Mradi wa kubadili gesi kuwa dizeli mbioni kutekelezwa Tanzania
Muktasari:
- Mradi huo unasimamiwa na kampuni ya Canada ya Rocky Mountain GTL kwa kushirikiana na mshirika wake wa Afrika, Memnon Africa, pamoja na kampuni ya ndani ya Rithi Tanzania Group Limited.
Dar es Salaam. Tanzania iko mbioni kuanza utekelezaji wa mradi wa kubadili gesi asilia kuwa dizeli, mafuta ya ndege na bidhaa nyingine za nishati, baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mradi huo.
Kutokana na hatua hiyo, kinachosubiriwa sasa ili kuanza utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya Dola milioni 420 za Marekani (zaidi ya Sh1.1 trilioni), ni makubaliano ya uhakika wa upatikanaji wa gesi kutoka kwa Serikali.
Mradi huo unasimamiwa na kampuni ya Canada ya Rocky Mountain GTL kwa kushirikiana na mshirika wake wa Afrika, Memnon Africa, pamoja na kampuni ya ndani ya Rithi Tanzania Group Limited.
Baada ya kukamilika kwa upembuzi huo, hatua inayofuata ni kusainiwa kwa makubaliano ya usambazaji wa gesi kati ya wawekezaji hao na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), jambo litakalofungua njia ya kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho kinachopangwa kujengwa mkoani Mtwara.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, amesema makubaliano hayo hayatatekelezwa kwa haraka hadi pale shirika litakapojiridhisha kuwa kuna kiasi cha kutosha cha gesi kitakachoweza kuhudumia mradi huo bila kuathiri mahitaji mengine ya kitaifa.
Amesema kwa sasa mahitaji ya umeme nchini yameongezeka kwa kiasi kikubwa, hivyo matumizi makubwa ya gesi yameelekezwa katika kuongeza uzalishaji wa umeme.
“Tutaisaini mikataba hiyo pale tutakapokuwa na uhakika kwamba tuna gesi ya kutosha kuuwezesha mradi huo. Kwa sasa tunaona ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme na kipaumbele chetu ni kutumia gesi katika uzalishaji wa umeme,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Memnon Tanzania, Jackson Pemba, amesema teknolojia hiyo inaweza kuwa suluhisho muhimu kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika wakati wa changamoto za upatikanaji wa mafuta zinazotokana na misukosuko ya kimataifa.
Amesema migogoro ya kisiasa na kiuchumi duniani, ikiwamo vita vinavyoathiri masoko ya nishati, imeonyesha umuhimu wa nchi kuwa na uwezo wa kutumia rasilimali zake kuzalisha nishati kwa ajili ya matumizi ya ndani.
“Teknolojia hii inaweza kusaidia Tanzania na nchi nyingi za Afrika kukabiliana na changamoto za mafuta pale zinapotokea kutokana na sababu za kimataifa,” amesema.
Pemba amesema baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu, majadiliano yanaendelea kuhusu muundo wa uwekezaji na namna ya kuanza ujenzi wa kiwanda hicho Mtwara.
Kwa kutumia teknolojia hiyo ya Canada, gesi asilia ya Tanzania itabadilishwa kuwa dizeli isiyo na salfa, mafuta ya ndege, petroli na bidhaa nyingine muhimu za viwandani.
Mbali na mafuta, teknolojia hiyo pia ina uwezo wa kuzalisha hidrojeni ambayo inaweza kutumika kutengeneza amonia na hatimaye mbolea, bidhaa muhimu kwa kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo.
Pemba amesema kampuni hiyo tayari imeanza maandalizi ya kujenga kiwanda cha kwanza cha GTL chenye mfumo wa moduli barani Afrika, chenye uwezo wa kuzalisha mapipa 5,000 ya mafuta kwa siku katika hatua ya awali.
Kiwango hicho ni sawa na takribani lita milioni nane za mafuta kwa siku, kiasi kinachokaribia mahitaji ya sasa ya matumizi ya dizeli nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, uzalishaji huo unaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa uagizaji wa mafuta kutoka nje, kuongeza usalama wa nishati na hata kutoa fursa kwa Tanzania kuuza mafuta hayo kwa nchi jirani.
Tanzania ina akiba ya gesi asilia inayokadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 57.54, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitumika zaidi katika uzalishaji wa umeme na matumizi ya viwandani.
Akizungumza bungeni hivi karibuni, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Arif Premji, aliitaka Serikali kuangalia uwekezaji katika teknolojia hiyo, akisema inaweza kusaidia nchi kujikinga na changamoto za mafuta zinazojitokeza mara kwa mara duniani.
“Tumefundishwa nini na changamoto za mafuta Tanzania tangu uhuru? Tuna gesi ya kutosha ambayo inaweza kubadilishwa kuwa dizeli, na tayari kuna wawekezaji walioonyesha nia. Serikali inapaswa kuangalia teknolojia hii,” alisema.
Mradi huo sasa unasubiri uamuzi wa mwisho kuhusu upatikanaji wa gesi, hatua ambayo itaamua kasi ya Tanzania kuingia katika uzalishaji wa mafuta yanayotokana na gesi asilia.