuna fedha taslimu inayopokelewa.

Kwa namba ya kumbukumbu anayopewa mteja, mkurugenzi wa idara ya mifumo usimamizi wa fedha wa wizara hiyo, John Sausi anasema fedha hupelekwa kwenye akaunti ya taasisi husika lakini ikionwa na Serikali nzima.

“Fedha zinalipwa kupitia benki au mtandao wa simu kutoka vyanzo tofauti. Kwa kila Shilingi inayoingia, Serikali inajua na kuona tofauti na ilivyokuwa zamani,” anasema Sausi.

“Mfumo hutoa muda wa kulipia huduma husika, ukipita huwezi kulipa. Ni muhimu kufahamu hili ili kupunguza uwezekano wa kulaghaiwa,” anasema Sausi.

Licha ya Serikali kujua kiasi kinachokusanywa kwa kila sekunde, Sausi anasema inapata mapato hayo kwa wakati.

Zamani, anasema wakala mfano benki alikuwa anakusanya fedha na alikuwa anaweza kukaa nazo kwa muda kabla ya kuzipeleka serikalini. Jambo hilo, anasema lilikuwa linailazimu Serikali kwenda kukopa ili kugharamia shughuli zake.

Licha ya mikopo hiyo inayolipwa kwa riba kuongeza gharama, anasema hata mawakala nao walikuwa wanalipwa kamisheni iliyokuwa inapunguza mapato husika.

“Hayo yote yameondoka sasa. Mfumo umetengenezwa na wataalamu wa ndani na una ulinzi wa kutosha. Kila mwananchi anayelipa serikalini, asikubali kutoa fedha taslimu,” anasema mkurugenzi huyo.

Unavyowanufaisha wananchi

Manufaa ya mfumo wa GePG yanaonekana kuanzia kwenye taasisi za Serikali ambazo zimeondoa kabisa gharama za kukusanya mapato yake.

Kamishna msaidizi mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Christopher Mtibili ambaye ni mkaguzi wa ndani wa hesabu anasema kabla ya kuanza kutumia GePG walikuwa wanakusanya kati ya Sh100 bilioni mpaka Sh200 bilioni kwa mwaka lakini baada ya kufungwa kwa mfumo huo, mapato yameongezeka sana.

“Mwaka jana, kabla ya corona tulikuwa tumekusanya Sh360 bilioni. Mwanzoni ilikuwa inatugharimu kati ya Sh1 bilioni hadi Sh3 bilioni kuwalipa mawakala waliokuwa wanakusanya fedha hizo,” anasema Mtibili.

Wakati mapato yanaongezeka, ofisa mwandamizi wa mifumo ya Tehama wa shirika hilo, Boniface Mariki anasema mwanzo walikuwa na zaidi ya akaunti 100 za kukusanya mapato lakini sasa zimebaki nane tu zikiwamo nne za Shilingi na nne za dola ya Marekani.

“Kabla ya mfumo tulikuwa tunakusanya mapato kwenye mageti ya hifadhi zote 22 za Taifa. Huko kote tulikuwa tunawalipa mawakala,” anasema Mariki.

Ukiacha Tanapa, mkuu wa kitengo cha Tehama wa Mamlaka ya Maji mkoani Arusha (Awusa), Ndaki Tito anasema kwa sasa wanakusanya Sh1.6 bilioni kwa mwezi kutoka wastani wa Sh1.2 bilioni walizokuwa wanapata kabla ya mfumo huo.

“Mfumo umerahisisha ulipaji wa ankara na kuongeza imani ya wateja. Kasi ya ulipaji imeongezeka sana,” anasema Ndaki.

Licha ya kuimarisha ukusanyaji mapato, mfumo huo unawagusa wananchi wa kawaida pia. Mhasibu wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Said Ngonyani anasema kwa sasa mzazi anatumiwa namba ya kumbukumbu na kumlipia mwanaye ada na gharama nyingine za chuo.

“Kuna baadhi ya wanafunzi sio waaminifu, huwadanganya wazazi au walezi wao kuwa wameibiwa au kupoteza fedha ili wapewe nyingine lakini kwa mfumo huu, mwanafunzi anapewa hela yake ya matumizi tu kwani malipo anayafanya mzazi. Hakuna udanganyifu tena,” anasema Ngonyani.

Baadhi ya wananchi waliowahi kulipia huduma tofauti serikalini wanasema mambo yamebadilika kwa kiasi kikubwa.

Mwanahawa Athuman, mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam anasema hata kwa malipo madogo, fedha zinakusanywa kidijitiali.

“Nilipoenda kuchukua cheti cha kuzaliwa cha mwanangu, nililipa kwa control number. Sio fedha nyingi lakini nilipewa hiyo namba nikalipa kwa Tigopesa,” anasema Mwanahawa aliyejifungua mwanaye mwishoni mwa mwaka jana.

Aina za malipo

GePG inaruhusu aina tatu za malipo kutegemeana na huduma husika. Aina ya kwanza, Sausi anasema wapo wanaoruhusiwa kulipa kidogokidogo ndani ya muda waliopewa mpaka deni husika litakapoisha.

Kundi hili linawahusisha wateja wa huduma za maji safi kwa mfano pamoja na huduma nyingine.

Wengine, anasema wanatakiwa kulipa kiasi chote ambacho hakibadiliki ndani ya muda waliopewa. Iwapo wataingiza kiwango kidogo kuliko kinachotakiwa, anasema mfumo hautayakubali malipo hayo.

Na aina ya mwisho ni malipo yanayobadilika mfano faini ya makosa ya usalama barabarani ambayo huongezeka kadri mteja anavyochelewa kulipa.

“Mfumo haupokei malipo chini ya kiasi kilichokadiliwa lakini unakubali kiasi kilichozidi. Mteja akizidisha anaweza kudai kiasi kilichozidi ili arudishiwe,” anasema Sausi.


Advertisement