Minara 758 yazinduliwa, wananchi milioni 8.5 kunufaika na mapinduzi ya mawasiliano
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akisaini Hati ya Makabidhiano kati ya Serikali na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yas Tanzania Pierre Canton-Bacara (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Charles Kamoto wa kwanza (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mtandao wa Kampuni ya Vodacom Tanzania Andrew Lupembe katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma Aprili 10, 2026.
Muktasari:
- Rais Samia asema mawasiliano si tena huduma ya anasa kama ilivyokuwa zamani, bali ni uti wa mgongo wa uchumi wa kisasa na daraja la fursa kwa wananchi katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Dar es Salaam. Serikali imezindua minara 758 ya mawasiliano iliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayotarajiwa kuondoa changamoto za mtandao kwa zaidi ya wananchi milioni 8.5, hususan wanaoishi vijijini na katika maeneo ya mipakani.
Uzinduzi huo uliofanyika leo, Aprili 10, 2026, jijini Dodoma, ulienda sambamba na kuunganisha huduma za mkongo wa Taifa wa mawasiliano katika wilaya 85, jambo linaloashiria hatua mpya katika juhudi za Serikali za kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema uwekezaji huo umetokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano kwa lengo la kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi kwa ubora unaokidhi mahitaji ya teknolojia ya kisasa na kwa gharama nafuu.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo kutachochea ushiriki mpana wa wananchi katika uchumi wa kidijitali, sambamba na kufungua fursa mpya za ajira, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya Taifa.
“Mawasiliano si tena huduma ya anasa kama ilivyokuwa zamani. Leo hii ni uti wa mgongo wa uchumi wa kisasa na daraja la fursa kwa wananchi katika nyanja mbalimbali za maendeleo,” amesema Rais Samia.
Kutokana na umuhimu huo, Rais Samia amewataka wadau wa sekta binafsi kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kuhakikisha uwekezaji huo unaleta manufaa makubwa kwa vijana.
Amesema wizara hiyo, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana pamoja na wadau wengine wa sekta ya teknolojia, wanapaswa kuhakikisha vijana wananufaika ipasavyo na huduma za mkongo wa Taifa wa mawasiliano, hasa katika kukuza ubunifu, ujuzi wa kidijitali na kuongeza fursa za ajira.
“Uwekezaji huu kwa vijana ni muhimu kwa sababu dunia ya teknolojia ni yao. Dunia hii ipo viganjani mwao na ndiyo mfumo wa maisha yao. Ni lazima tuwawezeshe na kuwahamasisha kutumia mifumo hii ili waweze kukua kiuchumi na kijamii,” amesema.
Rais Samia amesema Serikali pia itatenga fedha zitakazowezesha wizara hiyo kusaidia kampuni changa za vijana kupata mitaji ili ziweze kukua na kuchangia zaidi katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
Amesema teknolojia ya habari na mawasiliano imekuwa sekta ya kimkakati inayochochea ukuaji wa ajira, kuongeza tija katika uzalishaji na kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rais Samia amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo mkongo wa Taifa wa mawasiliano ambao unaunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara na wilaya nyingi nchini.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo pia kutasaidia kuondoa changamoto kwa wananchi wa maeneo ya mipakani ambao awali walilazimika kutumia mitandao ya simu ya nchi jirani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Tuzo Mkurugenzi wa Mtendaji wa Kampuni ya Yas Tanzania Pierre Canton-Bacara kwenye hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma Aprili 10, 2026.
“Kwa muda mrefu baadhi ya wananchi katika maeneo ya mipakani walikuwa wakipata huduma za mawasiliano kutoka nchi jirani. Hatua hii ni ukombozi mkubwa kwao kwa sababu sasa watapata huduma kupitia mifumo ya mawasiliano ya Taifa lao,” amesema.
Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha miundombinu ya mkongo wa Taifa inalindwa na kutunzwa ipasavyo kwa kuwa ni mhimili muhimu wa uchumi na usalama wa Taifa.
Pia, amesisitiza kuwa huduma za mawasiliano nchini zinapaswa kuzingatia maadili, mila na tamaduni za Watanzania ili kulinda kizazi kijacho dhidi ya athari za matumizi mabaya ya teknolojia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso, amesema ujenzi wa minara hiyo ni hatua muhimu, lakini pia ni muhimu kuhakikisha changamoto za mawasiliano zinaondoka kabisa kwa wananchi.
Amesema wananchi wengi wangependa kuona minara inayojengwa inatumiwa na kampuni zote za mawasiliano ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bila kujali mtandao anaotumia mteja.
“Kwa teknolojia ilivyo sasa, mnara mmoja unaweza kutoa huduma kwa kampuni zote za mawasiliano. Watoa huduma wakiacha ubinafsi, tunaweza kuwafikia Watanzania wengi zaidi na minara hii ikaleta manufaa makubwa,” amesema Kakoso.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema mradi wa ujenzi wa minara 758 ulianza Mei 13, 2023, baada ya mfuko huo kukabidhiwa jukumu la kusimamia utekelezaji wake.
Amesema mradi huo ulitekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 126, ambapo Sh bilioni 55 ni mkopo kutoka Benki ya Dunia kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali na Sh bilioni 71 ni fedha za ndani kupitia UCSAF.
Kwa mujibu wa Mwasalyanda, mradi huo ulitekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na kampuni za mawasiliano nchini, ambapo Serikali ilitoa ruzuku ili kuchochea uwekezaji katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Katika mgawanyo wa ujenzi wa minara hiyo, kampuni ya Yas ilijenga minara 261, Vodacom 190, Airtel Tanzania 169, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) minara 104 na Halotel minara 34.
Aidha, amesema mradi wa kuongeza nguvu kwenye minara 304 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G ulikamilika Machi 2025, hatua inayolenga kuboresha ubora wa huduma za mawasiliano kwa wananchi.