Mpango wa Magufuli kwa wafanyabiashara

Monday March 29 2021
wafanyabiashara pc

Mmoja ya wafanyabiashara akichangia hoja wakati wa mkutano na aliyekuwa Rais wa Tanzania, marehemu John Magufuli.

By Mwandishi Wetu

Mara tu baada ya kuapishwa, Novemba 5 mwaka 2015, Rais John Magufuli alikutana na wafanyabiashara ikulu jijini Dar es Salaam. Hili ndilo kundi la kwanza kuzungumza nalo tangu aliposhika nafasi hiyo ya juu katika utumishi wa umma.

Rais Magufuli alikutana na wafanyabiashara hao Desemba 3 mwaka 2015, akarudia tena Machi 2018 halafu Juni 2019. Mara zote alisikiliza kero wanazokutana nazo na kupokea maoni yao juu ya maboresho wanayoyataka katika maeneo tofauti.

Ni mikutano hiyo iliyomshawishi Rais Magufuli kufuta takriban kodi na tozo 200, zikiwamo 105 za sekta ya kilimo ili kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kwa lengo la kuongeza tija.

Licha ya kufuta baadhi ya tozo na kodi zisizo rafiki, aliielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupunguza viwango vinavyotozwa mfano kwenye nyumba ili wengi wajitokeze kulipa pamoja na kuwaondoa wenye mtaji usiozidi Sh4 milioni.


Uchumi wa viwanda

Advertisement

Rais alitaka Tanzania iwe na uchumi mkubwa utakaoiruhusu kutoa msaada kwa mataifa mengine yasiyojiweza, hivyo falsafa yake ikawa ujenzi na uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.

Wakati wote alizitaka wizara na mamlaka za usimamzi kuweka mazingira wezeshi ya kuanzisha na kuendeleza viwanda nchini

Mkurugenzi wa DAE Group of Companies wilayani Mbinga, Danstan Komba anasema Rais Magufuli alikuwa karibu sana na wafanyabiashara, jambo lililowaongezea ari ya kuwekeza.

“Muda wote alipigania na kuhamasisha uwekezaji kwenye viwanda, hili linapaswa kuendelezwa. Kwenye mikutano tuliyokutana naye tulikuwa tunatoa kero na kuwasilisha maoni yetu ambayo yalifanyiwa kazi. Nitaendelea kumkumbuka kwa hilo,” anasema Komba.

Katika uongozi wake, Rais Magufuli alitaka kuona wawekezaji na wafanyabiashara bila kujali ni wakubwa au wadogo, wanafanya shughuli zao kwa uhuru na tija.


Utekelezaji wa blueprint

Kwa miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa inashuka kwenye viwango vya urahisi wa ufanyaji biashara vinavyotolewa na Benki ya Dunia kila mwaka kutokana na sababu nyingi zilizopo, hasa kwenye mamlaka za usimamizi.

Kwa kulitambua hilo, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) iliandaa mwongozo wa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini (blueprint) ambao mapendekezo yake yalianza kufanyiwa kazi mwaka 2016.

Mkurugenzi mtendaji wa TPSF, Francis Nanai anasema sio tu Rais aliipenda sekta binafsi kwa kuhakikisha anakutana nayo na kupokea maoni yao, bali aliweka misingi imara ya uwekezaji na biashara na akahakikisha anawekeza vilivyo kwenye miundombinu ya usafirishaji, umeme na huduma. “Alipozindua Bunge, aliahidi kutoa ajira milioni nane akiamini sekta binafsi itashiriki kwa kiasi kikubwa kufanikisha hilo. Alitamani kuwaona Watanzania wanakuwa mabilionea,” anasema Nanai.

Pamoja na mambo mengi aliyoyafanya kuimarisha misingi nchini, Magufuli hakutaka kuiona Tanzania inabaki nyuma kimataifa, hivyo alihakikisha inajipanga vyema kushindana.

Kwa miaka sita aliyodumu ikulu, Dk Magufuli alisisitiza uadilifu katika ulipaji kodi, huku akihamasisha kulinda rasilimali za umma.

“Rais alihamasisha matumizi ya sayansi na teknolojia serikalini ndio maana kuna Serikali mtandao na malipo ya kidijitali,” alisema Nanai.

Ni katika uongozi wa Rais Magufuli Serikali ilipokea maoni ya mpango wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara (blueprint) uliopelekwa bungeni na kuwekewa utaratibu wa utekelezaji.


Tanzania kimataifa

Wakati wote Rais Magufuli aliilinda Tanzania na rasilimali zake. Hili alilifanya kuanzia kwenye kilimo, madini mpaka lugha. Ni katika kipindi cha uongozi wake Kiswahili kimekuwa miongoni mwa lugha rasmi za Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Kwenye mazishi ya kitaifa yaliyofanyika jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi alisema Rais Magufuli amefungua ofisi mpya nane za ubalozi. Dk Magufuli aliwataka mabalozi wote kuhamasisha diplomasia ya kiuchumi ili Tanzania inufaike na fursa zilizopo kwenye mataifa wanakoiwakilisha.

Katika biashara ya kimataifa, Magufuli alitaka bidhaa zinazosafirishwa ziongezewe thamani kwanza nchini ili kutoa ajira kwa wazawa, hivyo kupata bei kubwa itakayokuwa na tija zaidi.

Alisitisha usafirishaji wa makinikia mwaka 2017 na kuagiza vijengwe viwanda vya kuchenjua madini nchini na akabadili sheria ya madini ili kuongeza ushiriki wa wananchi. Alijenga ukuta Mirerani kuzuia utoroshaji wa Tanzanite.

Katibu wa Chama cha Wasafirishaji wa Bidhaa kwenda Nje ya Nchi Zanzibar, Khamis Issa Mohammed anasema chini ya uongozi wa Dk Magufuli mengi yenye manufaa yamefanyika.

“Mimi ni msafirishaji wa spicies (viungo vya chakula), Zanzibar ilikuwa inasifika sana zamani kwa usafirishaji wa bidhaa hizo lakini sasa bara nayo ipo juu. Taasisi kama Tantrade (Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania) zinaandaa na kuratibu uuzaji wa bidhaa nje ya nchi. Haya yote yamewezekana kutokana na utayari wa Rais,” anasema.


Miundombinu wezeshi

Kwa kutambua Tanzania inapakana na mataifa manane, yakiwamo yasiyokuwa na bandari, Rais Magufuli alijielekeza kujenga barabara za lami kuunganisha kila mkoa na wilaya nchini ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa huduma na bidhaa.

Profesa Kabudi alisema Rais Magufuli alijenga kilomita 12,961 za lami pamoja na madaraja 13 makubwa yanayosaidia kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi na wafanyabiashara.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo anasema Magufuli alikuwa Rais wa mfano Afrika Mashariki, lakini Tanzania ndiyo iliyobahatika kumpata.

“Sekta ya usafirishaji ametuneemesha zaidi. Amejenga vituo vingi vya mabasi kuanzia Dar es Salaam, Kibaha, Morogoro, Iringa mpaka Tanga. Barabara za lami zimepunguza gharama za utengenezaji wa mabasi yetu ambayo mengi ni ya Kichina yasiyohimili mikikimikiki ya barabara mbovu,” anasema Mwalongo.

Kuhakikisha inakuwa rahisi kupeleka bidhaa nje ya nchi na kuwaleta watalii, Rais Magufuli alilifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) sambamba na kuboresha viwanja vya ndege katika mikoa tofauti.

Advertisement