Tanzania kuchakata mafuta machafu kuwa vilainishi
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akizungumza wakati alipotembelea Kiwanda cha Kamal Refinery kilichopo Kerege, Bagamoyo, ambapo alishughudia uhifadhi wa mazingira kupitia uchakataji wa mafuta taka yanayotumika kama malighafi muhimu ya utengenezaj wa vilainishi vya magari. Na Mpigapicha Wetu.
Muktasari:
- Serikali imesema inaona umuhimu wa kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika uchakataji wa mafuta taka ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuleta manufaa ya kiuchumi.
Bagamoyo. Tanzania itakuwa katika nafasi nzuri ya kupunguza utegemezi wa malighafi za viwandani zinazoagizwa kutoka nje, iwapo juhudi za kuchakata mafuta taka na kuyageuza kuwa bidhaa zitakamilika.
Juhudi hizo zimeelezwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alipotembelea Kiwanda cha Kamal Refinery kilichopo Kerege, Bagamoyo, kujionea shughuli za uchakataji wa mafuta taka kuwa mafuta ya vilainishi.
Amesema uwekezaji katika uchakataji wa mafuta taka una manufaa ya kiuchumi na kimazingira kwa wakati mmoja, kwa kuwa unasaidia kupunguza taka zinazoweza kuathiri mazingira, huku ukizalisha malighafi muhimu kwa viwanda.
Amesema Serikali inaona umuhimu wa kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta hiyo kwa sababu uzalishaji wa mafuta ya vilainishi nchini unaweza kupunguza uagizaji wa bidhaa zinazotokana na malighafi hiyo kwa kiwango cha kati ya asilimia 10 na 12.
“Miradi ya aina hii ina mchango mkubwa katika kulinda mazingira na wakati huohuo inachochea biashara na ukuaji wa viwanda. Hii ni fursa muhimu kwa Tanzania kuongeza thamani ya rasilimali zilizokuwa zikionekana kama taka,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamal Group, Sameer Santosh, amesema wamewekeza katika teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na rasilimali zinazopatikana ndani ya nchi.
Pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, amesema bado kuna changamoto zinazohitaji ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na Serikali ili kuongeza upatikanaji wa malighafi na kukuza ushindani wa sekta hiyo.
Meneja wa Miradi wa Kamal Refinery, Prince Mwakimenya, amesema kwa sasa kiwanda kinapokea kati ya tani 300,000 na 600,000 za mafuta taka kwa mwezi, kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji halisi ya uzalishaji.
Amesema kiwanda kinahitaji takribani tani milioni moja za mafuta taka kwa mwezi ili kufikia malengo yake ya sasa, huku mpango wa muda mrefu ukiwa ni kupanua uwezo wa uchakataji hadi tani milioni tatu kwa mwezi.
Ameeleza kuwa ongezeko la upatikanaji wa mafuta taka litawezesha uzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ya vilainishi, kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje na kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Kamal Refinery kwa sasa ni kiwanda pekee nchini kinachojishughulisha na uchakataji wa mafuta taka kuwa masafi, hatua inayotajwa kuwa mfano wa kubadili taka kuwa rasilimali yenye thamani ya kiuchumi,” amesema.