Mianzi kukuza uchumi wa Tanzania, mkakati wa kumega Sh18 trilioni waundwa

Muktasari:

  • Zao la mianzi kwa sasa linatajwa kuwa na thamani ya soko ifikayo Dola bilioni 7 (Sh17.81 trilioni) kwa mwaka duniani kote na sasa, takribani watu bilioni 2.5 kutoka Bara la Asia, Afrika na Amerika ya Kusini wanatumia zao la mianzi kwa matumizi mbalimbali.

Miaka michache ijayo Tanzania inatarajiwa kuingia kwenye idadi ya nchi duniani ambazo sehemu ya ukuaji wa uchumi utakuwa unategemea zao la mianzi ambalo kwa sasa lina uhitaji mkubwa kwenye masoko ya nje.

Takribani watu bilioni 2.5 kutoka Bara la Asia, Afrika na Amerika ya Kusini wanatumia zao la mianzi kwa matumizi mbalimbali.

Zao hilo kwa sasa linatajwa kuwa na thamani ya soko ifikayo Dola bilioni 7 (Sh17.81 trilioni) kwa mwaka duniani kote na sasa Tanzania inataka kuwa sehemu ya mzunguko huo wa fedha ambao unaweza kuchochea ukuaji wa uchumi.

Pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi, tafiti duniani zinaonyesha kuwa zao hilo linaongoza kwa unyonyaji wa hewa ya ukaa kuliko mti wowote duniani kwa takriban asilimia 40.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Mianzi na Rattan (INBAR) na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Delft, nchini Uholanzi, shamba la mianzi linaweza kuhifadhi tani 401 za kaboni kwa hekta (kwa ekari 2.5).

Hivyo basi ili kuhakikisha fursa inachangamkiwa, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilizindua mkakati wa kitaifa wa mianzi na mpango kazi wake wa Mwaka 2023 -2031.

Taarifa mbalimbali zinaeleza kuwa mianzi inahitajika zaidi kwenye taifa la China na nchi nyingine, hususan za bara la Asia kwa ajili ya kutengeneza samani za ndani, ujenzi, urembo na biashara ya kaboni.

Wataalamu wa masuala ya misitu nchini wanasema zao hilo linaweza kustawi popote katika ardhi ya Tanzania, hivyo wanashauri elimu zaidi utolewe kwa wananchi ili waweze kuzitambua fursa mbalimbali zitokanazo na mianzi ili waweze kuinua uchumi wao.

Mkakati huo wa miaka nane, unalenga kuhamasisha kilimo biashara cha mianzi katika mashamba makubwa, kwani kwa Tanzania bado hakifanyiki na hata mianzi iliyopo hailimwi kibiashara.

Wadau wanaamini kwamba ulimaji wa mianzi kibiashara utainufaisha Serikali, sekta binafsi hususan katika mauzo ya nje na biashara ya kaboni ambayo inakuwa maarufu katika ulimwengu wa sasa.

Katika miaka nane ya utekelezaji wake mkakati unalenga kuongeza soko, kukuza matumizi ya bidhaa endelevu za mianzi nchini, kutengeneza viwango vya ubora.

Akizindua mkakati huo mwanzoni mwa wiki hii, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki alisema kupitia mianzi nchi itaweza kupata kodi na kuongeza fedha za kigeni pamoja na upandaji na utunzaji wa mianzi, wananchi watapata huduma muhimu za kijamii, kujiongezea kipato na ajira za kudumu.

"Tunapoteza takriban hekta 469,000 za eneo la msitu kila mwaka. Hali hii si nzuri kwa sababu iwapo juhudi za pamoja hazitachukuliwa, basi kasi ya kuenea kwa jangwa itaongezeka, itaathiri nchi yetu na hatimaye kuchangia kuathiri dunia,” anasema.

Anasema Serikali inaweka mazingira wezeshi kwa wadau wote wa zao la mianzi ili kuhakikisha linaleta tija kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Kairuki anasema iwapo mpango kazi huu utatekelezwa ipasavyo utawezesha kuendeleza uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu ya zao la mianzi kwa maendeleo endelevu katika sekta nyingine.

Kamishna wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Misitu Nchini (TFS), Profesa Dos Santos Silayo anasema mkakati huo unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 50 duniani zinazotumia mianzi kama mmea wa faida.

Anasema kwa mkakati huo uzalishaji wa mianzi utaongezeka huku akiongeza kuwa, tayari kuna mashamba saba yametengwa kwa ajili ya upandaji wa zao hilo lenye thamani ya matrilioni ya shilingi duniani.

“Katika mkakati huu baada ya kukamilika, tunatarajia kuwa na jumla ya hekta 10,000 za mashamba ifikapo Juni 2031 pamoja na bustani mbili za mbegu za mianzi,” anasema Dos Santos.

Aliongeza mianzi ni mti aina ya nyasi ambao hustawi kwa muda mfupi, una manufaa mbalimbali ambayo yanasaidia kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla, hivyo utekelezaji wa mkakati huu utaiweka nchi kwenye ramani ya dunia.

Wasemacho wadau

Mtaalamu wa misitu na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kuilimo (Sua), Dk Paulo Lyimo anasema mianzi ina manufaa mengi, ikiwemo kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi, kutengeneza bidhaa mbalimbali za ujenzi, samani za majumbani na urembo.

Changamoto iliyopo kwenye jamii ya Tanzania ni uelewa juu ya zao hili, kwani walio wengi wanafahamu kuwa mianzi hutumika kwa ajili ya kutengeneza pombe, samani na fimbo za kuchapia ndio sababu limeachwa.

"Nchi za Asia kama China zinafanya biashara kubwa na kuuza kaboni kupitia mianzi, pia inatumika kwa ajili ya ujenzi, badala ya nondo wanachanganya na teknolojia nyingine, uhitaji wa zao hilo kwenye soko hilo lenye takribani watu bilioni moja ni mkubwa, hivyo tunahitaji kuweka mkazo ili nchi iweze kunufaika," anasema.

Dk Lyimo anaongeza, tafiti zinaonyesha zao hili lina uwezo kustawi kwenye ardhi yoyote hapa nchini, hivyo kuna haja ya wawekezaji kuona fursa hii na kuifanyia kazi, pia huchukua takribani miaka mitatu mpaka mitano hadi kuvunwa kwake tofauti na miti mingine.

Endapo mkakati huu ukitekelezwa vyema, miaka michache ijayo Tanzania itaingia kwenye ramani ya nchi zinazouza mazao ya mianzi kwenye masoko ya nje na kuongeza pato la taifa.

Kuhusu mianzi

Mwanzi ni jina la spishi nyingi za nyasi ndefu zinazoweza kuonekana kama miti. Mianzi yote huwa na shina aina ya ubao.

Mianzi hupatikana kiasili katika bara la Afrika, Amerika na Asia, lakini inastawi pia ikipandwa barani Ulaya.

Urefu wa spishi kubwa hufikia kina cha mita 40. Inaweza kukua zaidi ya mita 1 kila siku, lakini kwa kawaida ni sentimita 3-5 kwa siku.

Shina la mianzi huwa na umbo la bomba na unene wake ni hadi sentimita 30. Shina hugawiwa na vifundo. Kila kifundo kina chipukizi na machipukizi yanaweza kuendelea kuota matawi.

Matumizi ya mianzi ni kwa ajili ya ujenzi na mashina yake hutumika pia kwa mabomba ya maji katika nyumba na kilimo.

Wakati mianzi ikiwa michanga na laini, yaani kabla ya kuwa ubao inafaa kama chakula baada ya kupikwa, lakini pia matovu yake yakikusanywa na kusindikwa hutumiwa kama kinywaji cha ulanzi.